Wakiwa kwenye ile
hali. Mama mchungaji karibu yake pamoja na mama zake wengine Jelini walishafika
hapo hospitalini na Jema akiwepo, James akawasogelea. “Najua tupo kwenye
kusubiri, hatujui kinachoendelea ndani, lakini mama Jema, tafadhali jikaze
uangalie hii video, ujue kilichokuwa kikiendelea mpaka kumfikisha Jelini hapo
alipo. Usibakiwe na yote. Angalau utoe sintofahamu moja.” James akavuta masikio
na akili za kila mmoja pale. Mchungaji na vijana wake walikuwa wameinama kila
mmoja akimsihi Mungu kivyake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hali ya Ezra ndio
alijawa hofu! Vifo vya ndugu zake zaidi alivyoshuhudia akiwa ameitwa kuzika
wazazi vilimjia. Hapo alikuwa na hali mbaya. Hata kukaa chini alikuwa hawezi. “Mungu wangu nisaidie!” Ndio neno lililosikika
akilisema kila wakati akitembea hapo bila kupumzika, mikono kichwani. Macho
mekundu kama aliyevuta bangi ya kupitiliza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Aliposikia hivyo, akasogea
hapo kwa haraka. “Ezra wewe nimeshakutumia wa kwanza maana Colins ameomba nikuonyeshe
wewe wa kwanza.” Wote wakashangaa. “Na ujumbe mwingine kutoka kwake,
nitakwambia baadaye maana najua sasahivi haupo kwenye wakati wakuelewa” “Aisee
hata sijui simu yangu ilipo!” “Uliacha kwenye gari yako, nimekuchukulia.”
Junior akatoa mfukoni na kuitafuta hiyo video kisha kwa heshima akamkabidhi
Ezra mwenyewe.
“Naomba tukae hapa
tungalie na baba.” Maana mchungaji alibaki ameinama kwenye kiti alichokuwa
amekaa kama ambaye bado anaomba.
Ezra akatoa wazo la kuthamini uwepo wake, vijana wakasogea alipokuwa amekaa
mchungaji. Kwa hiyo kukawa kama na makundi matatu yaliyotengenezwa. Kwa mama
Jema na dada zake pamoja na mama mchungaji. James na mkewe. Mchungaji, Noah,
Ezra na Junior. Wakaanza kuangalia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Colins alikuwa
akifikiria kwa haraka huku anahasira kali sana. Akaamua kumtumia ile video na
Kevin Kasa. Na ujumbe. ‘Natarajia kupokea simu yako
punde utakapomaliza kuangalia.’ Akamtumia na kubaki akimsubiria huku
akiangalia saa. Alijua wazi anamuogopa na kule kumkamata akiwa anataka kufuta
hiyo video, akajua hawezi kuwa amepata usingizi.
Akasubiri kwa muda wa
ile video, kimya. Kevin hapigi. Akaamua kumpigia yeye. Ikawa ikiita bila
kupokelewa. Akaamua kumtumia ujumbe mwigine. ‘Nina hali
mbaya sana. Kupotezewa muda ni jambo la mwisho kabisa nataka kukumbana
nalo usiku huu. Tafadhali pokea simu yangu Kevin.’ Baada ya sekunde
chake akaona anampigia.
Colins akapokea.
Kimya upande wa pili. “Naomba nitumie ile video ya
kwanza uliyofuta ya dada yako alipomtega Jelini, na kumpasua kichwa.” “Nini
kinakufanya ufikirie ninayo!?” “Kevin! Rudia ujumbe wangu niliotoka kukutumia.
Nimekwambia, kupotezewa muda ni kitu cha mwisho kabisa usiku huu, na sitaruhusu.
Sijui kama unanielewa? Kwa sababu mimi na wewe wote tunajua wazi, wewe
ukishindwa kunipa hiyo video, ndani ya masaa 24, mimi mwenyewe nitakuwa
nimeipata. Lakini haitakuwa nzuri kwako.” Kevin kimya.
“Nitahakikisha
nina kuadhibu kama nitakavyo muadhibu dada yako.” “Kwa nini unifanyie
hivyo wakati ni Kemi mwenyewe!?” “Nitakuadhibu kwa kusaidia kwenye uhalifu
wake. Zaidi kwa kumuangamiza mwanamke pekee ninayempenda hapa duniani na ambaye
alinipenda mpaka dada yako akafanikiwa kututenganisha. Na leo
amegongelea msumari wa mwisho. Sitamsamehe.”
“Nyinyi si
mnahela na najua hata akishitakiwa, baba yenu atamtetea, lakini.” Akaweka
kituo cha mkwara. “Kwa hakika atatamani angeshitakiwa
kisheria kuliko kukwepa hukumu yake. Na wewe, nitahakikisha kila mwenye
kampuni, vyombo vya usalama, vyote vinajua wewe ni mtu hatari sana mitandaoni.
Nitakuweka kwenye orodha ya kimataifa. Nitaku blacklist, hakuna security
system utapita hapa duniani, zaidi
kwenye viwanja vya ndege, ukaruhusiwa. Watakushikilia kama gaidi au mtu hatari, mpaka
baba yako aje akuokoe! Utakua umelipa. Na najua, unajua sishindwi, ila pengine unaweza dhania
nakutisha tu ili nipate hiyo video.” Kimya. Akajua ametishika.
“Sasa,
nakupa lisaa, uwe umeipata hiyo video na imeingia kwangu. Lasivyo, hutakaa
ukanisahau kama ambavyo sitakaa kumsahau Kemi Kasa. Nitakulipa mpaka ujue nimekulipa kwa dada yako kunipokonya penzi la Jelini, akiwa
amenifanya tahira na leo kukusudia kumuua kwa mara ya pili. Hakika utalipa kwa
uchungu, labda ujiokoe kwa hili.”
“Vinginevyo
jua kuanzia sasa, cha kwanza huna kazi. Maana nina ushahidi wote wa usiku wa
leo ulivyoingia kwenye ule mtandao wa ile hoteli. Mpaka Ip address ya ulikokuwepo ukifanya huo uhalifu, ninayo. Sasa jua mabosi wako wote,
ifikapo kesho asubuhi hata kabla ya siku ya kazi kuanza, watakuwa na hizo
taarifa kwenye simu zao za mkononi wakiwepo wafanyakazi wote wa ile kampuni.” Kevin alimjua Colins
na uwezo wake.
“Cha kwanza
naomba nisamehe Colins. Mimi sikujua mchezo wowote Kemi aliokuchezea. Ningejua
kama ni wewe, kwa hakika unajua nisingefanya nilichofanya. Ukiweka
hasira pembeni, utagundua mimi simjinga wakutaka kukuzidi mahesabu. Na hata ile
video ya kwanza, Mungu wangu ni shahidi. Alinipigia kama hivi kwa haraka, akiniomba
msaada kwa haraka.” “Unanipotezea muda Kevin. Acha kunifanya mimi mjinga. Na
nikikata hii simu…” “Colins! Colins!” Akaita kwa kupaniki.
“Basi na
mimi nikuombe kitu.” “Haupo kwenye hiyo nafasi Kevin.” “Kumbuka mahusiano yetu
Colins! Mimi sijawahi kukukorofisha hata mara moja, hata jamaa pale ofisini
walikuwa wakinitania kuwa nakuogopa, wewe ndio unaniweza. Uongo mkuu?” Colins kimya.
“Sijawahi
hata mara moja kukanyaga ulipokanyaga nikakuumiza hata kwa bahati mbaya. Na
wewe ni shahidi Colins. Nishagombana na kila mtu pale ofisini lakini haijawahi
tokea mimi na wewe tukapishana hata mara moja. Ndio naomba uelewe katika hili, sihusiki Colins. Kwanza nisingethubutu.” Kevin huyu
alijishusha na mnyenyekevu aliyejawa hofu utafikiri sio Kasa! Ungejua
amekamatika.
“Unataka
nini?”
Colins akauliza kwa jeuri. “Nakutumia hiyo video
sasahivi. Lakini tafadhali naomba usinitaje popote, hata iweje.” “Mimi si mtoto
mdogo. Na nakutuma kwa baba yenu. Hakikisha unamfikishia huu ujumbe. Mwambie
Kasa, safari hii hakuna umbali atamficha
Kemi, malipo yake yasimfikie.” Kisha akakata simu.
Hazikupita hata
dakika 5, tayari lile tukio zima la Kemi kumtega mguu Jelini na kuumia vibaya
sana, likawa limeingia kwenye simu ya Colins na ujumbe. ‘Tafadhali kumbuka ahadi yako Colins.’ Colins akaanza kuangalia,
mpaka akatupa simu hapo garini kwa mshituko. Akabaki akihema kwa hofu,
akitafakari ni kiumbe gani anaweza kumfanyia mwanadamu jambo baya kama hilo! Hasira dhidi ya Kemi
ikazidi kuwaka ndani yake. Akamalizia kuangalia na kumtumia na James pia.
Mfa Maji.
Huku kwa Kevin akajua
maji yameshatibuka, akaona ajisalimishe kwa kujitetea. Akampigia simu baba
yake. Simu ile ya dharula ambayo mzee hazimi sauti hata usiku. Ni wachache sana
walikuwa nayo, na wenyewe walijua si ya kuipiga hovyo. Ni iwe dharula
kwelikweli.
Mzee Kasa akapokea
bila ya kuchelewa. “Kuna nini!?” “Safari hii Kemi
ameharibu baba! Na ameharibu pabaya sana. Mbaya zaidi alichokifanya safari hii,
amekifanya kwa mtu yuleyule ila akiwa na mtu hatari sana. Ametibua siri zote.
Hapa tunapo...” “Acha kunizungusha kwa maneno mengi ya mafumbo, muda huu unaojua
ninatakiwa kuwa usingizini.” “Amemdhuru tena Jelini ila…” Kusikia Jelini
mzee akaruka kitandani.
Kevin akahisi simu
imedondoka kwa ule mlio aliosikia. Akaona amtumie ile video aliyotumiwa na
Colins na kisha akamtumia na ya kwanza ambayo baba yake anaijua, ila
akamdanganya. ‘Mbaya zaidi na hii pia Colins
amefukunyua mpaka ameipata. Amenituma nikwambie, safari hii huna umbali
utamficha Kemi, malipo yake yasimfikie.’ Akautuma huo ujumbe na
kujituliza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hapo Colins alikuwa
akifikiria kwa haraka akijiweka kwenye viatu vya Kemi, Kasa, ndugu wa Jelini,
kila mmoja wapo na kutaka kuwa hatua nyingi mbele ya kila mtu. Kwa ndugu wa
Jelini alihakikisha anawatoa macho na akili zao kwake kabisa wabakiwe
wakimfikiria Kemi na Love tu.
Halafu kwa Kemi,
alifikiria kwa muda huo atakuwa anapanga kutoroka nchi. Akamuwahi kusambaza
zile video zote kwenye vyombo vya usalama. Halafu kwenye balozi zile kubwa,
zaidi Uingereza alipokuwepo mama yake, akatuma kwa siri angalizo la Kemi Kasa
na kuunganisha na zile video akimsema ni mtu hatari, aangaliwe
anafikiria kukimbia nchini kwake baada ya kufanya jaribio la mauaji.
Akasambaza picha zake zote kwenye mitandao ya kiusalama kwa wazi kabisa. Yaani
kile alichomwambia Kevin angemfanyia, basi akafanyia dada yake.
Akawa amemuwahi yeye
hata na baba yake kama angefikiria kumtorosha nchini. Kwamba tayari Kemi akawa
amemfunga kifungo cha nje cha nchini hata kabla kesi yake haijatajwa.
Alikuwa na hasira na
Love naye, yeye aliomba Mungu asije akafa kabla hajamfikia. Alishampigia
mahesabu. Alihakikisha anamuweka kwenye nafasi zote. Alishaanza kuhisi kwa lile
tukio moja walilosaidiana na Kemi pale, wanaweza kabisa kujitetea, zaidi
Love akashinda. Lakini hata hapo alijiapia kumtenda vibaya sana. “Kicheko
alichocheka leo, hakika ndio cha mwisho katika maisha yake hapa duniani.” Akajiapia
Colins kadiri alivyomfikiria Love.
Kwamba hata akishinda
kesi, kwa kosa la jaribio lakutaka kuua, alinuia kumuadhabu vilivyo huko
uraiani. Akabaki akiweka mikakati yake taratibu na kwa akili sana bila
ya kuacha hata punje ya kuhisiwa kama ni yeye.
Kujihami Kwa Kila Mmoja.
Mmiliki wa Hoteli.
Wakiwa wametaharuki
na ile video ya pili, akawafuata yule mmiliki wa hoteli. Kama alivyoambiwa na
Colins, salamu ya kwanza akapiga kwa kilugha. Hapo akapata attension
ya mama Jema na dada zake. Akaendeleza kikwao akiwapa pole kwa kuwashika
watu wote mikono kwa heshima sana. Wakabaki wakijiuliza ni nani!
Upande wa kina Ezra
wakadhania pengine ni mjomba! Kwanza alizungumza lugha ya kwao na kusalimia kwa
ukaribu haswa kama aliyeguswa na tukio! Lakini kina mama Jema wao wakabaki
hawajui ni nani! Wakabaki wamekodoa macho.
“Nimekuja kumwangalia
Jelini kama mteja wangu aliyedhuriwa kwenye hoteli yangu.” Hapo wakakaa
sawa. Akaendelea kwa haraka kabla hawajamuingilia. “Tumekamata tukio zima, hapa
nimetoka polisi kufungua kesi, zaidi kutaka wasichana wawili tulio waona kwenye
video wakamatwe. Kuhakikisha kwanza hawatamdhuru tena mtu mwingine na waadhibiwe
kwa hiki walichomfanyia Jelini. Sitatulia mpaka hiki walichofanyia Jelini,
nikiwekee kikomo na wahalifu watiwe nguvuni.”
“Yule muhudumu aliyekuwa
akimuhudumia Jelini ameshahojiwa kwa undani sana, na taarifa zake zimetunzwa
kwa sir...” “Yeye amesemaje?” James akauliza. “Naomba kwa heshima ya
Jelini na kwa haki yake, nisitoe ushahidi wake hapa hadharani. Siku hizi
teknolojia imekwenda mbali sana. Sitaki mtu asikie haya na kurikodi halafu
kusambaza na kuwafanya adui kujipanga dhidi ya uhalifu wao.”
“Hata yeye atafichwa kabisa
hata jina lake litahifadhiwa mpaka uchunguzi mzima utakapo kamilika. Hakuna atakayezungumza
naye wala kumfikia kwa wema au hata ubaya kutaka kumuhonga au hata kumdhuru ili
kuficha ushahidi. Atakaa mafichoni mpaka Jelini apate haki yake kwa kukamilisha
uchunguzi mzima. ”
“Hii nawaambia tu
nyinyi kwa heshima ya hawa dada zangu tu.” Akimaanisha mama Jema na dada zake. Undugu
tayari! “Lakini hata polisi nimeomba wafiche kabisa taarifa za yule muhudumu
mtu hatajua alipo ila mimi tu, mpaka kesi itakapokamilika. Ila kila atakapohitajika
katikati ya uchunguzi, watawasiliana na mimi, na mimi nitahakikisha anafika
kituo cha usalama kutoa ushirikiano, na kurudi mafichoni.” Akaongea mengi
akichanganya na kilugha akiweka undugu mpaka akafanikiwa kupata mioyo yao. Kwa
hakika alikuwa upande wao, na alionekana kutetea Jelini vilivyo.
“Hapa tunapozungumza
nimeshatafuta mwanasheria wakumtetea Jelini. Ni pesa nyingi, lakini pia niwe tu
muwazi, nataka kuhakikisha Jelini anapata haki yake na kuweka kikomo kwa yeyote
anayefikiria kufanya jambo kama hili pale kwenye eneo langu la biashara.
Sitatulia mpaka hili likamilike. Hata kama wao watakuwa na pesa kiasi gani, na
mimi nitapambana kama hivi binti yangu Jelini anavyopambania uhai wake,
kufa na kupona.” Mama Jema akampa kabisa mkono akimshukuru. Ndipo sasa akataka
kujua taarifa za mgonjwa huku akiahidi kulipia garama zote.
Penzi Lililogoma Kutoka Moyoni.
Isivyo ya kawaida,
hakuna aliyetegemea, wakashangaa Kasa na askari wawili nao wamefika hapo. Waliomfahamu
wakabaki wamepigwa na butwaa na yeye akawahi kabla hawajatoka kwenye ile hali. Akamsogelea
mama Jema.
“Najua mimi ni mtu wa
mwisho kabisa ungetamani kuniona usiku huu. Lakini mama Jema, nipo hapa
kwa ajili ya Jelini. Nimeshajua ameanza kutapika damu, na hapa hapana vifaa
vizuri vya kumchunguza. Wataandika vipimo, ambavyo itabidi isubiriwe kesho, tena
akafanyiwe kwenye hospitali kubwa, sio hapa, kitu ambacho kitachukua muda
mrefu ambao Jelini hana kwa sasa.”
“Ningeweza kujificha
na kukimbia kama kina Kemi, lakini siwezi kufikiria wala kupata usingizi
nikijua Jelini yu matatizoni, tena kwenye tatizo la hatari kwa kiasi hiki. Sipo
hapa kwa ajili ya Kemi, nipo hapa mimi kama Alexender Kasa, nikitaka kumsaidia
Jelini. Sasa basi.” Akaendelea wote wakimtizama.
Kwanza ni KASA. Vile tu
alivyosimama pale, alivyopendeza usiku huo, msafi, mavazi si ya kiofisi, track
suit nyeupe haswa yenye zipu na nembo nyeusi ya under armour. Akavaa
sneakers nzuri nayo ni nyeupe na nyeusi, Nike safi. Harufu nzuri na
safi ikaenea hapo kutangaza aghueni ya maisha. Yaani mpaka hapo tu, uwepo wake
ulishaenea. Anazungumza kwa kujiamini. Halafu ametokea katikati yao, kwenye
wakati mbaya kama huo! Ni anayejielewa na kujiamini tu, ndiye anayeweza
kufanya alichofanya.
“Taarifa za
kinachoendelea huko alipo Jelini sasahivi, wanakomsaidia, zimeshapokelewa
na madaktari wanao msubiria kwenye hospitali yenye vifaa vizuri na wanao weza
kumsaidia. Najua wamemtapisha sumu, lakini hata wao wanataka kujua juu ya damu
inayomtoka. Hapa ninapozungumza na wewe, gari ya hospitali ipo hapo nje, na
kama nilivyo kwambia, nina madaktari wapo tayari wanamsubiria yeye tu. Akifika
tu huko, apewe huduma nzuri, na ya hali ya juu, kwa haraka.”
“Sidharau kile anachofanyiwa
hapa, ila mkumbuke mlimleta hapa kwa dharula, inamaana usiku huu anakutana na
daktari wa zamu ambaye wagonjwa wengi wanamtegemea yeye daktari mmoja. Lakini kule
anasubiriwa na zaidi ya madaktari wawili, kumshugulikia tu yeye. Nakuomba mama
Jema, niruhusu kumtoa hapa Jelini, akatibiwe ndipo adhabu zangu zote
zinifuate baada ya hapa.”
“Na nakuhakikishia,
akifikishwa tu kule, nikahakikisha wale madaktari wamemshika, nitaondoka
kabisa wala hutapata shida ya kuiona sura yangu. Nia nikutaka Jelini si atoke
tu kwenye hii hali, bali kutibu madhara ya ndani zaidi. Sio wamruhusu kesho au
usiku huu sababu wamefanikiwa kumtoa sumu, kisha kuachwa na madhara makubwa
zaidi ndani yake! Hapana. Nataka wamuangalie na wajue jinsi ya kumsaidia. Wakisema
amepona, iwe kweli amepona.”
“Na msihofie juu ya
garama. Kila kitu kimeshalipiwa. Ninachokuomba ni ruhusa ya Jelini akatibie
vizuri na kwa haraka. Ni hilo tu. Tafadhali tuokoe muda ambao umeshapotezwa.”
Mama Jema akabaki akimtizama Kasa. Wengine wote kimya wamepigwa na butwaa. Wamemkodolea
macho Kasa kama wanaojiuliza gati hizo anapata wapi!
~~~~~~~~~~~~~~~
USIKU WA HEKAHEKA.
WAKATI JELINI AKIPAMBANIA UHAI WAKE, MENGI YALIKUWA YAKIENDELEA.
KILA MMOJA
KWA WAKATI WAKE NA SABABU ZAKE.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment