Chris akaendelea.
“Kwanza kabisa nataka niwatoe paniki. Ile video haina ushahidi wa kutosha
kumfunga hata mmoja wenu. Kwa sababu haijaonyesha kama Kemi uliweka kitu pale. Unaweza
hata sema ulikuwa ukifukunza inzi au mdudu, tutaamua pamoja.” Hapo akampata
Kemi. Kidogo akatulia na kuanza kusikiliza.
“Mnaweza sema
mlivutiwa na ile juisi ndio maana mkamsimamisha.” “Mara zote mbili?!”
“Nisikilize Love. Uzuri hakuna ushahidi wa maneno. Ni maneno yenu nyinyi dhidi
ya yakwake. Nyinyi mpo wawili. Mkijipanga vizuri, mkaelewana, na
kuweka tofauti zenu pembeni, mnaweza kushinda kabisa na ndipo kuweka madai
yenu kwa ile hoteli. Badala yake mkaibuka mamilionea, mchana kweupeee.”
Hapo ndipo wote wakatulia. Akawa ameshapata mioyo yao.
“Tunakwenda polisi
sisi wenyewe hata kabla hamjafuatwa. Mnajisalimisha na tunafungua mashitaka.
Tunashitaki ile hoteli kwa kusambaza taarifa zenu hadharani, mkiwa mmepaamini
pale kama sehemu salama ya starehe. Wamewachafulia jina, na kuweka maisha
yenu hatarini kwa jamii, inayowatizama sasa kama nyinyi ni wauuwaji.”
Chris akawapanga vilivyo.
Mpaka wanatoka hapo,
ni kitu kimoja. Wanazungumza ukweli ambao kwanza wameshauamini. Wamejipanga
vilivyo. Kemi huyu badala ya kukimbia nchi, anadalili za kulipwa fidia! Stori
ikabadilika. Tumaini jipya. Ujasiri ukarudi. Hofu ikaondolewa.
Kuliko Unguzwa Mpini, Kukaachwa Jembe Lina Moto Unaokataa Kupoa.
Colins yeye
alishindwa kulala. Alirudi nyumbani kwao, akaingia chumbani kwake na kurudia
kuitizama ile video tena taratibu akijiweka upande wa Love na Kemi vile ambavyo
wanaweza kujitetea. Mwishoe na yeye Colins akafikia kufikiria kama vile
Chris.
Ukweli hapakuwa na
ushahidi wa kutosha wa kumfunga Kemi hata Love. Kemi alionekana kunyanyua mkono
juu ya ile trei iliyokuwa imebeba glasi ya vinywaji ikiwepo na hiyo juisi ya
embe aliyokunywa Jelini. Na kwa sababu ya giza hapakuonekana kama ametia kitu
kwenye ile juisi. Na mbaya zaidi, ile juisi hata ilipowekwa mezani ambako
alikuwa amekaa Jelini na Colins, mwangani, haikuonekana kubadilika
rangi. Bado ilibakia kuwa rangi nzuri sana ya embe hapo kwenye glasi. Colins
akabaki akikuna kichwa akijua wazi hawatakamatwa kwa hilo. Akaona aongeze
uzito.
Kwa kutumia tena Ip
adress ya Love, akaingia tena kwenye akaunti ya kampuni anakofanyia Love, na
kuchota mapesa, kisha kumrushia Kemi. Ila safari hii alichota yakutosha tu ili makusudi
kugutusha muhasibu siku inayofuata. Akafanya yake na kubaki akifikiria endapo
hawata kamatwa, au kutiwa nguvuni na vyombo vya sheria, atawaadhibu
vipi! Akabaki akifikiria.
Ujanja Kuwahi.
Wakati hayo yote
yanaendelea usiku huo wenye mengi, kila mtu akijipanga kivyake, yeye Jelini
bado yupo hospitalini akipambania uhai wake. Kina Kemi wakatokea kituo
kikubwa cha polisi cha Oysterbay, wakisindikizwa na wakili wao pamoja na wazazi
wa Love.
Wakaonyesha ile
video, na hapohapo wakashitaki ile hoteli kwa kuvujisha taarifa
zao wakiwa wamepaamini pale ni sehemu tulivu ya starehe, kuwa wangelindwa
kama wateja, lakini sasahivi wameanikwa hadharani. Wakasema wao hawapo
tena salama, jamii inawachukulia ni kama wauuaji.
Wakaeleza kuwa ile
hoteli ndio inayotoa vyakula vyenye sumu, hawapo makini na vyakula
pamoja na vinywaji wanavyotoa kwa wateja wao. Wakisaidiwa na wakili wao, wakatengeneza
mashitaka yao kwa makini, mpaka wakafanikiwa kuandikisha kesi nzito.
Ndipo wakaondoka kituo cha polisi, lakini mpaka hapo hakuna mtuhumiwa
aliyekwisha kamatwa. Kila mmoja akimshitaki mwenzie.
Mpaka hapo, usiku huo
kituo hicho cha polisi wakafungua kesi mbili. Mashitaka tofauti tofauti,
lakini kisa kinachomlenga mtu mmoja. Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Saa kumi alfajiri
ndio Love na wazazi wake wakaweza kurudi nyumbani. Hata Love aliamua kulala tu
kwao. Kwanza bado alijawa hofu. Hakujiamini tena kurudi Kigamboni, ambako
wakati wowote alijua Colins, kiumbe aliyekuwa akimdharau sana, gafla
akageuka tishio kwake kwa namna ya ajabu sana. Akajua akiwa huko, tena peke
yake, anaweza kumfikia bila shida kwa sababu ile nyumba ni kama ni ya Colins
pia. Ukimya wake tokea apone, na usiku huo pia, akijua anajua alichomfanyia,
ndio ukazidi kumuogopesha zaidi.
Akaingia kwenye chumba ambacho bado
kinatambulika kama ni chake hapo nyumbani kwao, na bado kilikuwa na vitu vyake,
akalala hapo kupata usingizi mfupi, kuwahi majukumu ya siku inayofuata.
Kila Jambo Na Majira Yake.
Ni kweli kila kitu kina majira yake, kila
jambo duniani lina wakati wake. Wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa;
wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna kilichopandwa; wakati wa kuua
na wakati wa kuponya; wakati wa kubomoa na wakati wa kujenga;
wakati wa kulia na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza
na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe na wakati wa kuyakusanya
mawe pamoja; wakati wa kukumbatia na wakati wa kuacha kukumbatia; wakati wa kutafuta na
wakati wa kupoteza; wakati wa kuhifadhi na wakati wa kutupa;
wakati wa kurarua na wakati wa kushona; wakati wa kukaa kimya
na wakati wa kuongea; wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia; wakati wa vita
na wakati wa amani. {Muhubiri 3:1-8}
Wakati Wa Kuua Na Wakati Wa Kuponya
Hilo andiko likatimia
kwa Jelini naye. Baada ya vipimo vya kina ndipo wakajiridhisha hayupo
hatarini tena. Mmoja wa daktari aliyekuwa akiongoza hayo matibabu yake, akawafuata
kama aliyekuwa ametumwa kwao. Akawasogelea pale walipokuwa wamekaa. “Jelini
amepelekwa kwenye chumba ambacho atapumzika. Mpaka sasahivi alipo hayupo kwenye hatari ya kifo, na hana
madhara yakudumu ya hatari yanayo mkabili.” “Unamaanisha nini, maana tuliambiwa
ameanza kutapika damu!” Akawahi Ezra.
“Ametapika sana kiasi
cha kukwangua koo. Na kwa jinsi alivyokuwa akitapishwa imekwangua hata tumbo
pia. Muda, dawa kiasi, na vyakula sahihi hata utumbo utarudi kwenye hali ya
kawaida. Ni kuepuka vyakula na vitu vyenye tindikali. Otherwise, msiwe
na wasiwasi. Na bado tutamwangalia mpaka kesho. Akiendelea hivi, ataruhusiwa tu
kurudi nyumbani.” Akaendela taratibu akijaribu kuwatoa hofu.
“Kama nilivyotangulia
kusema, hayupo kwenye hatari ya kifo. Mnaweza kwenda kumuona, ila
amelala. Amepewa dawa ya kuzuia kutapika na ya usingizi ili kumpumzisha kabisa.
Ila dawa zikiisha mwilini, anaweza kuzungumza kabisa, na sisi tulizungumza naye
kabla hatujamlaza.” Gafla wakamsikia mama Jema anaanza kulia. Alilia mpaka
akakaa chini kabisa.
Bwana mama alilia
huyo kama ambaye amepewa habari za msiba, mpaka daktari akajaribu kurudia
akidhani hajaelewa. Lakini asijue ule mshituko wa kuambiwa Jelini amenyweshwa
sumu, ukafunga kabisa hisia za machozi mpaka hapo ndipo alipoweza toa hofu
yake.
Yaani hata alipokuwa
akionyeshwa tukio zima la Jelini kule hotelini na kutegwa na Kemi mpaka
kupasuka kichwa, yeye akili yake na hisia viligoma kupokea na kutafasiri
zile taarifa. Yeye mawazo yakabaki kwa mwanae aliyekuwa ana karibia kufa. Yaani
hata Kasa alipokuwa akizungumza naye, akili ilikuwa imekufa ganzi, hajui
afikirie nini au afanye nini. Ile kumuangalia Ezra ilikuwa ni asaidie ushauri.
Jema alipowahi, ikawa bora kwake.
Muda wote alikuwa
kama amekufa ganzi kabisa! Kimya mpaka hapo alipoambiwa hakuna hatari tena, yaani, Mungu
hakuwa tayari naye, ndipo akafunguka na kuanza kulia mpaka Jema
alipomwambia waende wakamuone.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wote wakaongozana
kwenye hicho chumba, lakini alikuwa amelala hata hajui alipo. Ezra akaenda
kuinama pale pembeni yake akimwangalia jinsi alivyolala pale, mwishoe na yeye
akaanza kulia mpaka Junior akaenda kumtoa pale na kutoka naye nje kabisa. Mengi
yalikuwa yakiendelea kichwani mwake. Alipotulia ndipo wakarudi.
Walikaa pale mpaka wakaamua kuondoka, ila
wakakubaliana mama Jema na Ezra ndio wabaki. Sasa Junior naye hawezi
ondoka hapo bila Ezra. Wakajikuta wamebakia watatu. Kwa ahadi ya
chochote kitakachotokea watoe taarifa kwa ndugu wote hao. Mchungaji akafanya
maombi ya shukurani, ndipo wakatawanyika.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kimya hapo chumbani kila
mtu akitamani angalau afungue macho tu. Ezra alikaa pale akimsihi Mungu
amtunzie huyo Jelini, akimkumbusha Mungu yeye ni yatima, na Jelini ndio kila kitu chake. Akaomba yote mpaka
akasogeza kiti kabisa pale karibu ya kitanda, akamshika ule mkono ambao haukuwa
na dripu. Akajikuta akirudia maombi yaleyale akimkumbusha Mungu kana kwamba
anatatizo la kusahau! Mwishoe na
yeye akapitiwa na usingizi. Chumba kizima wakalala kwa uchovu na hofu ya massa
machache yaliyopita.
~~~~~~~~~~~~~~~
Majira ya saa 12
alfajiri, wakati mchungaji, mkewe na Emelda wameingia hapo na nesi naye alikuwa
ameingia kuongeza dripu ingine iliyokuwa ikienda taratibu. Maana alishawekewa
nyingine kwa haraka. Hizo zilikuwa zakumpa tu nguvu. Kwa hiyo zilikuwa zikienda
taratibu.
Wakati wanaelezea
hali yake kwa waliorudi asubuhi hiyo na kifungua kinywa kwa wote, maana mama
mchungaji ni kama alirudi kwake kupika tu. Aligeuza na kurudi hospitalini hapo akiwa
na Emelda pia na vyakula vingi tu.
Wakati wakitoa
taarifa zake, Jelini akawa anatoka usingizini. Akawatizama kwa muda kama ambaye
anajaribu kuelewa. Wote kimya wakawa na wao kama wamepigwa na butwaa kumuona amefungua
macho. Kisha wakamuona kama amegutuka,
akaanza taratibu kuficha mkono wenye pete ile ya uchumba, ambao ndio una
sindano ya dripu.
“Huo mkono una dripu
Jelini! Acha kujiumiza zaidi.” Junior akamuwahi. “Nilikwenda
kuwekana sawa na Colins. Sijafanya jambo baya.” Akajitetea huku
akificha mkono, kwa sauti iliyojaa usingizi. Ezra akamuwahi. “Naomba utulie.
Mimi mwenyewe sithubutu kutoa hiyo pete
kidoleni mwako Jelini. Ni maombi yangu isiwahi kutoka. Nipe huo mkono.”
Ezra akamvuta huo mkono taratibu.
“Sikufanya
jambo baya!”
“Najua Jelini. Hakika wewe ni muujiza wangu. Namshukuru Mungu amenihurumia na kunirudishia
wewe.” Akaubusu ule mkono kwa muda mrefu akiwa amefunga macho, wakamuona
machozi yakitoka. Jelini akamuhurumia.
“Pole
Ezra. Najua nimekushitua. Lakini sikuwa na jinsi ingine. Tumbo lilivyoanza tu
kuvuruga, na kwa kuwa nilishamuona pale Kemi na Love, nahisi kama Mungu tu,
nikajua kuna kitu wameniwekea. Nikakimbia na kukupigia simu.” “Na ndio pona yako.
Ungechelewa tu, usingepona.” Junior akajibu yeye wakati Ezra akijifuta machozi
na kujaribu kutulia.
Wakamsimulia na kumuonyesha ile video. Jelini
akashangaa sana, ndipo sasa wakamuonyesha ile ya ofisini kwa Kasa, alishituka
sana. “Mmepata wapi hizi video!?” “Kwanza
mpaka sasahivi zimeenea mtandaoni! Kazi ya Colins.” Akamwangalia mama yake. “Mimi sijafanya jambo baya, mama. Nilikwenda kumalizana
naye tu. Mimi natulia na Ezra.” Akawa akijitetea kwa mama yake akitokwa
machozi taratibu. Mama Jema akaanza kulia tena. Ila safari hii kwa kwikwi, mpaka Jelini akamuhurumia na
kuzidi kulia. Alilia mama Jema mpaka akatoka hapo chumbani. Mama mchungaji
akamfuata.
Baada ya muda
wakarudi akiwa ametulia. “Pole mama. Pole sana.” Mchungaji akamwambia mama
Jema. Kisha akamsogelea na Jelini aliyekuwa akibembelezwa na Ezra. “Pole sana
Jelini, binti yangu. Pole sana.” Akamuongelesha kwa upendo, kama baba kwa binti
yake kweli.
“Ningekushika mkono
ila mmoja ndio huo una sindano na mwingine umeshikiliwa kana kwamba
utakimbia!” Wote ndio wakaangalia na kuanza kucheka. “Acha nishike baba yangu.
Niliingiwa na hofu! Hakika sijawahi ogopa
vile maishani. Sikujua kama…” Akashindwa kuendelea, wakamuona anapambana na
machozi.
“Nilijua. Pole sana
Ezra. Pole. Lakini leo wote tuna sababu ya kumshukuru Mungu. Jelini amepona
mauti. Mungu akipenda leo atalala nyumbani.” “Nilitaka niombe angalau niende
naye nyumbani. Nishinde naye mpaka mama yake akiwa anatoka kazini, ndio
nimrudishe.” “Naomba nizungumze na nyinyi wawili hapo nje.” Junior na Ezra
wakaangaliana kama wanaoulizana. ‘Tumefanya nini tena!’ Mchungaji
akawaona. “Sasahivi, Junior na Ezra.” Akatangulia nje, wakamfuata.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Kuna nini tena!?” “Wazo
la kwenda kushinda na Jelini, nyumbani kwako, nyinyi wawili, kipindi kama hiki,
HAPANA.” Wote wakabaki wakimwangalia kwa mshangao. “Unanisikia Junior na Ezra?”
“Kwa nini?!” “Nisikilize Ezra. Jana ulikuwa ukilia, ukijilaumu jinsi
mlivyoachana mara ya mwisho na Jelini. Ukawa ukilia ukisema wewe ndio
umemsababisha mpaka akaenda kwa Colins. Ungezungumza naye vizuri, ungemuongoza
vizuri yasingempata hayo yote. Si ndivyo?” “Wala sipingi!”
“Ewaaah! Sasa katika
hali hiyo, na yeye anajilaumu kwa yake, mkajikute mpo wawili tu, baada
ya kuombana msamaha, furaha ya kupona Jelini! Unafikiri ni nini
kinafuata?” “Baba!?” Ezra akashangaa sana. “Kwani unafikiri faida moja wapo za mpishano
ndani ya ndoa ni nini?” Kimya. “Kwenye kupatana. Mkifanikiwa mkafikia
sehemu nzuri kila mmoja akakubali yaishe msameheane! Mtakuja kuniambia.” Junior
akaanza kucheka akiwa ameshaelewa.
“Mimi nipo makini.
Siwezi anguka dhambini.” Ezra akapinga. “Maana wewe mwenzetu si mwanadamu kama
sisi? Maana wote tumeamriwa kuikimbia zinaa. Halafu wewe ndio unataka kuikimbilia!?
Hapana Ezra. Huyu binti anakwenda kuugulia kwao. Wewe utaenda kumtembelea.
TENA baada ya kazi. Huwezi kuacha kazi sababu ya kupendana. Hilo hapana.”
“Sasa kipindi hiki si ndio ananihitaji!? Nisipokuwepo kipindi kama hiki, si
ndio kutojali huko??”
“Nisikilize Ezra. Hapo
ulipo upo kwenye kuweka msingi mgumu sana wa hatima yako na Jelini. Ukitetereka
tu, ukaruhusu nahisia zikuongoze, ukatoa mwanya wa kosa dogo tu, ambalo
sasahivi unaweza kulitolea sababu ya kwa nini ulifanya, na kujipa amani
kwenye hilo. Maana sasahivi si jamii inajua Jelini ni kama mkeo!
Una baraka za wazazi! Halafu utajiambia si nitamuoa tu! Si ni kama au atakuwa
kama mke wangu tu! Utaruhusu hili na lile. Na kweli Mungu atasaidia, mtaoana,
kama hapajapatikanika na mimba kabla ya ndoa. Ambayo si tatizo sanaaaa. Maana sisi
si tunaamini nguvu ya toba! Basi tunaamini tukitubu, tutasamehewa.
Mtatubu, tutabariki ndoa yenye mtoto tayari, mtaanza maisha.”
“Lakini kumbuka,
mlishafungua mlango wa kosa tokea mwanzo. Unajua vipi mkija kujaribiwa huko baadaye,
na watu wengine, hamtarudia kosa?” “Baba!??”
“Unakataa nini Ezra,
mwanangu!? Huoni msingi wa anguko kubwa sana wa ndoa nyingi, ila hawataki
tu kuliweka wazi. Kama ulianguka na yeye, mkapona. Kwa
sababu yeyote ile mtakayoichagua nyinyi, unajuaje kama hapo ndio itakuwa mwisho
wa kujaribiwa kwenu? Tuseme wewe utaishia kuzini na yeye tu, kisha kumuoa.
Unajuaje kama yeye atakapokuja kujaribiwa tena, na mwanaume mwingine je? Hata
akiwa ameshakuzalia watoto wa tatu! Akakumbuka alikosea na wewe,
ikawa SAWA. Sasa kwa nini asikosee huko na mwanaume mwingine tena na kutubu?
Kwa sababu yeyote ile atakayochagua tena, kama mlivyofanya naye.” Wivu
tayari kwa Ezra.
“Si Mungu alisamehe uzinzi
wa kwanza uliofanya naye! Sasa huyohuyo Mungu atashindwa vipi kusamehe
ushareti wa baadaye? Tena na yeye akatafutia sababu nzuri sana, ambayo
mimi na wewe hapa tuliposimama, sasahivi, hatuna, kwa kuwa tunampenda
Jelini, tunajiambia hataweza kufanya, kwa sababu pia bado hamjaingia
kwenye ndoa. Hamjajua changamoto zenu za ndoa zitakazowakabili.”
“Nakuhakikishia Ezra,
kwa aina ya mwanamke uliye naye, anavyogombaniwa na kusubiriwa
huko nje, kupokelewa kwa mikono yote miwili, utakapo mfundisha kukosea
sasahivi hata mara moja tu, shetani atarudi baadaye na mfano wako
wewe mwenyewe. Utakuja kukumbuka haya ninayokwambia kama usipokimbia
sasa.”
“Tena mbaya zaidi,
Jelini anakuangalia sana wewe Ezra, kama mfano wa kuiga. Usifikiri ni
jambo dogo kukupigia wewe simu wa kwanza akiwa kwenye hatari ya kifo na
hamkuwa mmeachana vizuri. Ana imani na wewe.” “Kabisa Junior!” Mzee akaafiki.
“Na usifikiri pia ni
jambo dogo kwa Colins tuliyemsikia ni mkorofi hakubaligi kushindwa linapofika
swala la Jelini, eti leo anakutambua wewe! Tena kwaheshima kwa kiasi
hiki! Sio kitu kidogo Ezra. Mimi mzee amenifanya nifikirie, nimeona ni bahati
imekujia mara moja. Upo na nafasi nzuri sana ya kujenga mke utakayefaidi
matunda yake kwa mpaka kifo kitakapo watenganisha au kuweka msingi
mbovu, nyumba ije iwaangukie baadaye. Tujikaze tuoe mapema, kufupisha haya
maisha ya kukaa mbalimbali.” Wakamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha
taratibu.
“Upo sawa?” “Basi
naomba leo nikamsaidie huko kwao! Angalau tu nikae naye. Kesho narudi
kazini. Nakuahidi baba yangu. Na nimeelewa. Nitaongeza umakini lakini angalau
leo niwe naye sehemu itakayonilinda na mimi, lasivyo sitaweza fikiria
popote nitakapokuwa bila ya leo kuwa naye na kuwekana naye sawa. Kwanza namuona
bado ana hofu akihisi nimemkasirikia kwa kuonana na Colins bila ya kunitaarifu.”
“Nimemuona anavyohofia utamuacha. Anaficha pete kabisa!” Junior
akaongeza.
“Huyu binti ameamua
kutulia na wewe Ezra. Hakikisha unaomba hekima jinsi ya kumuongoza.” “Na
namuona si mbishi na ni kama amekubali Ezra amuongoze na kutaka watu
wajue yupo chini ya Ezra. Hata Colins alimwambia tokea tupo njiani.
Unakumbuka?” “Nakumbuka ndio maana najilaumu. Niliruhusu wivu ukanifanya
nishindwe kufikiria. Nitaongeza umakini.” Mzee akaridhika, akajua somo
limeeleweka.
“Sasa jioni mama yenu
ameamua kuzungumza na mama Jema, tufanye ibada ya shukurani pale kwao.
Sisi kama familia namaanisha wakiwepo na wale mama zao wengine. Na sisi ndio
tutaleta vyakula na vinywaji.” “Nashukuru mzee wangu. Asante.” Wakataniana
kidogo ndipo wakarudi ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mipango ikakaa sawa. Mama
mchungaji akamruhusu mama Jema arudi nyumbani angalau aoge na kumpumzika. “Huyu
atatolewa, wala usiwe na wasiwasi, na sisi wenyewe tutamrudisha nyumbani.
Naomba ukapumzike.” “Na kumwangalia Jeremy. Nimemwambia hata shule asiende leo.
Yupo kwa Jema. Maadamu unanipokea hapa, acha nikamchukue, nimwandae aende
shule. Asikose shule. Ila kukiwa na chochote, tafadhali niambieni. Msiache, hata kwa kidogo vipi.” “Wewe usiwe na
wasiwasi. Nitabaki hapa mimi mwenyewe.” Mama Jema akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Nani Atalipa Kwa Kilichompata Jelini Ikiwa Wahusika Wamekana
tuhuma zao? Na Tayari Wana Mwanasheria Mzuri Anaye
wahakikishia Si Ushindi Tu, Bali Kuibuka Hata Mamilionea!
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment