Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 11. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 11.

Asubuhi hiyo ya jumamosi aliamka mapema kuwahi kurudi hospitalini kumuona Kamila. Alimkuta amelala hana habari. Akaona aondoke tu, asije zua maswali kwa wafanyakazi wa hapo, tena akiwa ameshajipatia jina kubwa, mwanzoni mwanzoni.

Alipofika tu ofisini kazi zikaanza hata kabla ya saa mbili, akawa busy akihangaikia mambo ya hospitalini hapo, nyuma ya pazia. Akatingwa na kuzama kazini mpaka kwenye majira ya saa 4:30, mmoja wa viongozi wa manesi akaomba kumuona Colins. Akaruhusu aingie.

“Samahani bosi.” Colins akamtizama. “Sijui unamkumbuka yule binti aliyetolewa hapa ofisini kwako jana?” Alikuwa mama mtu mzima kidogo. “Kuna nini?” “Mimi namfahamu yule binti. Anamatatizo ya akili. Hajaanza leo wala jana. Alishakuja hapa muda kidogo kwa madai kama amempoteza mwanaume wake hapa, anafanyia fujo manesi, akitaka wamwambie alipo. Na akianza fujo, hamalizi mpaka askari wamtoe.”

“Sasa nimeingia asubuhi hii, nimekuta ripoti kuwa, jana alipewa kitanda, tena kwenye chumba cha peke yake!” Colins akabaki akimtizama, huku akimsikiliza na kutaka kujua tatizo. Ule mtizamo akaona aongeze nguvu. “Hata hivyo tumepita raundi na madaktari, anaonekana pressure imerudi kuwa ya kawaida. Daktari amemruhusu aondoke ila aongeze mapumziko, hataki. Sasa kila anavyoeleweshwa kuwa hapa ni hospitali, tunawapatia wagonjwa wenye uhitaji huduma, atoke ili apishe mtu pale, analia kwelikweli! Hataki kuondoka. Ndio nikasema kabla hajatolewa tena kwa nguvu kama jana, maana nimeambiwa wewe ndiye uliyeidhinisha apewe kitanda tena baada ya kumrudisha alipotolewa getini. Ndio nikaona kwa heshima yako, nije nikwambie hali ilivyo.”

“Mmeshapata mgonjwa mwenye uhitaji na hicho kitanda?” Akamuuliza vizuri tu. “Kwa sasa hapana. Lakini si unajua wakati wowote tunaweza pata mgonjwa mwenye uwezo, akataka chumba cha peke yake?” “Maadamu sasahivi hakuna anayekihitaji, mwacheni alale hapo. Na naomba apewe chakula kama wagonjwa wengine, na iwe ni lazima kuingia chumbani kwake, vinginevyo aachwe apumzike. Wewe si unatoka saa 8 mchana?” “Ndiyo.” Akajibu kwa kutoridhika.

“Basi kabla ya kuondoka, hakikisha anapimwa tena pressure. Na akishapewa chakula, mwacheni kabisa apumzike.” “Unajua hata daktari ameshauri pengine apelekwe kwenye hospitali inayotoa huduma ya wenye matatizo ya akili. Pengine huko watamsaidia zaidi kuliko kumuacha tu hapa.” “Na kwa sababu sasahivi ameshapimwa, hamna sababu ya mtu kumghasi tena. Mpeni mataulo, abadilishiwe na mashuka, aachwe. Kazi njema.” Ikabidi tu atoke maana Colins alishageuka na kuendelea na kazi ila akamkumbusha mbali.

Hapo alipo Kamila, alishapita na yeye, ila yeye akiwa na hali mbaya zaidi ya Kamila, bila msaada wowote au akizungukwa na watu kama huyo mama. Ambao hawakuona umuhimu wakumsaidia. Ikawa kama amemkumbusha machungu.

Twins Couple

Huku Junior, mzee wa mipango ambaye kama ndiye anayeendesha mahusiano ya watu wa nne, jumamosi hiyo akaonelea wakutane tena, wao tu wanne, tena nyumbani kwa Ezra, kuwakumbusha na kuweka msisitizo kwa wanawake zao juu ya umoja wao.

Kama kawaida ya Jelini, hana dogo. Walitaka wakutane na wawe pamoja kwa siku nzima, yeye akasema lazima wakajisafi kwanza saluni. Akampitia Emelda mida ya saa tatu asubuhi, akiwa yeye ameshaweka sawa nyumba ya mchungaji, akatoka na Jelini kwa furaha zote akitarajia kupendeza.

Warembo hao wakatengenezwa wakitaka kuvutia kwa wanaume zao, lakini Jelini alihakikisha Emelda anatengenezwa vizuri mpaka kucha za mikono akijua kidole kitapata pete kesho yake. Akamtafutia na vazi la kesho yake, Emelda anachekelea tu akijua ni Jelini mpenda vizuri, kumbe anamuandaa kwa siku muhimu waliyoiandaa watatu hao, yeye hajui. Hata mama yake alijua atachumbiwa kanisani na kutakuwa na tafrija.

Basi mpaka wanafika kwa Ezra, Jelini ameridhika na maandalizi ya Emelda kwa siku yake maalumu. Waliwakuta wote wawili nyumbani kwa Ezra. Ukweli warembo hao walipendeza mpaka kina Ezra wakafurahia. Emelda huyu alishaanza kuendana nao. Kazi ya Jelini hiyo. Kumtoa chini mpaka kufikia hadhi ya Junior. Mavazi, muonekano, na kumfanya ajifikirie kama mwanamke wa Junior, sio kujibana, akiona hastahili vitu vizuri.

Siku hiyo Jelini hakuwa na kazi popote, ndio yupo kwenye kupona. Alipofika tu, mikononi kwa Ezra. “Sio tule kwanza?” “Basi kama hujui mwenzio ninahamu na Ezra.” Mpaka Ezra mwenyewe akacheka. “Njaa inauma Jelini! Si tule kwanza ndio urudi hapo mikononi!” Akapandisha mabega kukataa na kujiweka vizuri kabisa hapo kochini mikononi kwa mwenzie. Junior akabaki akimwangalia. “Kidogo tu, Junior na wewe! Huwezi kufa.” Ikabidi wachukue vinywaji warudi kukaa hapo sebuleni walipo Ezra na Jelini.

Akamuwekea Jelini kinywaji mbele yake. Akakichungulia na kuanza kucheka. “Ujue wewe Junior unanipenda sana!” Wote wakacheka. “Nakufikiria lakini wewe hutaki kunifikiria.” “Haya twende tukale. Wewe wangu Junior. Sema nina hamu na Ezra.” “Siku nzima leo ni yetu! Tule, kisha turudi hapo kwenye makochi mpaka usiku.” Wakahamia mezani, stori zikaanza.

Kula kunywa wakiwa wamewaandalia wapenzi wao vilivyo na kujitahidi kuwaonyesha uzuri wa maisha yao ya mbeleni. Furaha tele hapo, kisha wakarudi sebuleni baada ya mlo na kusafisha jiko. Unaweza sema upo kwa Junior! Hamna tofauti hata ya kijiko.

“Chakula kilikuwa kizuri sana. Asanteni.” Warembo hao wakashukuru kuandaliwa mlo na wapenzi wao. Wakatulia kochini, kila mmoja na mpenzi wao, wakiongea yao, kama kuweka msingi wa maisha yao hao wanne.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati ya wanne hao yakienda sawa baada ya vijana hao wa kanisani wakiwa walishaombea hizo siku hata kabla hawajaziishi, tena kwa kufunga, wakimsihi Mungu kuja pata wanawake kama hao, watakao dumisha umoja wao na kuwaunga mkono kwenye maisha yao, huku wakitoa faraja vilivyo, huku kwa Colins yeye aliendelea na upweke. Kazi ikawa ndio sehemu pekee inayoweza kumficha asijifikirie zaidi. Ndio ameongezeka mrembo Kamila aliyejawa Mike.

~~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo wengi ikiwa ni nusu siku ya kazi, kwake ilikuwa kama siku ya jumatatu tu. Kushinda hapo kuanzia asubuhi mpaka usiku tena usiku mwingi tu. Akabaki hapo kimya akiendelea na kazi. Hata chakula hakula. Kuanzia anaingia mpaka jioni wafanyakazi wengine wakaanza kumuaga na kuondoka. Akajikuta amebaki peke yake. Hakumsikia mzee Simba wala familia yake. Akajua wanajipanga ili warudi na nguvu kubwa. Akacheka na kutulia.

Yanayo msibu Mrembo Kamila.

Akiwa amepotelea mawazoni, yupo peke yake hapo kwenye upande wa utawala, akashituliwa na hodi ya heshima mlangoni kwake. Akanyanyua kichwa kuangalia kupitia mlango wa kioo. Alikuwa mlinzi. Akamuonyeshea ishara aingie “Chifu. Kuna mtu anataka kukuona.” Colins akakunja uso. Akaangalia saa ya ukutani. Kabla hajajibu, akamwangalia tena mlinzi ili kumuuliza ni nani mida hiyo, lakini macho yake yakatua asipotegemea. Moyo ukapatwa hali asiyoelewa kumuona Kamila pale.

Akabaki ameduaa. “Nimuache? Maana amesisitiza lazima kukuona leo.” “Hamna shida. Karibu.” Akasogea karibu ya mlango kama anayesita kuingia. “Samahani kwa usumbufu. Wameniambia bado upo na majukumu mengi.” Aliongea kama mwenye akili tu timamu.

“Karibu. Ingia ukae.” Akasogea mpaka pale karibu ya meza, akakaa kama jana yake tu. “Karibu.” “Nimeambiwa wewe ndiye uliyeniruhusu kuwepo hapa, bila hivyo wangeshanifukuza. Asante.” “Karibu. Unajisikiaje?” “Najisikia vizuri kabisa. Nilihitaji muda kama huu wa kulala, na kutulia bila kelele wala fujo. Sijapata utulivu kama huu kwa muda mrefu. Nakushukuru.” “Karibu.” Colins akawa hajui azungumze naye nini. Akatulia kumsikiliza.

Lakini na yeye akawa ametulia. Akajua ataaga. Akafikiria kwa haraka. Akamuwahi. “Walishakupitishia chakula?” “Ndiyo. Nashukuru. Ila naona sasa niondoke tu.” “Usiku huu?!” Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha kama ambaye hana uhakika na maamuzi yake.

Kisha akamuona kama anayeongea mawazoni. “Lazima nianzie mahali. Iwe mchana au usiku, ni lazima nianze tu. Siwezi kuendelea kuishi hivi. Nimepata muda wa kulala vizuri, nimeona sifanyi vizuri ndio maana watu wananidharau wananiona nikichaa. Ila mimi si kicha…” Akasita.

“Nakiri kuna muda nakuwa sijielewi, lakini si kichaa.” Akaongea kwa utulivu kama anayefikiria akijitetea. “Ni kama Mike ndiye aliyekuwa akinisaidia kufikiria na kupanga kila kitu. Ameondoka gafla, nikapoteza dira. Sijui natakiwa kuanzia wapi! Na najua ikitokea anarudi muda wowote ule, hatafurahia maisha ninayoishi. Nitamuumiza sana mpenzi wangu. Si sawa.”

“Kwani unaishije?” Colins akaona amuulize tu. “Mimi mwenyewe hata sijui! Naipokea kila siku vile ilivyo. Mike yeye ndio mzuri wa mipango. Alipanga niache kazi, nitulie tu nyumbani tutafute mtoto. Maana stress za kazini zilikuwa zinanifanya nakuwa na pressure ya juu, mimba zinatoka. Ndio akasema niache, nitulie tu nyumbani. Yeye akawa ananitunza. Mike anaakili sana. Halafu anaupendo. Yeye si mnyanyasaji kama ndugu zake.” Akaendelea.

“Kwa hiyo mimi nikawa nakaa tu nyumbani, kila kitu anafanya Mike, halafu ananipenda sana. Sasa na yeye ameondoka gafla! Hajaniaga! Hajaniachia maelekezo yeyote! Nimejikuta nimekwama. Ndio ndugu zake wananiambia mimi si mke wa Mike, wala sijazaa naye, pale aliponiacha Mike ni nyumba ya familia, niondoke. Lakini mimi nilishashika mimba mara mbili! Zikatoka. Nikiwaambia, wananiambia mimi ni muongo. Ila Mike ni shahidi yangu. Mimi sidanganyi.” Colins akabaki kimya. Maana alianza kuongea kama aliyekuwa akitafuta jukwaa.

“Ndio wakaniambia nitoke pale. Kwanza wanasema eti maisha aliyonizoesha Mike ni ya garama sana, siwezi kuishi kwenye lile jumba peke yangu, eti ni kukufuru. Ndio wakaanza kuhamia hapo mmoja baada ya mwingine huku wananifanyia fujo niondoke. Mimi nikawaambia mimi ni yatima, na Mike alikuwa anajua ndio maana alikuwa akinitunza, wanasema Mike wakunitunza hayupo, niondoke.”

“Ni wakorofi hao! Wakorofi sana. Kwanza ujue wala si ndugu wa kuzaliwa wa Mike. Na yeye Mike alilelewa na baba yao tokea yupo mdogo. Baba yao alikuwa mjomba wake Mike. Watoto wake wakakataa shule, ila Mike yeye akakazana kusoma zaidi yao, ndio mjomba akawa anampenda sana Mike. Hata mimi alikuwa akinipenda. Sema watoto wake wana wivu halafu wakorofi.”

“Wakajaa hapo kwenye nyumba, wakagawana vyumba vyote, wakaniachia chumbani kwangu. Tena si kwa hiari! Nilikuwa najifungia ndani ili wasinitoe mpaka nilipougua.” Akawa kama amemaliza, au anafikiria. Colins akashindwa kumuelewa, mbaya na yeye akataka kusikia zaidi.

“Nini kilitokea ulipougua?” Akamwangalia kama hakumbuki au hajaelewa swali. “Ulisema mpaka ulipougua. Ni nini kilitokea?” Akakumbuka. “Nilipokwenda hospitali, niliporudi nikakuta wamenivunjia chumba changu, wamekichukua. Wananiambia pale sio kwangu, niondoke. Ila nimekataa kuondoka. Nahofia Mike asije rudi, akanikosa! Maana aliniambia pale ni kwangu na watoto wetu.”

“Sasa kama wamechukua chumba. Na wamejaa humo ndani, wewe unalala wapi?” “Kwenye makochi. Ila wakizidisha kelele. Wanaangalia tv kwa muda mrefu, naenda kulala kwenye gari.” Colins akamuhurumia huku akishangaa. “Tena walivyo na tabia mbaya, wamenichukulia vitu vyangu vyote, wanasema mali ya kaka yao. Na Luca naye anasema kama nataka kuendelea kuishi pale, basi nikubali anioe tuendeleze ukoo! Haogopi hata kidogo, wakati mimi ni shemeji yake jamani!”

“Nimemwambia si sawa kwa Mike na kwanza haikubaliki kwenye jamii. Mimi ni shemeji yake. Mike akija rudi ataniona mimi ni msaliti. Kwanza siwezi kuishi naye. Sina hisia naye. Mimi nampenda ndugu yao. Ndio akakasirika akanipokonya funguo za gari.” Akatulia kabisa. Colins naye kimya akimwangalia huku akizidi kushangazwa na kinachoendelea kwenye maisha ya mrembo huyo.

Kwa kumuona alionekana mzima. Akianza kuzungumza ndio utajua kuna kitu hakipo sawa. Bado hajakubaliana na kifo cha Mike.

“Mike ananipenda sana. Halafu ananijali. Kabla sijalia shida, anakuwa ameshanitimizia. Ndio hapo ninapochanganyikiwa! Mike si mtu wa kuondoka na kuniacha kwenye hii hali! Mpaka mimi naingia dhambini jamani!” “Kwa nini?” Akaguna.

“Unajua mjomba alipomtambua Mike kama kiongozi wa mali zake, wale watoto wake walikasirika sana. Kukaanza visa visivyoisha. Mimi mpaka nahisi wamemteka nyara, Mike wangu. Wamemfungia mahali, halafu wanadanganya watu amekufa. Mike si wakuondoka dunia hii bila mimi. Namjua Mike. Popote anapokwenda, hawezi niacha hata kama ni kwa usiku mmoja tu. Kuna kitu hakipo sawa.”

Akafikiria. “Nimemtafuta kila mahali, ila kumbukumbu zinaishia mara ya mwisho nilimuacha hapa! Sasa sijui walimlipa yule nesi aseme hajawahi kumuona ili waendelee kumficha wale mali za baba yao!”

“Kwani mjomba wake yuko wapi?” “Mjomba alifariki. Alipojua hatapona ndio alimtangaza Mike kuwa ataendeleza mali zote. Alisema kwa kuwa Mike anaupendo na kujali sana watu, anajua atatunza watoto wake. Hawakupenda kabisa.” “Na mama yao?” “Alifariki zamani sana. Mjomba hakuo tena.” Akatulia hapo kitini kama amefika. Analoliwaza ndilo analiongea mdomoni. Colins kimya akimsikiliza huku akisema, “Kweli hujafa hujaumbika.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Kamila aliyekuwa mtandaoni na huyo, walifanana kiasi kwa muonekano ila pia wakawa kama watu wawili tofauti! Yule wa mtandaoni alikuwa mrembo na nadhifu sana. Huyu alikuwa na uzuri wake ila hana nywele zakueleweka. Kama aliyekuwa ametia dawa! Juu laini, chini kipilipili ambacho hakijachanwa. Si ndefu wala fupi sana.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akamtizama, akakuta na yeye anawaza yake. Kisha akawa kama amegutuka. “Acha nikuache ufanye kazi. Usiku mwema.” “Unakwenda wapi?” “Narudi palepale. Kisha nitatafuta kazi ili nianze kujikimu.” “Unajua sasahivi inakwenda saa tano usiku? Utafikaje huko?” Akawa tena kama amekwama. Akatulia. Kisha akamwangalia. “Unafikiri sasahivi siwezi pata daladala za Salasala?” “Sidhani.” Akatulia kama aliyefika mwisho.

“Nashauri ulale hapa mpaka kesho.” “Wale manesi wakorofi. Sipendi wanavyonisema mimi nikichaa. Wanataka niende hospitali za vichaa, sio hapa. Kwanza hawawezi niruhusu nirudi pale. Wameniambia nichukue vitu vyangu vyote.” “Acha nipige simu kujua kama chumba kilishapata mtu.” “Haitakuwa usumbufu kwako?” “Hata kidogo.” Akashangaa anasimama.

“Unakwenda wapi?” “Umesema unapiga simu. Nakupisha. Au sikuwa nimeelewa?” “Hamna shida. Wewe subiria tu hapo.” Akarudi kukaa.

Colins akapiga simu moja tu. Alipoambiwa kile chumba bado hakijapata mtu, akamwambia huyo wa kwenye simu, aandikishe jina la Kamila. Akampa simu Kamila mwenyewe atoe taarifa zake kamili. Akatoa jina kamili na mwaka wake kuzaliwa. Kwa kifupi kile chumba kikaonekana kina mtu, ili asisumbuliwe tena.

“Kwa sasa hicho chumba ni chako. Hakuna atakaye kusumbua mpaka utakapokuwa tayari kuondoka.” “Hiyo kesho?” Akauliza kwa wasiwasi kama anayeomba kukaa zaidi. “Utakapokuwa tayari kuondoka.” Akajirudia akimtizama.

“Mimi najua sana kupika na napenda. Mike alinipeleka shuleni kabisa ili kukuza kipaji changu. Nikawa napika kwenye mahoteli makubwa, wananisifia.” Colins akabaki akimwangalia, hajaelewa inahusiana vipi na malazi yake! Akiwa bado hajamuelewa, akaongeza. “Hata Mike anapenda sana chakula changu.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Kuna mapito yakuumiza tunapita duniani, hayana majibu na pengine unaona kabisa hustahili. Ila wakati mwingine hufanyika msaada kwa wengine wanapopitia hapo.

Katikati ya vita kali na upweke wa mapenzi, akiwa amejawa hasira, akilipiza kisasi kwa kila aliyemuumiza, Kamila aliyejawa mpenzi Mike, naye anapita kwenye maisha yake akiwa bado hajamuelewa ila kuona anawajibika kumsaidia.

Mwisho wake ni nini?

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment