Kwa kupaniki, asifikirie kwamba pale ni eneo la
hospitali, yeye akakurupuka akikimbilia chini ya hilo gorofa. Ile GPS
haikutoa eneo kamili alipo. Ila tu kuonyesha yupo hapo.
Akatoka kwenye lift kwa haraka akiangaza macho kila
mahali. “Uzuri wa Kamila si wa kujificha. Popote alipo anaonekana tu.”
Akawaza Colins huku macho ameyatoa. Hata mpaka hapo bado hakuwa na wazo kwamba
yupo eneo la hospitali. Akaanza kuzunguka mpaka akajikuta ametokea mapokezi.
Alipoona wagonjwa pale ndipo akili ikamjia pengine amefika pale kwa kuwa ni
mgonjwa. Wasiwasi ukazidi kumuingia.
Akamsogelea mmoja ya muhudumu na kumuomba ampishe kwenye
kompyuta yake ili aangalie kama kuna mgonjwa mwenye jina hilo. Akavuta keyboad
kwa haraka na kuandika jina la Kamila tu. Wakati mtandao unajaribu kutafuta
kwenye kumbukumbu zote zilizoingizwa humo, kuona kama kuna jina la Kamila,
mlinzi anayesimama pale mapokezi akarudi.
“Umemfanya nini?” “Nimempeleka getini, nimewaambia wale
askari wamuitie polisi. Mwaka jana alifanya hivyohivyo! Alikuja hapa akidai
mwanaume wake, kana kwamba hapa ni nyumba za kulala wageni! Akasumbua
hapa kwa muda mrefu mpaka tukamfukuza. Sasa naona leo ameamkia hapahapa hata
kabla hapaja pambazuka.” “Msichana mzuri, yupo kama amechanganyikiwa jamani!
Hapo atakua aliiba bwana wa mtu, na wenyewe wakamkomoa kwa kumfanya
chizi! Ndio wakomage kuiba mabwana za watu!” Colins akashituka sana.
“Yuko wapi?!” “Ni kichaa tu bosi wangu. Atakuja kurudi tu
tena, utamuona. Tumemtoa sababu anasumbua wagonjwa.” Colins akatoka hapo kwa
haraka kuwahi getini. Akakuta wakimsukumia nje na yeye amekazana anataka
kuingia ndani. Amechoka usoni, hata nywele hazija chanwa.
“Subirini kwanza, msimsukume. Mwacheni kabisa.” Wale
askari pale getini wakamuachia baada ya kumuona na kumsikia Colins. Alikuwa
akilia sana mpaka sauti ilikuwa ikikaukia. “Tulia kabisa, uniambie unataka
tukusaidie nini?” “Mimi nataka kujua walipomuhamishia Mike.” Akaanza akilia na sauti iliyokuwa ikikwaruza kwa kulia.
“Nimekuja
naye hapa, jana tu! Nilimleta kwa dharula akiwa anaumwa tumbo. Ila nikawa
nimesahau pesa nyumbani. Maana nilitoka naye nikikimbia. Nikamuaga yule muuguzi
kuwa narudi nyumbani kuchukua pesa, maana matibabu mengine waliniambia
yatahitajika kulipia ndio afanyiwe. Mike alianza kutapika damu. Mimi nikatoka
kwa haraka. Kufika njiani tairi ikapata pacha. Mpaka kuja kufanikiwa kufika
nyumbani, na kurudi hapa sikumkuta Mike pale nilipomuacha.” Akaendelea.
“Nimemuuliza
yule nesi, mpenzi wangu yupo wapi, maana nilimuacha hapa muda mfupi uliopita,
ananiambia yeye alikuwepo hapo usiku kuchwa, hamna mgonjwa mwenye jina hilo!
Nikaendelea kumuhoji ndio akaniitia askari akitaka nitoke kule walipolazwa
wagonjwa, eti napiga kelele, wakati mimi namuulizia mpenzi wangu!”
“Alikuwa akifanya fujo, bosi. Hapo anaongea taratibu.
Alikuwa anapiga kelele kabisa, anasema hatoki mpaka atoke na mumewe
sijui ni mwanaume gani! Wakati hata pale mapokezi wamemsaidia kuangalia, hamna
mgonjwa mwenye jina hilo aliyepokelewa hapa muda aliosema yeye! Akaambiwa
kiustarabu pengine amechanganya hospitali, atoke, hataki. Na yupo hapa
tokea saa 10 asubuhi!” Colins akawa kama ameelewa ila akawa amemchanganya tena.
“Jina ni nani tena?” Akamuuliza kutaka uhakika. “Kamila.” Akamtajia akilia. “Tafadhali tulia na samahani kwa
chochote ambacho umefanyiwa hapa, ambacho hujapenda. Samahani sana.” Kidogo
akaanza kutulia. “Nashauri turudi ndani kwenye ofisi yangu, tuanze kumtafuta
Mike. Si unakumbuka muda mliofika hapa?” “Ndiyo.” “Jina lake kamili na tarehe yake ya kuzaliwa vyote
unakumbuka?” “Ni mpenzi wangu!”
Akamjibu kama anayeuliza unaulizaje pingu polisi! Ila Colins akawa
mstaarabu, akamchukulia taratibu. “Sawasawa. Tuongozane.” Wakampisha, Colins
akaongoza njia, akifuata taratibu akilia.
“Hawaniamini!
Wananiona nimechanganyikiwa.” “Pole sana.” Colins
akaendelea kutembea akimfuata. Mpaka juu ofisini kwake. Akamkarimu maji lakini
akakataa. “Siwezi kula nikiwa sijui Mike alipo! Nahisi kuna kitu hakipo
sawa.” “Sasahivi, tutapata uhakika.” Akamjibu hivyo
ila akijua kwa hakika Mike alishafariki muda mrefu sana.
Ila akaanza kuhisi pengine alifia pale kwenye hospitali
yao. Akamuangalia pale alipokuwa amekaa. Amejawa wasiwasi kama ambaye kweli
amepotelewa na mtu muda mfupi uliopita, anamsaka. Akafungua kompyuta ya
hapo hospitalini. Akaanza kumuuliza taratibu.
“Unakumbuka kumuandikisha pale mapokezi muda uliokuja
naye?” “Ndiyo! Wasinge mpokea wodini bila kupitia mapokezi.” “Ni kweli. Jina
lake kamili na tarehe ya kuzaliwa?” Akawa akimuuliza macho kwenye kompyuta
akiwa na uhakika kabisa na anachotafuta. Ila akataka kuelewa vizuri. Kwamba
bado Kamila haamini kama Mike alifariki au imekuaje! Maana alikumbuka
kwenye moja ya jumbe zake ni kama alitambua kutokuwepo kwake! Akaendelea
kusaka.
“Ulipotoka kwenda kufuata walet au pochi nyumbani,
unasema ulikuwa na usafiri. Ukaharibika njiani. Ulirudije tena hapa?” Akamuona
ni kama anajaribu kufikiria. Kisha akakumbuka. “Ilikuwa ni tairi tu. Mike
alinifundisha kubadili tairi ili isijetokea usiku naharibikiwa peke yangu
njiani, nikakwama. Kwa hiyo najua kubadili tairi. Nilibadilisha kwa haraka nikaendelea
na safari.” “Kwa hiyo ndilo lililokuleta au kukurudisha hapa sasahivi? Kwamba
lipo hapo nje?” Akaendelea kumuhoji.
Hapo akamuona kama anajaribu kufikiria, kisha anashindwa.
Akamwangalia na kurudisha macho kwenye kompyuta. Jina la Michael Zwambo
likatokea hapo. Ni kweli alikufa kwenye hiyo hospitali. Kuangalia tarehe
ni kama ya siku hiyo. Muda aliokufa ulikuwa saa 7:30 usiku wa siku yenye
tarehe kama hiyo. Akajua hiyo ni anniversary yake, ndio imemtibua. Akamuhurumia na
kumwangalia.
“Nahisi kama nachanganya!” “Kwa nini?” “Mmmh!” Ikawa kama
hana tena uhakika. “Niambie tu unachofikiria.” Colins akamchukulia taratibu. “Sina
uhakika sana. Maana ile gari niliyobadilisha tairi, ndiyo Luca alinipokonya jana!”
Colins akakumbuka moja ya jumbe zake kwa Mike ni kuwa huyo Luca anayafanya maisha
yake kuwa magumu. Ila hakujua ni nani na anahusikaje.
Akataka kufahamu zaidi.
“Kwa nini Luca akupokonye?” Akamuona ametulia na kuinama.
“Eti Kamila?” “Kulitokea kutoelewana, ndio akasema na gari anachukua. Ni
mali inayotokana na kampuni, haikuwa ya Mike. Ndio nachanganyikiwa maana ndiyo
hiyohiyo nilikuwa nayo usiku nilipomleta hapa Mike!” Akawa amekwama na
sauti ikaisha kabisa.
Colins akaenda kumletea maji ya kunywa. Akamkabidhi
mkononi bila ya safari hii kumuuliza. Akayanywa yote. Kisha akabaki kama ambaye
amepoteza dira, na yeye Colins akawa amebakiwa na ukweli halisi
juu ya Mike, lakini hajui kama amwambie au la! Akarudisha macho
kwenye kompyuta ili asome chanzo cha kifo chake. Akaona ni kama madaktari
walihisi alikuwa na sumu mwilini.z Lakini ndugu wa familia walipoambiwa
mwili wake ufanyiwe vipimo zaidi ili kujua kilichomuua, ilionyesha ndugu walikataa,
na kuondoka na mwili wa Mike. Kwahiyo haikujulikana chanzo cha kifo chake kwa
hakika. Lakini Mike alikufa akiwa bado hajapokea matibabu yeyote.
Colins akaumia sana. Akamuangalia Kamila. Akakuta
amelala na chupa ya maji mkononi. Akashangaa! Maana alilala hapohapo mbele ya
meza yake! Kama aliyekuwa amechoka haswa. Ila akagundua ni tarehe
tu ndio amechanganya ila alikuwa sahihi.
“Itakuwa
alipoondoka kufuata pesa, huku nyuma Mike alifariki dunia. Hakumkuta tena, ndio
maana akili bado inamrudisha hapa!” Akawaza Colins akimtizama asijue
anafanya nini na huyo Kamila hapo ofisini kwake.
Nini dawa ya mapenzi!
Gafla kitu kikapita kichwani na kumtia hofu. “Isijekuwa
amepoteza fahamu mimi nadhania amelala!” Akapiga simu akitaka aitiwe muuguzi
na afike hapo na vifaa vya kupimia pressure.
Baada ya muda mfupi akafika hapo. “Mguse taratibu,
mwangalie mapigo ya moyo, oxygen mwilini na BP yake.” Akamgusa
taratibu, akaamka. “Nataka kukupima. Nitakuvuta mkono.” Akakubali. Baada ya
vipimo kidogo tu akaambiwa pressure ipo juu sana.
“Bora umemuwahi. Angeweza pata shindikizo la damu.”
Akamwambia Colins akishangazwa na hiyo pressure ya Kamila. Wakaita mtu
mwingine na kitanda cha wagonjwa, akatolewa hapo kwa haraka na kupelekwa wodini
kuanza matibabu. “Tafadhali mnijulishe itakavyokwenda.” Colins akabaki ofisini
hakutaka kufuata nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye mida ya saa 11 jioni ndio akapigiwa simu kuwa wameweza
kushusha hiyo pressure, na wamempumzisha. Ndio akili ikatulia. Akasubiria mpaka
wafanyakazi wote wa pale juu alipo waondoke, ndipo akaenda kwenye chumba
alichoambiwa amelazwa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamkuta amelala kama mtoto. Na ni kama walimsafisha
kidogo na tayari alishavalishwa mavazi ya wagonjwa. Colins akapotelea mawazoni
akimtizama huku anawaza jinsi maisha yalivyo. Ni kama Kamila alikuwa na kila
kitu maishani, gafla amebakiwa mpweke! Tena yeye si kwa kupenda kwake
au kukosea kama yeye! Bali maisha yakamuweka kundi moja na yeye. Wapweke
waliozungukwa na watu. Wakisaka kitu ambacho hakuna uwezekano wa
kuja kupata tena katika ulimwengu huu. Mapenzi ya walio wahi kuwapenda.
Jelini na Mike.
Akajikuta anaelewa pale anakopitia Kamila na
kumuhurumia sana. Yeye mapenzi yalimfanya kichaa na mgonjwa. Na Kamila naye kila
siku ya kumbukumbu ya kifo cha mpenzi wake, huharibika akili,
akipoteza kumbukumbu pamoja na hiyo pressure. Akavuta pumzi kwa nguvu na
kuzishusha. “Mbona huku kupenda kunakuwa ni adhabu tena!” Akawaza
Colins. “Nini dawa ya mapenzi!” Akaendelea kuwaza bila jibu asijue muda
unazidi kwenda.
Kilichomshangaza, muda wote huo, hakuna hata mtu mmoja aliyemtafuta
huyo Kamila japo simu yake ilikuwa hewani. Akaangalia muda. Ilishakuwa saa nne
usiku. “Yaani mpaka muda huu hakuna mtu hata mmoja mwenye kutaka kujua alipo,
tokea asubuhi alipofika hapa!?” Akashangazwa sana. Akajikuta ni kama
amekwama pale mpaka nesi alipoingia pale. Akamtoa mawazoni.
“Bosi wangu bado upo?!” Akamrushia neno. “Natoka
sasahivi. Nimepatwa na wasiwasi naye. Angeweza kunifia pale ofisini!” “Kila mtu
anasema ni bora ulipomuwahi. Ila sasahivi anaonekana kuendelea vizuri. Usiwe na
wasiwasi.” “Nawashukuru sana.” Ndio akawa kama amemfukuza kurudi
nyumbani. Ila bado alijisikia anawajibika kubaki.
Mwana Kulitafuta!
Alirudi nyumbani akiwa na mawazo kibao. Wasiwasi juu ya
Kamila na kukumbushwa mapenzi. Hapo ndipo akili yake ikagomea hapo. Usiku
huo akazidi kujisikia mpweke na kushindwa kulala kwa haraka. Mawazo
yakamrudisha kwa Love, ndipo akamkumbuka Chris.
Akaanza kazi ya kupekua simu ya Chris akimchunguza kama
ana siri yeyote anayoweza itumia kumpunguza makali. Alikuwa
kwenye kompyuta yake. Akaangalia huo mwezi. Akapita pote, hakuona cha siri
sana. Akaendelea kusaka mpaka miezi 6 nyuma, ndipo akakutana na jumbe za
mapenzi alizokuwa amefuta! Ila kwa utundu wake akapekenyua mpaka akapata
na jumbe alizokuwa amefuta.
Akaanza kuzisoma na kugundua hazikuwa zikitoka kwa
mkewe. Akaanza kumtafuta mtumaji. Alikuwa mwanafunzi wa shule ya
sekondari Jangwani, lakini anaishi hosteli na wenzie maeneo ya Mwananyamala.
Akaendelea kusoma.
Ikaonekana ni kama alimuacha huyo binti akiwa mgonjwa.
Baadhi ya jumbe ni huyo binti alikuwa akimlalamikia kutomjali. Sasa moja
iliyomfurahisha Colins ni ile aliyomwambia, anamuacha akiwa mgonjwa, wakati ni
yeye mwenyewe ndiye aliyemlazimisha kutoa mimba! Tena kwa ahadi ya
kuendeleza mapenzi yao baada ya hapo! Colins akajikuta akicheka peke yake mpaka
kupiga makofi kabisa.
Katika hizo jumbe za mwisho, hakuonekana kumjibu
huyo mrembo. Mwishoe akaona alimfungia simu zake. Alivyo shabiki,
akahamia kwenye simu ya huyo mrembo alikuwa akiitwa Zulfa. Akaona alihangaika
kumsaka Chris kwa jumbe na simu kwa muda wakutosha tu, mwishoe ni kama alikata
tamaa, akaona jumbe zimekoma.
Kwa hiyo furaha tu, Colins akapatwa usingizi mzito na
mzuri akijiambia, “Nimekukamata Chris. Na huu ni mwanzo tu. Utajuta
kuingilia mambo yangu.” Usiku huo akawa la Chris ameshalipatia ufumbuzi,
akalala.
~~~~~~~~~~~~~~~
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment