Kisha simu ingine kwa
mama Jema. Akimwambia alipo Jelini na kile Jelini alichomwambia Ezra. Kisha akawapigia wazazi wake huku na yeye
akikanyaga mafuta kuelekea alipo Jelini.
Uzuri ni kweli
hapakuwa mbali na kwa kina Ezra. Njia za mkato hata dakika 10 hazifiki.
Akaegesha gari katikati ya njia na kukimbilia vyoo vya kike. Hakubisha hodi,
akaingia na kukuta wanawake wengine humo, asijue amempita Colins hapo mlangoni
akiwa anamsubiria Jelini atoke. Akaanza kuchungulia chini ya milango akamuona
Jelini amelalia matapishi sakafuni.
Akasukuma mlango kwa
nguvu akafanikiwa kufungua akiwa amemsukuma hata na Jelini hapo sakafuni.
Alipomtingisha, Jelini alishaanza kutoa povu mdomoni. “Kweli hii ni sumu!”
Akawaza Ezra akimtoa pale akikimbia naye. Anatoka nje, na Junior naye anashuka
garini.
“Nimeita gari ya
hospitalini, wapo njiani.” “Siwezi kusubiri.” “Najua umepaniki Ezra. Lakini
hawa watu wanakuja na huduma ya kwanza kumtoa hiyo sumu hapahapa kabla
hawajamfikisha hospi…” Wakasikia gari ya wagonjwa ikija kisha mataa. Angalau
Ezra akaridhika. Bado hakuwa amemuweka chini. Akaanza kukimbia naye kulifuata hiyo
gari ya wagonjwa. Wakasimama katikati ya barabara, Jelini akiwa hana fahamu,
akapokelewa. Ezra na yeye akaingia ndani ya gari hiyo ya wagonjwa, safari
yakurudi hospitalini ikaanza huku akiwa anapewa huduma ya kwanza.
Alichofanya Junior ni
kusogeza gari ya Ezra na kuiigesha sehemu nzuri. Akaifunga na kuondoka huku
akipokea simu za kueleza kinachoendelea. “Wameshamchukua,
tunaelekea hospitalini.” Akawatajia jina la hospitali, na kuendelea
kukaza mwendo.
Mpaka anafikishwa
hospitalini akawa ametapishwa sumu yakutosha tu, ila bado hakuwa akijitambua. Kila alivyotapika,
akawa akimaliza, anazima kabisa.
Hofu ikaanza kuwangia pale alipoanza kutoa damu mdomoni.
mungu Wa Mitandao.
Huku nyuma Colins
alipoona ile hali, akaingiwa na hofu ya ajabu lakini hakuthubutu kuwafuata. Akafikiria
kwa haraka. Akajua lazima wanao husika ni kina Love ambao Jelini alishawaona
tokea mwanzo. Akaamua kuwafuata ili kuhakikisha kama ni wao, lakini hawakuwepo.
Kumbukumbu ya alichoambiwa na Jelini juu ya nguvu ya Kemi, ikapita
kichwani kwake. Na yeye bila ya kuchelewa, kwa haraka sana akaomba kuonana na
meneja.
“Mna kamera hapa?” Likawa
swali la kwanza na kwa haraka. “Baadhi ya maeneo.” “Naomba kuona.” “Unajua
hatuwezi kukuonyesha bila kibali
maalumu.” “Unatania wewe!? Mteja wenu
aliyekunywa juisi ya hapa ameondoka
hapa mahututi. Nataka kuangalia ili niwasaidie,
unakataa!?” Ile kelele ikamsogeza na
mmiliki. Bahati nzuri jioni hiyo alikuwepo.
Alishuhudia lile gari
la hospitali na fujo ya mpaka Jelini anatolewa pale. “Hivi unajua kinachokukabili?” Akamuuliza kwa ukali
haswa. “Mimi nataka kuwasaidia kabla hawajaingia kwenye mtandao wenu nakufuta ushahidi! Ukichelewa tu,
wakifuta ushahidi, ujue utafia jela.” Akamkimbiza chumba chenye kompyuta na
vivaa vyakutunza kumbukumbu za kamera za ulinzi.
Zimefika (40)
Colins alipofanikiwa
kuingia tu kwenye mitambo ya hapo, akagundua kuna mtu mwingine naye upande wa
pili, anajaribu kuingia hapo.
Akawaonyesha. “Unaona huyu, anahangaika kuingia kwenye mtandao wako, kufuta
ushahidi wa kile cha kweli kilichompata mteja wako.” Colins alihakikisha anamuelewesha
jukumu lake kama mmiliki wa ile hoteli. Kwa hakika walishituka sana.
“Tafadhali tusaidie.”
Colins akaanza kazi. Viwanja vya nyumbani! Wamegusa TENA penzi lake!
Akakusudia kulipiza kisasi haswa.
Kwanza kabisa, akaweka
security ngumu mpaka akafanikiwa kumzuia
au block yule mtu upande mwingine ambaye alijua kwa hakika atakuwa ni Kevin
Kasa. Kisha akamtumia ujumbe mfupi kwa barua pepe. ‘Hilo
ni kosa ambalo sitakusamehe, Kevin.’ Ikawa kama amemwambia nakujua
wewe ni nani na nimekufikia.
Maana alimtumia kwa email
yake kabisa lakini ambayo si kwamba ina jina lake Kevin Kasa, kwamba Colins
amejua kirahisi. Hapana. Alimtumia kwa email yake anayotumia kwenye
mambo yao hayo ya mtandaoni, yenye nicknames zao za huko mitandaoni,
majina ambayo hayana hata herufi za majina yao.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kevin alivyopata ule
ujumbe, alishituka akasimama kwa haraka karibu atupe kompyuta. Akajua wazi
ameingia kwenye anga za Guru. Yupo vitani na akajua alivyotumwa na dada
yake safari hii pia ni kikubwa zaidi, na mbaya zaidi, kinamuhusu Guru Colins
ambaye mpaka hapo ameshamshinda. Akajua kwa hakika dada yake yupo
matatani. Alichotaka kifutwe safari hii, kipo kwenye mikono sahihi, hatapona.
Akampigia. “Umefanikiwa?” Likawa swali la kwanza kutoka kwa dada
yake. “Umefanya nini tena Kemi!?” “Acha
kunihoji. Nakuuliza umeshafanikiwa?” “Safari hii nahisi umecheza pabaya. Kama
ni jambo hatari, nakushauri kimbia usiku huuhuu, nenda hata Nairobi, kesho
ukimbilie kwa mama moja kwa moja.” “Acha
kunitisha wewe! Fanya kazi yako.”
“Hakika
safari hii ondoka na usirudi Kemi. Inavyoonekana umeingia vitani na
Colins. Yaani pale kwenye ile kampuni tunapofanya kazi, anajulikana kama mungu
wa ile kampuni na mpaka leo hawajaziba pengo lake. Hapa tunapozungumza,
amefungia ile system nzima, nina uhakika hata umpigie nani simu umuombe
msaada, hataweza kuingia.”
“Na mbaya
zaidi amejua kama ni mimi ndiye nimejaribu kuingia kule kutaka kufuta. Maana
amenitumia ujumbe kwenye email yangu ya siri, ambayo wanajua watu
wachache sana. Na amenitambua kabisa kwa jina langu kamili, mpaka nimeogopa!
Umefanya nini tena Kemi!? Na kwa nini unapenda kuniingiza kwenye matatizo yako
kila wakati?! Kwa nini unataka niangamie na wewe?” Kemi akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Colins akaendelea kufanya
yake mpaka akakamilisha kulitenga na kulitengeneza lile tukio zima vizuri na
kifasaha. Tena katikati ya hiyo video, akarudiarudia kuzitengeneza
vizuri zile sehemu maalumu kuweka msisitizo. Akajitumia yeye na James
kama kujihami.
‘Tafadhali naomba
unielewe James na umueleweshe Ezra. Nilimuomba Jelini kikao kwa heshima kabisa
ili na yeye asikie upande wangu, asiishie kuniona nitapeli. Niliyemuacha
njia panda na kuhamia kuishi na Love, kama muhuni tu na kumdharau yeye kwa kumtelekeza.
Najua na wewe unajua, anastahili kusikia ukweli kuliko kumuacha na maumivu ya usaliti.’
‘Sasa kilichoendelea
hata hapo kwenye video utaona ni mazungumzo sehemu ya wazi kabisa, nikimwambia
upande wangu na mimi kile kilitokea siku ile nikiwa napanga kwenda kwao na
nikiwa na nia ya kumuoa kabisa na si kumpotezea muda. Nampenda Jelini na nilikuwa
tayari kuishi na kumkuza Jeremy kama kijana wangu.’
‘Tafadhali angalia
hiyo video kwa makini sana. Ndio ukweli halisi wa kilichompata Jelini
usiku wa leo tulipokuwa pamoja. Nimewahi kabla kina Kasa hawajafuta. Maana
nimemkuta na kumblock Kevin akiwa ameshaingia kwenye mtandao wa hii
hoteli akijaribu kufuta kama tukio la kwanza walilomfanyia Jelini ofisini
kwa baba yao na kumjeruhi vibaya sana.’
‘Ila Jelini
alificha hakutaka kuwaambia nyinyi. Ila Kevin anahusika kwenye kupoteza
ushahidi hata na kwenye tukio la kwanza alilosababisha huyo Kemi ambalo na leo
utagundua amehusika na kuweka sumu kwenye kinywaji cha Jelini, akisaidiana na
Love. Ila nakuahidi kuipata na hiyo video ya kwanza aliyofuta Kevin ofisini kwa
baba yao. Nitakutumia nikishaipata.’
‘Najua kwa
sasa ‘samahani’ haitasaidia, ila hii hoteli ni chaguo la Jelini mwenyewe
akitaka tukutane hapa, tuzungumze. Sikupachagua mimi. Na mimi sikuwaona Love na
Kemi, wameshakimbia hapa. Utaona kwenye video wakiondoka.’
Akamtumia na huo
ujumbe kama akijitetea lakini alijua wazi, hakuna anayetaka kumsikia. Na
alifanya bila ya kuwaambia hapo.
Ukweli Wa Kilichompata Jelini.
Alipokamilisha hilo ndipo
akawaita wenyeji wake, ili na wao waone. Maana walibaki hapo ndani ya hicho
chumba, hawajui chakufanya, roho mkononi, wakimsubiria amalize. “Sasa nimekutolea
tukio zima. Maaana mama wa yule binti mimi namfahamu.
Jiandae na kujipanga ukiwa na huu ushahidi.
Na uwe na maelezo yakutosha, lasivyo, atakuchomea
hii hoteli nzima mpaka iteketee.”
Akaendelea akiwa ameshawatisha zaidi.
“Na wakati
ukijipanga, omba yule binti apone.
Ndio itakuwa pona yako hata utaweza kumsogelea mama yake. Ila mimi ningekuwa
wewe, ningejiwahi mapema sana.” “Mbona kama unatupa lawama kwangu moja kwa moja wakati hoteli yangu haihusiki? Kama alikuja hapa na ugonjwa
wake!” Akawahi kujitetea. “Njoo nikuonyeshe kilichotokea mpaka kufikia yule
binti kukimbizwa hospitalini.” Akafungua ile video.
Mwanzoni
kabisa akaonekana yule muhudumu anapita. Akasimamishwa kwenye meza ya kina
Kemi, Love na wanaume wengine watatu. Ikaonekana kama Kemi amemuuliza kitu.
Akaonekana baada ya kujibu yule muhudumu akaondoka.
Kisha
baada ya hapo Kemi na Love wakajadiliana kitu, nakuondoka pamoja pale hotelini.
Colins alifanikiwa mpaka kuwapata kwa kutumia kamera za nje sehemu ya kuegesha magari.
Wakaonekana wakiwa nje wanaondoka na gari ya Love. Kisha baada ya muda wakarudi
pale hotelini na kukaa palepale walipokuwa wamekaa mwanzo.
Wakala
na kunywa mpaka mara ya nyingine tena yule muhudumu anarudi akiwa na ile juisi
ya Jelini na chakula cha Colins. Wakaonekana kumuita, akasimama. Love
akaonekana kumzonga na maneno, ndipo ikaonekana kama Kemi akapata upenyo wa kutumbukiza
kitu ambacho kwanza, kwa kuwa ilikuwa usiku na walipokuwa wamekaa palikuwa na
giza kidogo, Colins akajaribu huvuta lile tukio, ikaonekana kama Kemi
amenyanyua mkono juu ya glasi ya Jelini.
Hapakuonekana
kwa uhalisia kitu kilichoingia ndani ya hiyo juisi ambayo pia juisi hiyo
ya embe haikuonyesha kubadilika rangi. Lakini alipomaliza Kemi, ni kama akarudi
kumzungumzisha kidogo yule muhudumu, kisha wakamuona yule muhudumu akiondoka.
Akaonekana
hakupitia sehemu nyingine tena wala kusimama popote ila moja kwa moja mpaka
mezani kwa Jelini na Colins. Akaonekana aliweka kwanza ile juisi ya embe mbele
ya Jelini. Akaonekana Jelini kutosubiri. Palepale akapata funda mbili mfululizo
wakati huyo muhudumu akimuwekea Colins chakula chake. Kisha akaonekana Jelini
kusimama muda mfupi sana baada ya funda la pili, akielekea chooni kisha kuongeza
mwendo kwa kukimbilia.
Baadaye
Ezra kuingia pale hotelini, mpaka vyoo vya wanawake. Akaonekana ametoka
akikimbia na Jelini kisha kumuweka kwenye gari ya hospitali. Kisha baadaye
akaonekana Love na Kemi wakitoka kwa kukimbia kuingia kila mmoja kwenye gari
lake na kuondoka kabisa kwenye eneo la hoteli hiyo.
~~~~~~~~~~~~~~~
Yule mmiliki jasho
lilikuwa likimtoka kama hapakuwa na A/C kwenye chumba hicho. “Mpaka hapo tupo
pamoja?” Colins akamuuliza. “Huna jinsi ya kumkwepa mama yake huyu binti, na
vyombo vya sheria kama wewe hutakuwa mbele
ya hawa wawili nilio kuonyesha.”
“Tena unatakiwa uwe
mbele yao hata kwa hatua 5 zaidi.
Kwa sababu hawa wanawake wawili, kwanza wametoka kwenye familia zenye pesa
sana. Inamaana watatafuta mtu mzuri kuwawakilisha kwenye mashitaka
yeyote yale dhidi yao. Nakuhakikishia usipojipanga vizuri na kwa makini ili
kuwawahi, watakushinda, utafia jela.”
“Pili,
nimeshakuonyesha jinsi walivyo wajanja. Wanaakili sana kwenye uovu wao. Wakati
wewe hujui kilichokuwa kikiendelea, wao walishamtafuta mtaalamu kuingia kwenye mtandao wako, kufuta ushahidi. Sasa akili
kumkichwa.”
“Tafadhali nisaidie
kwa ushauri kwa sababu wewe unaonekana unawaelewa vizuri na umeshawashinda!” “Cha
kwanza na haraka, huu ushahidi ukulinde. Namaanisha usiulazie damu.
Yaani sasahivi wewe jionyeshe upo makini, hakuna mtu anacheza na usalama wa wateja
wako.” Akajiweka sawa kumsikiliza.
“Afisa usalama wako aivujishe hii video kwa haraka sana.
Kisha kimbia nayo polisi kushitaki.
Ili hata kama wakiwahi kukuziba polisi, jamii imeshaona walichokifanya. Watashindwa
kukuzima huku nyuma kwenye vyombo vya usalama. Jamii nzima itakuwa nyuma yako.”
“Kingine cha msingi
ambacho nakusihi usisahau, ukitoka
tu polisi, usiku huuhuu, hakikisha unakwenda hospitalini kumuona mama yake huyu
binti. Kikubwa, nguvu yako ni hiyo lafudhi yako. Mama yake ni mkabila
sana. Ukimuongelesha kikwenu. Halafu ukaonyesha upo upande wake kwa asilimia
100. Na umeshawashitaki, hawa watu. Utaupata moyo wa huyu mama, na anaweza hata
kukusikiliza. Lasivyo ni wakumuogopa kuliko hata kituo cha polisi.
Wanaomjua watakwambia.” Kimya amekodoa macho.
“Yaani hapo
uliposimama mpaka sasa hivi, umeshaanza kuchelewa. Changamka. Umechezewa
mchezo mchafu sana, tena na watu makini, halafu ni makatili
wanaojua kujipanga kwa makini sana. God
speed.” Colins akasimama na kuondoka bila ya kuaga.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment