“Nilijua
ningeenda, nikamalizana naye kwa amani, halafu nikuletee tu habari njema. Ulikuwa umekasirika Ezra!
Vile ambavyo sikuwa nimekwambia juu ya jumbe zake. Nikapaniki. Nikajua utanichoka na matatizo yangu, nikaona bora nirekebishe kwanza ndio
nikutafute tena.”
“Naomba wakati
mwingine, tutatue matatizo yetu pamoja. Hata kama yanatisha vipi, tufanye
pamoja. Umoja wetu ndio iwe nguvu yetu, adui hatatushinda. Ila tukitengana,
vita yetu itakua ngumu.” “Nimekosa Ezra.
Usikasirike.” “Na mimi nilikosea tokea, mwanzo. Niliruhusu wivu
unitawale. Ila wakati mwingine nitafanya vizuri zaidi. Samahani.” Akambusu na
mkono kabisa kisha akaanza kumfuta machozi.
“Sasahivi usione tena
wivu. Hata Colins nimemwambia nabaki na wewe tu, hata iweje. Kwa hiyo usi..”
Junior akaanza kucheka kwa sauti ya chini bila kutarajia. “Mwaya Junior!”
Jelini akalalamika. “Samahani Ezra, samahani sana. Hapo Nimeshindwa kujizuia.”
Wote wakajikuta wakicheka.
“Sasa unacheka nini
wakati mwenzio nipo matatizoni!” “Hivyo ulivyosema juu
ya wivu! Hakuna mtu anajiambia naanza wivu au naacha! Halafu wewe
umejitafutia matatizo Jelini! Tena wewe mwenyewe.” “Nyie Junior! Ujue mimi
nilijua wewe ni mtu wangu!” “Sana
tu. Na uwe unalikumbuka hilo wakati wote. Usiwe
unasahau.” Junior akaendelea.
“Ulitakiwa kusema
tokea mwanzo, juu ya jumbe na kusimamia msimamo wako wa kwanza, ule niliokusifia. Ungebaki salama.
Sasa shetani ameona umejipinga wewe
mwenyewe, ndio akapata mwanya.” “Si ndio nilipokosea nikapaniki!” “Hata
ukipaniki, wewe sema. Usitafute suluhu ukiwa na paniki, tena peke yako.
Tutakupoteza, utuache na majonzi
daima. Wenzio tunakuhitaji Jelini!
Kumbuka ulivyopooza kule Songea?” Jelini akanyamaza.
“Wote tulipoa sababu
wewe ulipoa. Ndio ujue wewe ni kiungo
muhimu sana kwetu. Ukiathirika kwa chochote, ujue umetuathiri na sisi wote.
Ndio maana unaona asubuhi hii tuliyopanga twende kazini, kutunza siku za
fungate, tupo hapa. Na bado wamekuumiza!” “Samahanini. Nilikosea na naahidi
kuwa mwangalifu zaidi.”
Huyo Jelini
anazungumza hapo, hajui hekaheka ya usiku uliopita. Hajui hata kama
alishahamishwa hospitali na Kasa. Kwamba wote hapo wanamfahamu milionea Kasa,
na amepigania uhai wake, pamoja na mtaalamu Colins. Usiku huo mchungaji na
mkewe wakatambulishwa ma ex wa
Jelini kila mmoja na hekaheka yake.
Anayetaka Usawa Mwisho Wake Uchawi.
Ndicho kilichompata
Raza. Ilikuwa mapema sana wakati Raza, anti lake Jelini akipokea simu ya
Kasa. Akashangaa sana. Akapokea kwa haraka. Ni Kasa, anayehonga pesa ya
kubadili maisha! “Nataka uende hospitalini sasahivi.
Umepelekee Jelini maua na chocolate.” Raza akashituka sana. Hakuwahi
hata kuropoka jina la Jelini kwa Kasa, na hata siku moja hawakuwahi
kumzungumzia Jelini.
“Unanielewa?”
Akauliza kwa sauti ya
ukali na amri. “Mbona hamna hata salamu!? Unajuaje kama
na mimi pengine nipo hospitalini?” Akamtibua Kasa zaidi, akitaka
kujifananisha na Jelini. “Usinipotezee muda Raza. Nina
usingizi sijalala usiku kuchwa. Leo sina muda wa kudanganyana. NATAKA uende sasahivi,
na unijulishe anavyoendelea yeye. Si vile anavyosema daktari. Hapana.
Kwa kuwa wewe ni mtu wako wa karibu, nataka uzungumze naye vizuri, umsikie
ili ujue anavyoendelea mpaka anavyojisikia nafsini kwake na
unirudishie majibu yakueleweka kwa haraka, ili niweze kufikiria na
kufanya kazi.”
Raza akashangazwa, asiamini.
“Sasa wewe
unafikiri Jelini ataniambia mimi la rohoni?! Kwani mimi kungwi wake?” Akawa kidogo
amekasirika, akajikuta anazungumza na Kasa kama yeye na si kama
alivyofundishwa na Jelini. Lugha ya kiustarabu.
“Yeye si
ndiye aliyekufundisha jinsi ya kuwa na mimi mpaka kitandani?” Raza akashituka
karibu atupe simu. Akashindwa kabisa kujibu. “Usifikiri
mimi ni mjinga. Uwezo mkubwa wa kufikiria ndio umenifikisha hapa nilipo. Ila
nasikitika tu, ulinikuta kipindi cha upweke, nikakufumbia macho mpaka
nilipolala na wewe ndio nikagundua nimelala na Jelini kupitia wewe.
Nikataka kukuadhibu vibaya sana kwa kunidanganya.” Raza akaanza
kuogopa.
“Lakini
nikafikiria kwa haraka, nikagundua unafanya kila kitu alichokuelekeza Jelini,
bila ya kukosea. Ukawa kile nilichokipoteza kwa Jelini.
Ukazungumza lugha yake. Na ukiwa na mimi kwa sababu alikwambia nipo makini,
hukosea hata mara moja kama uliyekuwa ukijikumbusha kila unapokutana na
mimi. Unavaa ngozi nyingine kabisa, na kuhakikisha hakuna kosa, kila
unapokuja kwangu, unahakikisha huji na simu zako.” Raza akazidi
kuogopa, maana ni kweli alikuwa hashuki na simu zake garini kila anapokwenda
kukutana na Kasa.
“Utulivu
unaokuwa nao kwangu si wako, ni wa Jelini. Lugha unayozungumza na
mimi pia si yako, ulifundishwa na Jelini. Ukamudu vizuri tu,
mpaka sasahivi hapa ulipopaniki, ndio umejisahau nakujitoa
makucha, ukazungumza kama wewe. Mpaka hapo umenielewa, au unataka uniudhi
zaidi? Nikwambie ni kwa nini nakupa pesa yangu, tena nyingi?” Kimya.
“Ili uache kujiuza
kwa wanaume wengi mpaka mawaziri na madereva wao, utulie. Niendelee
kumpata Jelini kupitia wewe.” Ulikuwa ni udhalilishwaji wa hali ya juu kwa Raza, lakini
aliingiwa na hofu akawa kama amekufa ganzi, ila aliweza kusikia maumivu sawia
ya wivu. “Nakufahamu Raza, anti lake Jelini.”
Hapo akamalizia na kummaliza vilivyo kwani ndivyo anavyoitana na Jelini.
“Ulitaka
nimnunulie maua gani?” “Umnunulie maua kwani wewe ndiye unayempa au mimi!?”
“Basi nielekeze vile unavyotaka, nitafanya. Maana mimi haya mambo siyajui.” Haraka sana
akakumbuka nafasi yake hapo, kwa huyo mzee. Akajishusha asije haribu. “Ndio maana tokea mwanzo kama ungekuwa umenisikiliza kwa
makini, nilikwambia NAKUTUMA kwa Jelini. Ukinunua wewe
na kumpelekea itakuwa na maana gani! Si itakuwa ni kama wewe tu ndio umenunua?”
“Samahani.”
Raza hakutaka kumkorofisha kabisa Kasa.
“Tukutane
nikukabidhi vitu vyote ninavyotaka umpelekee. Mimi ndiye nimenunua, wewe
ni mpelekaji tu.” Kisha akaongeza kwa msisitizo. “Na Raza, kuwa makini
sana unapozungumza na Jelini juu yangu. Chochote kitakachotufanya tuwe mbali
zaidi na hivi tulivyo sasa, ukiwa wewe umesababisha, ujue utanikorofisha
sana na hutapenda upande nitakao kuweka.” Mzee akapiga mkwara.
“Siwezi
kufanya hivyo. Kwanza mwenyewe Jelini ameniambia hataki hata kujua kama
ulinikubali au la. Na hataki kujua kinachoendelea kati yetu. Amenionya kabisa
tusikuzungumzie tena. Kinachoendelea kati yetu, hataki kabisa kujua. Na
amenionya hata nisiwaambie watu kama yeye ndio amet…” “Hayo ni ya wakati
mwingine. Sasahivi nataka utoke kitandani, ukamuone.” Kasa alisikika
hataki kupotezwa malengo.
“Sasa
akiuliza nimejuaje alipo na kama ni mgonjwa?” “Wewe hujapata habari zake kuwa
amenyweshwa sumu?”
Akashituka sana. “Hapana! Jana nilibakisha simu moja tu
ambayo ni ya mambo maalumu. Na niliwahi kufunga hii saluni mpya. Halafu kwenye
hii saluni mpya ninayokuwepo muda wote wateja wangu si kama wale wa kule. Ni
kina dada wanao jiheshimu. Wakija pale hawana maneno mengi na hata wafanyakazi
wangu wa huku hawana maneno maneno. Kwa hiyo sipati yanayoendelea kwa haraka.”
Akaongea kwa huruma.
“Sitaki
tugombane Kasa. Wewe nitume utakapo, nitafanya. Umenisaidia maisha yangu,
angalau sasahivi nalala nikiwa nimetulia nina uhakika wa wanangu kwenda shule
bila mahangaiko ya zamani. Sikupenda yale maisha, wala sikuchagua. Ila mume
wangu alinitaliki na kuniachia watoto wote na mimi sina wazazi wa kunisaidia.
Ikabidi kupambana kwa kila namna ili wanangu wasome na angalau waweze kupata
hata mlo. Lakini huyo anayekwambia habari zangu, kama ni mkweli kwako,
atakwambia nimetulia. Nimeachana na wanaume karibia wote, nime…” “Kuwa makini sana na unachotaka kuzungumza baada ya hapo.
Maana uongo wa namna yeyote ile sitakusamehe Raza, haswa kwa siku ya leo
ambayo Jelini yupo hospitalini. Umenielewa?”
“Lakini
kumbuka na mimi ni binadamu Kasa! Nipo mpweke kama wewe ulivyosema. Hujawahi
nifungulia moyo wako kama Jelini alivyokuwa akiniambia unavyokuwa ukiwa naye.
Unaniita nyumba za kulala wageni, hujawahi nikaribisha kwako hata mara
moja! Tena unaniita mara chache sana, halafu ni pale unapopenda wewe. Jelini
aliniambia huwa hutumii kondumu kabisa, kwanza hupendi, lakini kwangu
unakua mkali kabisa kwenye swala la kondomu, tena unanipima UKIMWI kila
tukikutana! Unafanya mapenzi na mimi vile unavyochagua wewe, kwa staili zako
wewe tu, hutaki kabisa na mimi nifanye kwa uhuru wangu!” Akalalamika ila kwa
heshima.
“Hatuzungumzi
Kasa! Nakujua kupitia Jelini! Tena kwangu haupo hata nusu ya alichoniambia
Jelini! Mpaka nadhania amenidanganya! Hujataka hata kunifahamu mimi moja kwa
moja ila kupitia watu wanao kuletea taarifa zangu! Na mimi ni binadamu Kasa.
Napendwa kujaliwa.” “Wewe si kama Jelini. Jelini alinipenda mimi kama
Kasa. Ni mwanadamu pekee anayenifahamu mimi, na hajawahi niomba pesa
hata mara moja ila kunitaka mimi kama mimi.” Raza akashangaa sana, asiamini.
“Lakini
wewe ulikuja kwangu kwa nia moja tu. PESA. Na ndizo ninazokupa kila mara unaponiomba.
Si kweli?” “Na nakushukuru kwa hilo lakini…” “Tafadhali fanya haraka ukamuone
Jelini hospitalini. Hayo mambo mengine unayotaka kuanzisha sasahivi, sina
muda nayo. Wewe upo kwangu kama wengine tu. Kutaka kunitumia. Usinidanganye.”
“Kujibu
swali lako, ukifika hospitalini, wewe mwambie Jelini umeona mtandaoni
ndio umeamua kwenda kumuona. Nakutumia sasahivi video yake ya jana usiku ili
ujue utakacho zungumza naye. Kisha mpe pole. Jelini hana makuu,
ukimuendea vizuri, hatakuhoji kama hivi. Anachotaka maishani ni kupendwa
na kujaliwa tu. Kufika kwako pale, hakutazua maswali ila furaha.
Sasa usinicheleweshe. Kila kitu nimeshaandaa. Tukutane upeleke.” “Natoka
sasahivi.”
Simu ikakatwa. Raza akahema kwa nguvu huku akijaribu kutulia maana alikuwa
akitetemeka kwa hofu, hasira na wivu juu.
Wakati Wa Kutafuta Na Wakati Wa Kupoteza.
Alimkuta Jelini amelala usingizi mzito. Chumba
kimetulia kweli. Alibakia hapo na mama mchungaji tu. Wengine wote waliondoka.
Emelda alikuwa na ugeni nyumbani. Lazima arudi, asiwaache peke yao na mama yake
mgonjwa. Ndio mchungaji akarudi naye nyumbani. Hao mapacha ndio walilala hapo,
ikabidi warudi nyumbani kujisafi, na kukimbilia kazini kwani waliambiwa Jelini
angelala siku nzima. Hapakuwa na maana ya kushinda naye.
“We Jelini?”
Akamuamsha kiafande. Jelini akashituka kutoka usingizini. “Anti,
kwema!?” Ikabidi amuulize kwani hapakuwa na tabasamu na jinsi alivyomuamsha pia
haikuwa kawaida yao. “Nikuulize wewe uliyelala hospitalini!” Akajibu
mpaka mama mchungaji akaweka kila kitu pembeni ya kochi na kubaki akiwatizama
na kusikiliza.
Jelini akabaki kimya.
“Na maua yako pamoja na chokleti, sijui pipi hivyo hapo. Usijesema hujapokea
kutoka kwangu, ukadhania ni mtu mwingine ameleta.” Jelini akageuka kuangalia.
“Kwamba huamini au?” “Kwema!? Maana naona umekuja kuniona inakua kama umelazimishwa!?”
“Huna shukurani
wewe! Ulitaka nikufanyie nini!? Nimekuja kukuona halafu unanipa maneno ya kejeli?
Umenigeuza mimi mtumwa wako! Umeniingiza mahali ulipojua sitapendwa
ila ukaniuza ili nikafanywe mimi mtumwa! Sina ninachofanya nikakufikia!
Eti leo naambiwa kila kitu nafanyiwa kwa sababu anakupata wewe kupitia
mimi!”
“Na wewe ukanifanyia kusudi.
Ukanifundisha nikawe kile ulichokuwa wewe, ili yule bwana abakie akikuwaza
wewe tu. Umeniuzia mbuzi kwenye gunia, ukiniambia anapenda
wanawake aina yetu. Nifanye kama ulivyonielekeza! Matokeo yake
ukanifunga kwa uongo! Mwanaume hanioni mimi, anakuona wewe
tu! Hanijui mimi na mautundu yangu, kwa sababu ulinidanganya
nikufuatishe wewe, ili abakiwe na wewe tu.”
“Na kweli umefanikiwa!
Mimi nilikuona mtoto mzuri, kumbe mjanja kuliko magumegume ya mjini! Umenitia kitanzi
shingoni, mimi ndiye ninayeteseka, mwenzangu unakula starehe tu. Natumwa
kwako kama mtumwa! Tena kwa kuamrishwa! Kwa kipi mno?” Jelini kimya
akimsikiliza.
“Nikadhani nimefua
dafu kumbe koroma!” Akaongea mengi akilalamikia pia kutokukaribishwa nyumbani
kwa Kasa, na mengine mengi. Jelini na mama mchungaji kimya wakisikiliza.
Akaongea kwa jazba mpaka akaanza kutulia. Raha ya ugomvi, mgombane. Sasa
hakupata uungwaji mkono, akaanza kupoa.
Alipotulia Jelini
akamuuliza. “Unakumbuka tokea mwanzo nakuja pale saluni kwako kwa zamani, ukawa
unaniunganishia kwa wanaume wenye pesa, jibu nililokuwa nikikupa?” Raza
kimya. “Eti anti? Sio kwamba nilikwambia mimi nataka wangu wa peke yangu,
kuchangia siwezi?” “Sasa kwa nini mimi ukaenda kunitega?”
“Kwamba umesahau
gafla ua la? Si wewe ulikuwa ukinishangaa kwa nini namuacha Kasa, nakupa
wewe kwa sababu ulizoita za kitoto? Nikakwambia namuacha, na mihela yake
yote, natafuta wangu wa peke yangu. Ukanicheka sana. Nikakupa Kasa na maangalizo
yake. Sikukutuma ikaishije naye. Tena nilikwambia namuacha Kasa sababu
nimegundua mwanamke aliyeniambia anamuacha ili tubaki naye, hajamuacha.
Nimemfumania. Unakumbuka ulinicheka sana tena ukasema wewe unamtaka
Kasa kama alivyo, huna shida au hutaki wako wa peke yako kwani
yeye roho! Unakumbuka maneno yako mwenyewe?”
“Sasa kwani kugeuzwa
mtumwa?” “Kinacho kuliza hapo ni wivu kitu ulichonicheka nacho
mimi. Umeona Kasa ameweka thamani kwangu kuliko wewe, ndicho
unacholilia. WIVU. Tena ni kitu ambacho unajipinga wewe mwenyewe. Maana
si kweli kama nimekuuzia mbuzi kwenye gunia! Nilikutambulisha kwa KASA, ukamkimbilia
na ukanishukuru sana, ukiwa umefurahishwa na hayahaya mapungufu
yake ukasema ndicho kitu unata, hutaki wa peke yako ili uendelee
na wanaume zako wengine. Umesahau?” Kimya.
“Kwa hakika umenikosea sana anti, na sitaki
tena mahusiano na wewe.” Hapo akashituka akajua ameharibu. “Yaani hivi ulivyonifuata
hapa leo, na kunitusi mbele ya mama mkwe wangu kwa chaguzi zako
mwenyewe za maisha, umeua mahusiano na mimi.” “Acha hasira anti! Nahisi
ni usingizi tu.” “Basi beba maua yako na vyote ulivyoniletea, peleka kwako na
mwambie Kasa, ameniudhi kupita kiasi.”
“Jelini u..” “Hapana
anti. Wewe si mtu mzuri na unataka kuniharibia mwenzio kwa
mwanaume ambaye mwenzio nilikuwa nahangaika kumpata, na wewe ulipokuja
siku ya kuchumbiwa kwangu, kwa wakwe zangu nilikwambia. Mungu amenipa
haja ya moyo wangu, roho yangu kwatu. Leo bila heshima unakuja kusema
mambo ya ndani hivi mbele ya mama mkwe wangu! Nia yako nini kama si kuniharibia?”
“Sikuwa nimemuangalia
vizuri. Sikujua kama ni mama mkwe wako.” “Hutanidanganya anti. Na
wala usitafute mchawi. Upo hapo ulipo na Kasa, kwa kuchagua kwako
wewe mwenyewe, na mimi nilikuonya tokea mwanzo, sikukuficha.
Nilikwambia pesa utapata, lakini jua hutakuwa peke yako. Ukasema wewe
mwenyewe una wako huko nje, hutaki wa peke yako. Na tena
nikakwambia ila yeye ana wivu sana, atakuchunga akikuchunguza. Unakumbuka
jibu lako.” Kimya. “Ulinijibu kuwa, Utampiga chenga akiwa amesimama.
Hatawahi kukukamata. Uongo?”
“Sasa waka…” “Wewe
sema umenogewa na Kasa, unamtaka moja kwa moja. Umeshindwa,
ndio unamtafuta mchawi. Lakini Kasa ni mfupa wa mbwa, wewe anti hutamuweza
hata kama unajiona mtoto wa mjini. Maadamu umeshaanza kupokea pesa
zake, tena mbaya zaidi kama ulikuwa ukimuomba, ndio umeharibu
kabisa. Ashajua unamtumia kama watoto wake na watu wengine wote, ndio
maana hakuthamini.”
“Mimi nimeishi naye
yule, sijawahi muomba hata shilingi moja, lakini alikuwa akitoa kama
amepagawa. Na nilikuwa naye yeye kama yeye kitu kilichokushinda
wewe sababu ya haraka ya pesa, na nilikwambia, Kasa anaakili sana. Kuna ulipokosea
kidogo tu, akakukamata na…” “Ameniambia anajua kama wewe ndio
umeniunganishia kwake.” Kidogo Jelini akaogopa.
“Ila anasema alitaka kuniadhibu
ila akaona anakupata wewe kupitia mimi, ndio maana ameniacha. Ananichunguza
kupita kiasi na anahabari zangu za…” “Hayo yote nilikwambia anti.
Nilikwambia, huwezi kumchenga Kasa. Ukajiita wewe mtoto wa mjini, hawezi
kukukamata. Leo umekamatwa unakuja kunitapikia mwenzio, tena hapa
hospitalini!?”
Mama Jema akawa
anaingia. “Nisamehe anti langu! Nahisi…” “Hapana anti Raza. Umevuka mpaka na
mimi maisha hayo mwenzio nilishayaacha zamani sana. Nilikukabidhi
Kasa na nikafunga huo mlango japo Kasa ananitaka mpaka kesho.
Yupo tayari kunioa kabisa. Na majuzi tu ameniambia yupo tayari hata kuzaa
na mimi kama nataka, ilimradi tu turudiane. Lakini huko mimi nilishatoka.
Nilichokuwa nikikitafuta nimekipata.”
“Nimelala hapa sababu
ya kupambania penzi la huyu mwanaume wangu wa sasa. Anaweza asiwe
kama Kasa, lakini anti, ananipenda na nipo peke yangu kwake. Sitaki
chochote kitokee. Aliyetaka kutishia penzi letu nilipoona tu, nikaenda kumpiga
marufuku, ndio nimeishia kutaka kuuwawa. Halafu wewe leo unakuja kunitapikia
hapa mbele ya mama yake! Heshima yako na shukurani vipo wapi?”
“Ulikuwa ukihangaika
na wanaume wanao kuhonga pesa za machungwa, nikakupa Kasa, japo
hatuzungumzi juu yake, lakini naona mabadiliko yako. Sasahivi una pesa na
vitega uchumi vyakueleweka, tena kwa ajili yangu. Kweli hiyo ndio shukurani
yako kwangu?” “Unaninyanyasa Jelini?” “Hapana anti. Si mimi niliyekwambia sitaki
hata kujua maendeleo yenu? Sitaki kujua kama alikukubali au la! Na
nikakwambia hata kwa mashoga zako usinitaje kama mimi nimekuunganisha
kwa Kasa. Amebadili maisha yako, na mimi najua yote uliyonayo sasahivi ni pesa
ya Kasa. Bisha.” Kimya.
“Lakini ushawahi
nisikia hata kuja kukuomba shilingi au kuja saluni kwako, kuomba nipewe huduma
ya bure sababu nimekusaidia kufika hapo ulipo?” Kimya. “Sasa mimi mambo
ya uswahili sitaki, na wewe unataka kunipora tonge mdomoni.”
“Sirudii anti yangu.
Kwanza nakupangia bonge la kitchen party. Hapo ndio utaona shukurani
zangu kwako.” “Sitaki. Na leo ndio uwe mwisho kunifuata. Unataka kunipokonya
ndoa, mwenzio naipigania mpaka uhai wangu! Yaani hapa ninapozungumza,
naomba beba kila ulichokuja nacho, mrudishie Kasa mwenyewe.” “Jelini
anti langu!”
“Hakika kama huondoki
navyo, mimi natoka sasahivi na hivi vitu, namrudishia maana kwa jinsi
vilivyo najua yeye ndiye aliye nunua na kupanga hivi, wewe mbembaji tu.
Bisha.” “Wala hutoki hapo kitandani. Maadamu yeye ndio amevileta, ataondoka
navyo. Akikataa, basi mimi nita vibeba, nimrudishie Kasa mwenyewe na
ndipo atanijua mimi ni nani.”
Mama Jema akapokea.
“Na nakuonya.
Kaa mbali na Jelini. Siku nyingine ukitumwa kwake, mwambie yeyote aliyekutuma
kuwa, mama yake Jelini hataki na mwanae. Lasivyo ni kunichokoza,
na mimi sipendi uchokozi kwangu wala wanangu. Hapo utaniona
mbaya. Wewe si umezaliwa hapa mjini, basi ukinianza, nitakutafutia
kijiji chakuishi maana mjini utapaona pachungu. Haya, kusanya vitu vyako
vyote, potea. Alipo Jelini, ona kituo cha polisi. Toka.”
Akakusanya vitu vyake
yote kisha akamgeukia Jelini. “Najua nimekuudhi anti. Lakini naomba haya mambo
yasiende mbali.” “Wewe ndiye uliyeyaleta ya mbali, karibu yangu,
tena nikiwa mgonjwa! Umenikosea anti, wala huna mlango wa kurudia
kwangu. Ulitaka kuniharibia kwangu wakati kwako nilikutengenezea tena
bila hila! Leo unalia wivu wa kuja kugundua Kasa ananipenda mimi
dhidi yako! Hakika ondoka, maana mchumba wangu atarudi muda si mrefu, na sitaki
kumchanganya kwa mambo ya zamani ambayo sina hata mpango wa kurudia
kuyaishi tena. Tafadhali ondoka tu.” “Unakaribia kuniudhi, na hutanipenda.
Ondoka kama alivyokwambia Jelini.” Akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini akaanza kulia
kwa hofu. Mkwe ashasikia kila kitu. Na yeye hasira za kina Love zikamfanya
akaongea mengi. Sasa hajui anamtizamaje mama mkwe. “Kwani imekuaje tena!?”
Ikabidi amsimulie mama yake. “Nahisi ametumwa kwa
kulazimishwa. Ndio ananimalizia mimi hasira zake.” “Sijui nitamfanyaje
huyu baba! Kila nikimfikiria, simpatii jibu! Jana katokea, bila kutarajia.”
Jelini akashituka sana.
“Kasa alikuja hapa?!”
“Wala si hapa tu.” Ikabidi mama yake amsimulie kuanzia mwanzo mpaka mwisho. “Mungu wangu anisaidie jamani! Huyu Ezra atanichoka
mama!” “Nisikilize Jelini, na uache kulia.” Mama mchungaji akamsogelea.
“Utaolewa na mwanaume
anayekufahamu vizuri sana. Ezra si mkurupukaji, na si myumbaji. Ukilijua
hilo, itakusaidia kutulia na kufanya naye maamuzi kama alivyokwambia
asubuhi ya leo.” Mama mchungaji akaendelea.
“Wote hao ni maisha
yako ya zamani, waliogoma kuondoka japo wewe umesonga mbele. Wala
wasikutishe au kukuyumbisha. Wewe endelea mbele na maisha yako hizo ni kelele
tu kutaka kukuweka njia panda. Ukiyumba tu, ujue utakosa kitu
ulichokuwa ukikihitaji. Wewe tulia. Angalia ya sasa. Unaumwa. Unatakiwa
upumzike, ndio jukumu lako la sasahivi. Kasa anafanya nini na kwa nani,
hayakuhusu kwa sasa. Rudi kulala.” Akamtuliza mpaka akatulia.
“Sasa na wewe mbona
hujatulia nyumbani, umerudi tena?” Mama mchungaji akamuuliza mama Jema. “Siwezi.
Hapa siwezi kulala wala kufikiria, labda wamtoe hapa. Kwanza yeye huyu ni muoga
kweli wa hospitalini. Kumuacha hapa najiona kama namtelekeza! Acha tu
nikae naye. Wewe nenda.” “Mie hapa nimefika.” Wakabaki hapo wao wawili na
mgonjwa.
Siku Ya Kufa Nyani, Miti Yote Huteleza.
Akiwa ameamka kwa
kuchelewa sana siku ya kazi, na si kawaida yake, akawa akijiandaa kuelekea
kazini. Msichana wa hapo kwao akamgongea. “Kuna watu wanakuulizia dada.” “Kina
nani!?” “Hawajanitajia majina, ila wanaonekana wana haraka.” “Hivi wewe ni mara
ngapi unafundishwa ukipokea wageni uulizie taarifa zao kamili ili unapomuita
mtu ajue anakwenda kukutana na nani?” “Wamekataa hata kukaa dada! Wamesema
wanaharaka, utoke.” Love akashangaa sana, ila akatoka kwani alishakuwa amevaa
anakaribia kuondoka hapo.
“Love Simba?”
Wakamuuliza kabla ya salamu. “Niwasaidie nini?” Love akauliza kwa kujiamini.
“Twende.” “Hamuwezi kunibeba kama mzoga! Lazima mniambie mnakonipeleka na
nyinyi ni kina nani.” Love akaweka mgomo wa kutoka hapo na hao waliomjia
nyumbani, tena kwa wazazi!
~~~~~~~~~~~~~~~
Mipango Iliyojaa Chuki Na Usaliti
Kwa Colins Inaendelea kwa kina na umakini wa namna yake.
Anapanga Kwa Makini, Ili Kuhakikisha Anamfikia
Kila Aliyemuumiza Kwa Namna Moja Au Nyingine. Na Kila Atakayesimama Katikati Yake Na Amtakaye, Amekusudia Kummaliza Vibaya sana.
Anataka Kumfikia Love Na Kemi, Lakini Wazazi wake, yaani
Kina Simba Na Chris Tayari Wapo Katikati Yao wakimkingia kifua.
Ni
Nini Atafanya Akiwa Hana Tena Chakupoteza.
Mjumbe Raza & Kasa nao Je?
Mapenzi Na Pesa.
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment