Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 3 - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 3

Kisha mama Jema akamgeukia Ezra kama kutaka kujua na yeye anashauri vipi! “Tunahitaji kila msaada tunaoweza kupata kwa Jelini. Nafikiri sio wazo baya.” Akaongea Jema kwa haraka hata kabla Ezra na mama yake kujibu. Bila kusubiri jibu jingine, akawageukia wale askari na kuomba wawaite wale watu waliokuja na gari ya wagonjwa ili wakamchukue Jelini.

Baada ya muda wakawaona wanaingia na kitanda cha wagonjwa na kuelekea alipopelekwa Jelini. Kasa akafuata kwa haraka. Ndani ya dakika 10, hata hazikuisha, wakaona tena wanatoka kwa haraka na Jelini akiwa amelala kwenye kitanda cha wagonjwa. Wote wakasimama kwa haraka wakikimbilia.

“Samahanini, naomba tena hapa tusipoteze muda zaidi. Mnaweza kufuata lakini nimeomba hawa polisi wanisaidie barabarani, ili kusaidia hii gari ifike huko kwa haraka. Hapatakuwa na kusimama tena mpaka wafike.” Kasa akaongea kwa haraka na kuomba wapishe pale kitandani, Jelini alikuwa hata hatikisiki japo waliona anahema, amefunga macho na dripu yake mkononi.

Wakatoka hapo wote wakifuata kitanda kwa nyuma. Akapandishwa kwenye gari, Ezra akapenya kama mshale na yeye akaingia alipolazwa Jelini, milango ilipofungwa tu, gari hiyo ya wagonjwa ikatoa mlio na mataa makali. Wale polisi wa pikipiki wakawa wameshapanda kwenye pikipiki zao, taa tayari, msafara wakutoka hapo ukaanza kwa kasi. Kasa naye alikuwa nyuma ya gari ya wagonjwa na yeye akifuata kwa kasi asiwe mbali na ule msafara.

Ndani ya dakika 5, wote, kasoro Ezra aliyeondoka na Jelini, wakajikuta wamesimama hapo nje, kimya, wamekodoa macho. Ikawa hali ya kuogopesha, lakini kama na tumaini jipya. Kwamba pengine huko wanapokwenda, watafanya miujiza ya kumponya kabisa huyo Jelini. Ndipo James akashauri na wao wafute bila kuchelewa zaidi.

Upande wa wakina mchungaji wakabaki kujiuliza huyo Kasa mwenye makuu hivyo ni nani, ila ikawa kwa mara ya kwanza, Junior na Ezra wakafanikiwa kuweka sura sahihi kwenye jina walilokwisha sikia na kumuona kwenye video waliyotumiwa na Colins. Vile alivyokimbilia kumuokoa Jelini pale sakafuni, na kumkumbatia akizuia damu iliyokuwa ikitoka kama bomba, ofisini kwake.

Kasa, Nguvu Ya Pesa.

Mpaka wao wanafika kwenye hiyo hospitali ingine, Jelini alishakuwa amepokelewa na kuanzishiwa huduma kana kwamba hakuwa ameonekana na daktari mwingine. Ezra ndiye aliyewapa taarifa. 

“Yaani wameanza upya kabisa na ameshaingizwa kwenye kipimo cha kwanza. Tumefika hapa walikuwa wakimsubiria na tayari walikuwa wana taarifa zake zote. Maana pia walikuwa wakiwasiliana hata na wale wauguzi tukiwa njiani kwenye ile gari ya wagonjwa tuliyopanda.”

“Hata ameweza kufungua macho?” “Kuna jinsi wamemfanyia hapa, wakajaribu kumuongelesha na kuangalia macho. Akarudi kulala. Tafadhalini tusiache kuomba japo yupo hapa kulikosikika kuna huduma nzuri.” Akasisitiza Ezra. Wakaanza kuomba tena. Na yule mmiliki wa ile hoteli naye akawasili na kujikuta amekaa hapo kama mmoja wa familia.

Kwa Kina Love.

Alipopata taarifa kuwa yupo mitandaoni kwa shutuma nzito, akajua ameangukia pua. Akakimbilia kwa wazazi wake. Akawaonyesha ile video na kuanza kueleza upande wake akijitetea. “Sisi tulikuwa tumekaa zetu tunakunywa na kina Festo. Kemi akanipigia na kuniambia ameboeka, anaomba kampani yangu. Nikamwambia tulipo, akatufuata tukaendeleza kikao.

Baada ya muda tukamuona Colins anapita na kwenda kukaa, sehemu ya peke yake. Hatujakaa sawa, Jelini naye akawa anapita, anaelekea kule alipokuwa amekaa Colins. Ndio Kemi akasema tuwakomoe. Mimi nikamkatalia kwa kumwambia sitaki tena michezo na Colins. Kwanza ukimya wake baada ya kupona, unaniogopesha. Akasema safari hii iwe Jelini, kama kumtia tu aibu pale mbele ya watu kisha ashindwe kabisa kuja kurudi kwenye ile hoteli.”

“Akapita muhudumu pale akiwa na vinywaji vyao, ndio akamuita kumuuliza wameagiza nini, maana tulimuona mwanzoni alipoenda kumuhudumia Colins kabla ya Jelini kufika. Akasema Jelini juisi ya embe, halafu Colins alitaka supu kabla ya chakula. Alipoondoka ndio akasema atatumia juisi hiyohiyo kumtia adabu Jelini, kumfanya aharishe hovyo. Mimi nikamuonya nikimwambia aachane nao. Akasema nimsindikize, yeye hatafanya kitu cha hatari.”

“Nikampeleka mpaka dukani, akaniambia nimsubirie ndani ya gari, akaenda kununua hiyo dawa aliyoniambia ni ya kuharisha tu. Akarudi nayo ndipo tukarudi tena pale hotelini. Tukaendelea kula ila akasema yule muhudumu akipita tena na vinywaji vyao, basi nimuongeleshe wakati yeye anaweka kwenye kinywaji cha Jelini. Ila sikujua ni nini anataka kuweka na wala mpaka sasahivi sijui ni nini aliweka.”

“Hivi sio nilikuonya urafiki na Kemi wewe!? Nikakukumbusha jinsi alivyokuacha wakati ule ulipompigia simu juu ya huyuhuyu Colins! Alikujibu hovyo na kukufungia simu zako zote. Akakuacha unahangaika na Colins hujui chakufanya. Nilikuonya uachane nae kwakuwa mwenzio anaonekana ana vita vikali sana na Jelini, ni zaidi ya anachokwambia. Maadamu alishakufanikishia mwanzoni, kwa nini umemrudisha tena kwenye maisha yako?” “Kumfanikishia!? Kivipi tena?” Mzee Simba akahamaki.

Mkewe akajua kashamwaga mchele kwenye kuku wengi. Akajirudi kwa haraka. “Hebu malizia tusikie mpaka mwisho. Huyu Kemi ni mshenzi sana.” Tayari mama Simba kama kawaida yake, akamtetea mwanae. Hakuhitaji kuaminishwa kwa chochote, ameshasimama na binti yake.

“Ndio tukafanya kama mlivyoona. Lakini nikashangaa Jelini anatolewa akiwa hana fahamu na gari ya hospitali, akasema tuondoke pale kwa haraka, yeye atashugulikia maswala yote. Hata kama kuna security camera imetuchukua, itafutwa kila kitu, wala hakuna atakayekuja jua kama tulikuwepo pale.”

“Lakini ndio nashangaa video zimevuja kwa haraka kama vile mtu alikuwa akitusubiria upande wa pili!” “Sasa na hapa na sisi ni kufikiria kwa haraka asije kukuingiza matatizoni.” Akasikika mama Simba, mama wa mipango. Hata katikati ya jambo zito vipi, atafikiria tu na kutoa mbinu zake zakutoka kwenye hilo jambo, hata kama si halali. Halafu ndio mshauri wa Love.

Simba akashangaa sana. “Asije muingiza matatizoni kwa mara ya pili?! Mpaka hapa huyu yupo matatizoni na ushahidi upo akishiriki naye. Umempigia?” “Naogopa baba. Naogopa hata kujulikana nipo naye.” “Sasa unakumbuka shuka kumeshakuchwa! Kwamba unaogopa kujulikana upo naye wakati video zote zinaonyesha mkishirikiana kwenye uhalifu wenu!?”

“Sasa hapo Simba na wewe unakua kama mtu wa nje kumshutumu mtoto, badala…” “Nawaambia ukweli wala sitamficha. Upo matatizoni Love. Na chochote kikitokea kwa yule binti!” “Wala sio binti yule, ni mwanamke. Tena mama kabisa. Wala hana udogo wowote ule.” Mama Simba akaongea kwa jazba.

“Vyovyote mtakavyomuita, maombi ya kwanza ni asife, apone. Lasivyo, huna jinsi ya kutoka kwenye hili.” “Sasa kabla hatujafanya chochote kwa paniki, tutafute ushauri wa kisheria. Tusije tukajitia kitanzi sisi wenyewe, kumbe kuna uwezekano wa kutoka. Maana hapa Kemi ndiye mwenye kosa.” Tayari mama akamtoa mwanae kwenye lawama.

Akampigia simu mwanasheria anayemfahamu, akamuomba msaada. Kwamba wakutane usiku huohuo. Na kwa kuwa na yeye alikuwa kama na deni kwa dokta Simba, yaani huyo mama, alishaokoa maisha ya mkewe na mtoto, akakubali wakutane. Akawafuata nyumbani kwa Simba, kuweka usiri zaidi.

Mikakati Ya Kuondoa Lawama.

Nani Wa Kulaumiwa?!

Wakawa mzee Simba, mkewe, Love pamoja na huyo mwanasheria nyumbani kwa Simba. Love akaeleza mwanzo mpaka mwisho akiwa ameshamtumia na yeye hiyo video. Akaiangalia tena na tena. Kisha akaanza.

“Cha kwanza ni lazima tumpate Kemi. Kwa kuangalia tu hii video, naona tuna tumaini.” Wote wakashangaa. “Msiwe na wasiwasi, tumpate kwanza Kemi ili tuwe ukurasa mmoja.” Kazi ya kumsaka Kemi kwa simu ikaanza. Akawa hapokei kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wasijue Kemi ameshapokea ujumbe kutoka kwa kaka yake. Alimpigia na yeye, baada ya kuzungumza na baba yao. Akapokea kwa haraka, ila hakuzungumza ili isijekuwa anamtega.

“Kama ulidhania upo matatizoni, jua upo matatizoni SANA. Na lile wazo la kukimbia kwa kupitia Nairobi, sahau. Hutavuka mpaka. Colins ameshakufunga kifungo cha hapa nchini. Ila kwa sababu wewe ni mbishi, sasa tokezea mpakani au uwanja wa ndege wowote ule, kama hujalala rumande leo. Na Colins hatakutania. Umepiga ikulu, mwanamke wake. Ameapa safari hii kukufikia popote. Na hata amemwapia na baba pia. Hakuna mahali atakuficha, asikupate.” Kemi akazidi kuogopa.

“Sasa nakushauri tu. Anza kujipanga sawasawa. Ila jua unapambana na Colins anayesema umeshamjeruhi vyakutosha, anataka kuweka kikomo. Taarifa zako zote, nina uhakika. Maana ndicho alichoahidi kufanya, na namjua jinsi anavyofikiria yule, atakuwa amesha kublack list.”

“Ameshakusambaza kwenye vyombo vya usalama, usafiri wa anga, na kila mpaka. Tena kwa kimataifa. Sasa mpaka uje ushinde kesi. Uje kusafisha jina lako kwenye vyombo vya usalama, si leo na si kimataifa. Nakuhakikishia Kemi, hapa nchini hutakaa ukatoka.” Kevin akakata simu.

Hakutaka hata ushahidi wa kutuma ujumbe, Kemi asije tumia baadaye. Ndio maana akampigia, akafikisha ujumbe, na kukata. Tena alimpigia akificha namba yake isionekane kwenye simu ya dada yake. Kwamba hata wakitafuta kujua usiku huo walio wasiliana na Kemi, basi na yeye asiwe miongoni mwao.

Akaona haitoshi. Akafika umbali wa kuingia mtandaoni, akafuta mawasiliano yote kati yake na dada yake usiku huo mzima. Kwamba pasionekane hata kama waliwasiliana. Kemi alishafika mbali sana wakati akipokea hiyo simu ya kaka yake yenye ujumbe wa kutisha. Akapiga break ya haraka na kugeuza.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wao wanahangaika kumpata kwa simu, alishaamua asizungumze na yeyeote yule mpaka ajue nini chakufanya. Mwishoe yule wakili akamwambia amtumie ujumbe. Love akamwandikia. ‘Najua umeingiwa hofu. Lakini tayari nimeshapata mwanasheria ambaye atakuwa wakili wetu, ameangalia ile video, anaona hakuna chakutufunga endapo kwanza sisi tutakuwa pamoja, yaani ukurasa mmoja. Halafu mbele bila ya kujificha. Kukimbia au kujificha, ni kujifunga wenyewe.’ Akatuma huo ujumbe.

Baada ya muda mfupi sana akampigia. Love akamkabidhi simu yule mwanasheria kabla hajapokea. Yeye ndio akapokea. “Huyu Jelini alikuwa na yake wala si sisi. Asitake kutu…” “Nisikilize Kemi. Huyu anayezungumza na wewe hapa si Love, naitwa Christopher, unaweza niita Chris. Huko tumeshapita. Sasahivi tunataka kujipanga. Na kwa kutumia video hiyohiyo mnaweza kushinda. LAKINI lazima tuwe ukurasa mmoja, kisha kuwa mbele ya hizi shutuma. Unanielewa?” “Nakusikiliza.” Kemi akasikika kutulia sasa, maana alianza kwa jazba.

“Lazima tukutane, sasahivi. Usiku huuhuu. Tujipange. Uko wapi?” “Mbali kidogo.” Akajua alikuwa anakimbia. “Sasa kukimbia ni kujifunga. Unanielewa Kemi?” “Hapa nageuza ili nirudi. Naomba mnipe kama masaa mawili na nusu, nitakuwa nimefika hapo.” “Sawa. Sisi tunakusubiri. Ila endapo utabadili mawazo, utujulishe ili tusikeshe tukikusubiria hapa.” “Hata hivyo siwezi kutoka tena nchini. Nimeambiwa wameshapeleka taarifa zangu kwenye vyombo vya sheria. Kwamba siwezi vuka mpaka wowote ule kwa njia yeyote ile. Ndio maana nilikuwa nikirudi.” “Ni wazo zuri.” Akamtia moyo ili tu arudi, na kukata.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Mnaonekana mmeharibu pabaya! Wameshawatangulia hatua ya mbeleni. Wameshawafungia mipaka. Kwamba hapo ulipo, hutaweza kutoka hapa nchini. Mwenzio anaonekana alikuwa akijaribu kukimbia, ameshindwa, anarudi.” “Mimi nilijua tu! Na nilimuonya Kemi juu ya kumchokoza tena Colins.” “Itabidi unieleze vizuri hizo ‘tena’ unazoweka juu ya Colins. Ulimfanya nini kingine?! Na inabidi uwe muwazi Love ili tujue jinsi ya kukusaidia.” Mzee Simba akauliza na kuzidi kumtia hofu Love.

Mama yake akaingilia. “Huko ndio kujichanganya Simba. Tufanye jambo moja baada ya jingine. Kuanza kufukua ya nyuma ni kujichelewesha na kupotea malengo. Hawa watu wamekua pamoja. Unafikiri kuvutana kwao imekua mara moja?” “Hili la leo nalo unaita ni kuvutana!?” Mumewe akashangaa sana. “Ndio tumalize moja baada ya jingine, si yote kwa wakati mmoja. Hatutatatua tatizo ila kujifunga wenyewe.” Mama akaweka ngumu.

“Tena huyo msichana ni hatari sana jamani! Nashauri tutoke hapa kwangu. Asije pafahamu, akaanza michezo yake kwa familia yangu. Mimi naijua nguvu yake. Hatari sana. Naomba tukamalizie haya mambo ofisini kwako, Chris. Tafadhali sana.” Wakati akimuunga mkono Love awe karibu na Kemi ili amsadie kwa Colins, Kemi hakuwa hatari. Alipoona alichomfanya Colins na usiku huo Jelini, mama Simba mwenyewe akamnyanyulia mikono Kemi. Wakaondoka hapo kwake kwa haraka huku wakimtaarifu walipo. Mzee Simba kimya akijua anajichanganya tu, kwani walishamuelekeza afike hapo kwao. Ila akaona afuate mkumbo aone watakapofikia. Maana alijua kwa hakika mwanae yu matatizoni.

Hasidi Asiyeacha Asili.

Nanga ilishakuwa ikipaa mida hiyo ya saa 7:20 usiku wakati Kemi akiwasili hapo ofisini kwa Chris. Macho, masikio na tumaini pekee ni kwa huyo nahodha Chris, kufikisha jahazi salama. “Cha kwanza kabisa, nataka kukusikia na wewe Kemi. Ila usinidanganye, maana mkisema tu uongo, nitashindwa kuwasaidia.” “Kwani wewe Love amekwambia nini?” “Nimeshazungumza na Love, nataka kukusikia na wewe.” “Nitajuaje kama hamnitegi? Maana mpo hapa nyinyi wanne, kwenye ofisi yako, tena mkiwa mmenibadilishia sehemu ya kukutania. Kama kuna video na vinasa sauti je! Halafu mkanigeuke baadaye! Mimi si mjinga.” Kemi akaongea kwa jeuri akijiamini bila hofu mbele yao.

Ukatokea uvutani wa namna yake mpaka ikabidi wote watoe simu zao, Kemi akague, kama hakuna kurikodiwa kisha nakutaka zibakie hapohapo juu ya meza anapoziona zimezimwa kabisa. Kisha akaanza kukagua hicho chumba kizima kuhakikisha hakujafichwa kamera yoyote ile. Akafanya kwa makini mpaka aliporidhika ndipo akaweza kuzungumza sasa.

Kujihami na uongo ukawa mwingi huku wakirekebishana na Love kwa ugomvi kabisa, wakitoleana siri. “Huyu Love anataka kujitoa sasahivi hapa, wakati na yeye alikuwa akishabikia akitaka kumkomoa Jelini. Tena akanihamasisha mpaka kwenda kununua dawa muda uleule!” “Acha uongo Kemi.” “Muongo na mnafiki ni wewe Love. Mbona unakataa kuhusika na kwenye ile video hukuonekana kufungwa kamba na kutoka pale na mimi nikikuburuza kwenda kununua dawa? Ulionekana umejawa cheko wala hapakuwa na dalili ya kulazimishwa kuongozana na mimi wala kuwekewa risasi kichwani kuzungumza na yule muhudumu?” Kemi akamjia juu kabisa.

 “Usitufanye sisi wote wajinga. Kama unadanganya, wadanganye wazazi wako lakini sio mimi ninayekujua hila zako. Sasa hivi unajidai kukataa, wakati muda mfupi uliopita ulikuwa ukinitia morari ukisema zege isilale, usiku huu huu lazima kumkomoa Jelini mbele ya yule mwanaume wenu, huyo Colins. Amuone anavyojiharishia hovyo, amuone takataka. Bisha.” “Huoni hata aibu Kemi wewe! Yaani unanibadilishia maneno hapahapa!”

“Ushahidi si upo? Kama kweli si wivu wako kwa yule mwanaume asiyekutaka, ila kujilazimishia. Si..” “Colins ananitaka sana, ila Jelini ndio anamchanganya. Na bora yangu mimi si mwanaume wa ndoa, kuliko wewe mumeo wa ndoa hataki hata kukuona!”

Kama Colins anakutaka, kwa nini kutumia nguvu kumfungia ndani ili asitoke kumfuata Jelini?” “Wewe ndio muovu kuliko hata shetani mwenyewe. Yote hayo ulipanga wewe. Sasa hivi ndio unataka kunitupia mimi lawama!” “Nakuuliza tokea mwanzo. Kama kweli wewe ni mtakatifu, kwa nini tulikwenda wote kununua dawa kwa ajili ya Jelini? Eti Love? Wewe si unajidai mtakatifu sana hapa mbele ya wazazi wako?” Akamuuliza na kuendelea bila kumpa nafasi ya kujibu.

Uliyataka wewe mwenyewe! Na huo ndio mchezo wako Love. Kutaka makubwa, halafu kukimbia matokea. Na mwanzo ilikuwa hivihivi. Ulimgeuza Colins tahira. Ukaona raha wakati ukila vyake, baadaye ulipoona vinakudodea, ukaanza kutafuta mchawi, wakati..” “Muongo Kemi. Mchawi ni wewe na yule mwanaume wako ndio mlomgeuza Colins tahira wala si mimi.” Hapo akamshitua zaidi baba yake.

“Love, anazungumza nini huyu?” “Kwanza mimi si huyu. Naitwa Kemi Kasa. Mwanao ananitafutaga yeye mwenyewe akitaka nimsaidie mambo yake, ila hayataki matokeo. Mnafik…” “Wewe ndio mnafiki. Aliyemtafuta mwenzie leo ni nani kama sio wewe Kemi?” “Unakimbia swali la baba yako. Mjibu sasa kama mimi muongo. Muelezee ukweli wako juu ya utahira wa Colins, nikusikie hapa.” Kimya.

“Si umemuona alivyo? Anajua hawezi jitetea uongo hapa kwa kuwa mimi nipo, mpaka akawadanganye mkiwa peke yenu? Sasa nasikia na wewe Colins amekupania, wala huna pakukimbilia. Hata ujitetee vipi, tupo kapu moja kama parachichi. Acha unafiki.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bado dhoruba inaendelea.

Wakati Jelini akipigania uhai wake huko hospitalini, huku nyuma kila mmoja anajitahidi kujitoa lawamani, kwenye vyombo vya sheria, hata na kwa Colins aliyesikika kuwajia kama faru aliyejeruhiwa.

Nani ataangukia kisu? Nani atashikwa na Mfupa mkononi?

Chris ameshaona ipo njia ya kuwatoa. Baada ya yote hayo, watakubali kuwa ukurasa mmoja ili wafikie muafaka wa huo ukweli mmoja, wakiwa tayari wameumizana kwa kiasi hicho?

Usipitwe



CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment