Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 6. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 6.

 “Tunaanzia kazini kwako.” Akawa hajawaelewa. “Kwamba leo nyinyi ndio

mnataka kunipeleka kazini!? Sina shida. Kwanza siwafahamu” “Sasa ni aidha utoke kwa ridhaa yako au tukutoe hapa kwa nguvu. Uchaguzi ni wako.” Wakambadilikia. “Na mimi bila ya kuniambia nyinyi ni kina nani, sitoki hapa. Mkiniteka je!?” Wakamvuta kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari yao na kuondoka naye akipiga kelele ili msichana wa kazi angalau ajue, atoe taarifa hata kwa wazazi. Love alishaingiwa hofu ya ajabu.

Hawakuwa wamemdanganya, ni kweli walimpeleka moja kwa moja mpaka ofisini kwao. Wakamuamuru ashuke. Safari hii hakufanya ubishi. Kwanza hakutaka tena kuvutwa na kuingia aibu pale ofisini ambako alikuwa akijulikana. Akaongoza njia wakimfuta kwa karibu.

Wakafika mpaka mapokezi, akataka kupitiliza kama mwenyeji tu, wakamzuia kitu kilichomshangaza. Wakamuamuru asubirie pale kama mgeni, mmoja akamwambia muhudumu waliyemkuta pale kuwa awataarifu kuwa wamemkamata Love. Akashangaa sana. “Mmenikamata vipi na mmenikuta kwetu!?” “Si ndiko ulikokuwa umejificha ukidhani hatutaangalia huko?” Akawa kama hajawaelewa.

Akiwa amekaa hapo anajaribu kuelewa, akagundua kuna kikao kinacho endelea chumba cha mkutano. Akazidi kushangazwa. Kwa sababu yeye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu hapo, lazima kila kikao hapo kumuhusu kwa silimia 85 kama si zote. Maana aliongoza kitengo cha fedha.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa hakika alikiwezea hicho kitengo. So smart. Kwenye kuweka budget ya kampuni. Matumizi yote yalikuwa lazima na yeye aidhinishe. Kwamba ni mmoja wa waweka saini hapo kwenye hiyo kampuni. Mwadilifu anayesimamia sheria za kampuni bila kuyumba. Na wote walimfahamu na wengine kumchukia kwa maadili hayo. Hapindishi malipo hata kwa punje ili waje wagawane baadaye. Aliweza dhibiti matumizi mabaya ya fedha, na kuwafungia au kuwazibia aliowakuta hapo ulaji waliokuwa wamezoea kwa kudanganya matumizi yasiyo kweli. Wakawa wakifuja pesa ya hiyo kampuni mpaka alipokuja yeye.

Na kwa kuwa alikuwa akijiamini kupitiliza na kulewa madaraka hayo makubwa akiwa bado msichana tu, ikamjengea kiburi. Hana ukaribu na watu. Alijiweka kwenye ngazi ya juu. Hata kuingia ofisini kwake ilikuwa ni mpaka akuite. Akajiweka kwenye hali watu wakimuona kama anatabia za uzungu, kumbe ni haiba yake tu ya dharau.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa bado anajaribu kuingiza zile taarifa kichwani, akasikia wameruhusiwa waingie. “Simama twende.” Akaamriwa. Akashangaa wafanyakazi wengine wanatoka kwenye ofisi zao kuja kumshangaa yeye. Akadhania pengine ni ile video ya jana imeenea! Asijue makubwa yanamsuburia.

Wakamuongoza moja kwa moja mpaka chumba cha mkutano. Akakuta wahasibu wote mpaka kiongozi wao kwenye hiyo ofisi wapo humo ndani kana kwamba wanajadiliana jambo zito! Kilichomshangaza zaidi ni kukuta bank statement imerushwa kwenye screen, kubwa ya ukutani ikijadiliwa. Yeye mkuu wa kitengo cha fedha hajahusishwa!

“Ni nini kinaendelea?” Wote wakabaki wakimtizama “Najua leo nimechelewa. Lakini sio sababu ya kuendesha kikao cha mambo ya fedha bila mimi! Kulikuwa na uharaka gani wakukifanya na kushindwa kunisubiria mpaka mnitumie watu?!” “Ulitaka kuendelea kutufumba macho kwa maneno mengi ya uzungu mwingi, ukituchanganya kwa mahesabu yasiyo kweli, ukiweka budget zinazosikika za kweli, huku ukikata matumizi ya kila kitengo, na kukataa kuidhinisha malipo muhimu yanayoendesha hii kampuni ili kuendelea kufuja pesa ya kampuni wewe mwenyewe!?” Kiongozi wao kwenye hiyo ofisi akamuuliza. Love akashangaa sana.

“Unazungumzia nini wewe!?” Akamuuliza kwa dharau kwa kutomtambua kwa wadhifa wake au angalau hata jina huyo kiongozi wake. Kwanza hakuwa amesoma kama yeye Love. Ni mtumzima aliyefanya kazi kwa muda mrefu sana hapo kwenye hiyo kampuni. Akawa muadilifu na akajua mambo mengi, mpaka akapandishwa cheo. Sasa Love alipoingia hapo na kujikuta yeye ndiye amesoma zaidi ya wote hapo japo wana uzoefu, kiburi kikapanda. Hakuwa akimuheshimu ila kujitahidi kwa kuwa alikuwa akiripoti kwa wakuu. Wote walijua hamuheshimu ila tu, kujitahidi asije mripoti vibaya kwa wakuu wake.

“Mbona mnanitolea macho tu!? Mnapoteza muda wangu. Ongeeni jambo linaloeleweka.” Love akafoka. “Nashauri aonyeshwe, tumtoe hapa, tusiendelee kupoteza muda zaidi.” Mmoja kati ya aliyekuja naye, kutoka kwao akashauri.

“Mnataka kunipotezea muda wangu, hamna kitu cha kuniambia.” Akataka kutoka. Mmoja akawahi mlangoni. Rudi kabla hatuja…” “Mtanifanya nini!? Utanifanya nini!? Akawa mkali.

“Huyo ni jeuri wakupitiliza. Na hapo ameshatuangalia chumba kizima, ametuona tumesomea chini ya miembe, hamna mtakalomwambia akasikiliza.” Mhasibu mmoja akaongea kwa kumchukia Love. “Kwanza anasema tukimzingua, anarudi kwa wasomi wenzie huko walikomfundisha kazi. Hapa amekuja kupumzika tu. Kama kusalimia ndugu.” Mwenzie akaongeza kama anayesemelea. “Sina muda wa majungu mimi. Kama hamna kazi, mimi nina majukumu mengine.” Akataka kutoka tena. Mmoja wale wawili, ambaye ni askari kanzu, akaenda kumvuta na mwenzie akavuta kiti. Wakamkalisha kwa nguvu, asiamini.

Akataka kusimama, wakamkalisha tena kwa nguvu. “Msinifanye mimi mjinga. Najua haki zangu na ninaye mwanasheria wangu. Mkikiuka haki zangu, kwa hakika nitawashitaki bila ya kufikiria mara mbili. Acheni kunichezea.” “Na sisi tuna majukumu yetu kama wewe. Tupo hapa kikazi tukiwa tumetumwa kutoka makao yenu makuu. Tunashauri utulie, usikilize kabla hatujakutoa hapa na kukupeleka kituoni, kukabiliana na mashitaka yako. Uchunguzi mwingine uendelee akiwa chini ya vyombo vya sheria.” Love akashituka sana.

 “Kama ni kesi ya jana, hata sisi tumeshitaki. Maana…” “Ndio baada ya lile tukio ukaamua kuchota mapesa ya kampuni ili mtoroke na mwenzio hapa nchini?” Love akashangaa sana.

“Taarifa zenu zote tunazo. Pesa mlizokuwa mkiibia kampuni kwa siri mkiishi maisha ya anasa hapa mjini, huku mkijenga majumba ya kifahari kwa kutumia jasho letu! Mnafanya maparty kwenye majumba yenu, mkialika watu kuwasaidia kufuja pesa za kampuni, kwa jasho letu!” “Hayo ni majungu tu. Unahasira kwa sababu sijawahi kukualika kwangu hata mara moja.” “Hata uliowaalika wanajua ulitaka tu kujionyesha. Sina shida na ukaribu na wewe. Sitaki unihusishe kwenye pesa za wizi.”

Ndipo wakamuonyesha pesa zote alizokuwa akiiba tokea mwanzo akimuhamishia Kemi na yule mtumishi. Za jana yake usiku ndio mbaya kabisa, kama waliokuwa wamepanga kutoroka nchini! Kila alipotaka kujitetea, hawakutaka hata kumsikiliza zaidi ya kumshambulia, kila mmoja na shutuma yake. Gafla hicho chumba kikajaa wafanyakazi wote. Fujo ikazidi.

Kwanza walikuwa na hasira naye. Pili walikuwa wakimtafuta siku nyingi ili wamtoe hapo, awapishe waendelee kutafuna pesa. Lakini wakuu wao walimlevya sifa kwa kubadilisha matumizi ya hapo ofisini na kuziba mianya ya ufujaji wa pesa kwenye tawi la hapo jijini.

Jazba ikapanda wakazidi kumzomea. Kwamba ni mwizi mstaarabu. Wakazidi kumzomea kwa fujo, walipotaka kumpiga ndipo wale askari kanzu wakamtoa hapo kwa nguvu, kumkimbiza kituoni.

 ~~~~~~~~~~~~~~~

Huku nyuma msichana wa kazi akawa ameshawapigia simu wazazi kuwataarifu kuchukuliwa kwa Love ila na yeye hakuwa na taarifa za kutosha. Hakujua ni nani aliyemchukua wala alipopelekwa. Siku ya madaktari hao ikawa imeshaharibika. Hakuna aliyekuwa na jibu, wakabaki kudhania ametekwa nyara kwani hakuchukua hata pochi yake na waliomchukua hawakujitambulisha hata kwa msichana wa kazi. Ikawa paniki. Simu ya Love ilibaki chumbani, hapakuwa na jinsi ya kufanya ila taarifa kusambaa kwa watu wa karibu kuwa ametekwa.

Kule Kulikoungua mpini, kukabaki shoka.

Kasa akaona hapati majibu kutoka kwa Jelini. na muda nao ukawa umeshazidi kwenda, akajua kuna ambalo halijakaa sawa. Akampigia. Ikaita mpaka ikakata. Hasira zilimpanda Kasa, alikaribia kurusha simu. Asijue yeye Raza ndio ana hali mbaya kupita kiasi. Alitoka pale, akijua ameharibu. Akatengeneza uongo wa kila namna ukawa unagoma. Akabaki hajui chakufanya, au uongo upi ndio amwambie Kasa.

Sasa wakati Kasa anampigia, ndio anamgutusha kutoka mawazoni. Alikuwa amebaki ndani ya gari, wala hakufanikiwa kutoka viwanja vya hospitalini. Muda wote alibakia hapo hajui chakufanya, au nani ampigie amuombe ushauri. Ila hofu akijua pesa alizozoea kupokea kutoka kwa Kasa bila shida ndio zimefika mwisho. Ila hakujua Kata atafanya nini na mihela aliyokwisha wekeza kwenye hiyo salunu yake mpya ya kisasa. Maana ni kweli Kasa alimbadilishia maisha. Atamdai au la!

Iwe mwanzo na mwisho kupuuza simu yangu.’ Huo ujumbe ulipoingia tu, Raza akampigia. “Samahani, bado nilikuwa hapa hospitalini ndio maana nikashindwa kupokea.” “Jelini anaendeleaje?” “Anaendelea vizuri, nimemkuta amelala.” Njia ya muongo ikawa fupi sana, akaanza kujichanganya. “Na amesema asante kwa maua na chokleti.” Hapo akamgutusha Kasa.

“Kwanza umesema umemkuta amelala! Amesemaje asante na amejuaje kama maua yametoka kwangu?” “Ilibidi nimsubirie aamke halafu ni kama alihisi tu kuwa maua yatakuwa yametoka kwako.” Hapo akajitetea lakini kichwa ni cha Kasa bwana! Ndicho kinamuweka mjini. Nguvu ya kufikiria. “Ni kama, au alihisi na wewe kumuhakikishia?” “Jelini mwenyewe alipaniki.” “Kuwa makini sana na unachokaribia kuzungumza juu ya Jelini. Maana mimi namfahamu sana. Na sitakuruhusu umsingizie kwa namna yeyote ile. Na Raza?” Akaweka mkwara. “Nipo.” “Uongo wa namna yeyote ile naomba kukumbusha kwa siku ya leo, hauna nafasi.” Raza akazidi kutetemeka.

“Jelini si mtu wa kupaniki. Hilo moja. Pili, unaweza kumfanya asifikirie mbali, endapo utamuonyesha tu upendo. Haitaji mambo mengi isipokuwa kujaliwa na kupendwa. Sasa basi, nataka kujua ukweli kwa kile kilichotokea ulipokwenda kumuona.” “Nahisi ni kama bado nilikuwa na usingizi. Nilipofika pale nahisi jinsi nilivyoanza naye ndio nikawa kama nimemgutusha.” “Raza?” Mzee akafoka kwa sauti ya juu. Kama anayemuonya usinipotezee muda na usinidanganye zaidi.

Na yeye Raza akachukia. Rohoni akajiambia usinibabaishe, akamjia juu mwenye nacho. “Mimi sikupenda ulivyonituma kwake, tena ukinitangazia yeye ni bora kuliko mimi. Ni..” Simu ikakatwa hapohapo, Raza asiamini. Alipojaribu kumpigia, hakumpata. Akajaribu tena na tena hakumpata tena. Ilikuwa ndani ya dakika tano, lakini tayari Kasa alishafungia simu yake.

~~~~~~~~~~~~~~~

Bila ya kufikiria, akatoka hapo ofisini kuelekea hospitalini alikokuwa amelazwa Jelini. Alifika pale, kumbe bado Raza hakuwa ameondoka pale kwenye viwanja vya hospitali akijaribu kumpigia tena na tena. Akamuona ameshuka garini. Anavua koti la suti, akafungua mlango wa nyuma, akaning’iniza kwenye henga. Kisha akavua tai. Raza akimwangalia, asiamini. Akaning’iniza na hiyo tai. Akamuona akijiweka sawa kabisa kama anayejiandaa kwenda kukutana na mtu maalumu.

Raza alizidi kushangazwa. Kasa mkorofi sio huyu. Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. Kisha akafunga gari yake. Akajitizama kwenye kioo cha dirisha la mlango. Akajiweka sawa kisha kuondoka. Hakuthubutu hata kutoka garini, au amuone. Alibaki akimwangalia akiwa ndani ya gari yake mpaka akapotea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mama Jema hakuamini alipomuona ameingia pale. Alibaki akimtizama, kama ambaye haamini! Mama mchungaji naye akatulia akimtizama maana ni kama alimkumbuka kwa wazi kabisa. “Nimekuja kumuona Jelini.” Akaongea kwa kujiamini, akiwa ametulia kabisa usoni. Chumba kilikuwa kimetulia haswa. Kimya. Hata aliowakuta walikuwa hawazungumzi. Kwa hiyo hata yeye alizungumza kwa sauti ya chini tu.

“Huwa najua chakufanya kwa kila mtu, linapofika swala la watoto wangu. Lakini wewe Kasa, hakika nimeshindwa!” “Nakuahidi sitakaa hapa muda mrefu, na sitakukera zaidi. Tafadhali nipe dakika chache tu nijue anavyojisikia ili wasije mruhusu, akabakiwa na maradhi ya kudumu. Ni hilo tu.” Akabaki kimya akimtizama kama hajui amjibu nini.

Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa, mwishoe Kasa akageuka na kusogelea kitandani alipokuwa amelala Jelini kama mzoga. Akabaki akimtizama. Jelini akiwa kwenye usingizi mzito, harufu iliyoingia kwenye fahamu zake ikaamsha hisia za zamani. Akiwa usingizini akaanza kujaribu kuitambua. Akili ikaanza kuitafuta ni harufu gani hiyo!

“Zenda!” Akaongea kwa sauti ya wazi ila ya chini akiwa kama ndio amejua ni harufu ya nani akiwa huko usingizini. Kisha akafungua macho na kumkuta Kasa akimtizama. Ila vile alivyolitaja jina lake, ikawa kama sabuni ndani ya moyo wa Kasa. Akamkumbusha mbali na kufurahia kufika hapo.

“Pole.” Jelini akabaki akimwangalia asiamini kama ni ndoto au kweli Kasa amemsimamia hapo. Na Kasa alijua. Akaongeza. “Unajisikiaje?” “Mbona wewe ndio unaonekana hujalala!?” Jelini akamuuliza taratibu akisikika kujali. “Nina wasiwasi na wewe? Vipi?” Jelini akavuta pumzi kwa nguvu, akazishusha kama anayejisikilizia. “Najisikia vizuri. Usingizi tu.” “Pole.” “Acha kufanya hivyo bwana! Wewe si Kemi. Na wala Kemi si mtoto mdogo kwamba unawajibika kwa makosa yake.” “Siwezi kuacha kujilaumu.” “Nilikwambia, hata kama isingekuwa mimi, angemfanyia mtu mwingine.” “Lakini amekufanyia wewe, Jelini.” Jelini akatulia kidogo kama anayefikiria.

Kisha akaongeza. “Sijakukasirikia Kasa na sikulaumu kabisa katika hili. Tafadhali acha kujipa adhabu sababu yake.” “Siwezi.” Jelini akabaki akimwangalia kisha akaongeza tena. “Asante kwa matibabu.” “Karibu. Lakini nitazungumza nao. Watakapo kuruhusu kurudi nyumbani, ukijisikia tofauti tu, hata kama ni kidogo namna gani, usivumilie. Urudi wakuangalie tena. Sawa?” “Sawa na nashukuru.” Wakatulia kidogo.

Akawa kama amekumbuka kitu. “Na uache kunitumia wanawake zako kuja kuniona, Kasa!” “Na wewe uache kunitumia mashoga zako kuja kunitongoza.” Jelini akanyamaza. Wakatulia kwa muda, Jelini akamwangalia, akakuta akimtizama. “Nenda ukapumzike. Mimi nitakuwa sawa. Na nikijisikia vibaya, nitarudi. Ila sasahivi naomba ukawaambie nataka kuondoka, narudi nyumbani. Waniruhusu.”

“Kwa nini haraka?! Kwa nini usiache mpaka wakuruhusu wenyewe watakapo jiridhisha? Tulia upone.” “Kwa sababu wewe na wanawake zako mnataka kuniponza.” “Situmi tena mtu, si umeona nimekuja mwenyewe? Nakuacha kabisa.” “Sitaki Kasa. Wewe waambie waje wanitoe hapa. Lasivyo naondoka mwenyewe. Wewe unataka kuniponza, mchumba wangu aniache.” Kasa akaanza kucheka.

“Sio sifa, na wala havichekeshi.” “Nimemuona jana. Alikuwa amepaniki huyo!” “Ondoka Kasa. Wewe unataka kuniponza mwenzio, niachike. Mimi nataka kuolewa na Ezra. Sitaki uanze kumchanganya mpenzi wangu. Ondoka na kawaambie waje wanitoe, nirudi nyumbani kwa mama Jema, ninakojua wewe na wanawake zako hamtanifikia.” “Naona kweli umeshaanza kupona, ujeuri umerudi vilevile. Jana ulikuwa mtoto mzuri!” “Ondoka Kasa.” “Muda na wakati wowote ukitaka kitu, usisite kunipigia.” “Sitaki.” Akamfanya acheke na kuondoka akiaga. “Nawashukuru sana.” Wala hakuwatizama tena wenyeji wake, akatoka ndipo Jelini akajua kuna watu wengine pale.

Akakaa kwa haraka kama aliyefumaniwa. Akamkuta mama yake na mama mchungaji wakimwangalia wakiwa wamekaa palepale alipowaacha upande wa chini ya miguu kwenye kochi. Akataka kusema kitu. Akasita. Mwishoe akaona aongee tu.

 “Mimi naona tufungashe, tuondoke hapa, mama yangu. Nikiendelea kulala hapa, hii fujo haitaisha. Namjua Kasa. Akitoka hapa, atatuma watu waje wetengeneze hiki chumba na kubadili aina ya mashuka na mito. Hatutakaa sawa, atatuma watu wakujaza hapa maua na baluni. Kisha jioni akitoka kazini, atapitia tena hapa ndipo na Ezra naye atamkuta hapa, halafu amchanganye Ezra wangu. Twende mama.” Wakaanza kukusanya vitu vyao.

Wakati Wa Kurarua Na Wakati Wa Kushona

Huku kwa Colins alikuwa akifanya yake akifikiria kwa haraka sana. Usiku ni kama hakuwa amelala. Alikesha akifanya kazi kwenye laptop yake huku akipitia pia sheria na mikataba ya hospitali ya wazazi wake. Alisaka kwenye system akifukunyua kwenye hiyo kampuni ambayo wazazi walikuwa na share zao, na watoto nao wakawagawia sawasawa. Kwa hiyo wazazi walikuwa na share kubwa zaidi yao.

Colins akarekebisha muongozo na taratibu zote pale, akaamka siku hiyo ambayo amefanikiwa kumtia nguvuni Love akiwa na yake kichwani. Yeye hakuchelewa kuamka akitaka kuwawahi wazazi wake kabla hawajatoka hapo.

Akawakuta ndio wanajiandaa kutoka, akawasalimia. Bado walijawa sana na hofu naye, hata kumtizama vizuri ilikuwa shida. Kwanza walikuwa kama wanamkwepa. “Sitataka kuwapotezea muda. Naona nipo tayari kuanza ile kazi mliyo niamuru kufanya.” Wazazi kimya.

“Sasa ili niifanye kwa uhuru bila ya kunikwamisha, mkiwa mmenitoa kwenye ndoto zangu, mkitaka niishi ndoto zenu, nilazima mniwezeshe.” Kimya wakimsikiliza. “Kama kina Simba wanavyosimama na watoto wao kuwapa kila wanachotaka, na wakifanya juhudi kufanikisha hilo, na nyinyi mkiwasaidia, basi ni wakati wa nyinyi sasa kufanya kwa wakati wenu kukamilisha mlichoanzisha kwangu.”

“Sina muda wa kupoteza zaidi kwamba mpaka mkawaombe ruhusa kwenye mambo fulanifulani ndio tufanye mambo! Hapana. Mlinitoa kwenye maisha yangu mkitaka niwatumikie, ndio nataka nikaanze kazi bila vikwazo.” “Unataka nini?” Ikabidi mzee aulize ili asiendelee kuwatonesha vidonda. Maana na yeye hapo walimuona hasira zinazidi kupanda wakajua anapokwenda ni pabaya zaidi.

Kutopotezewa muda kwenye maamuzi yangu ya kila siku kazini, na sitataka mambo yaendelee kuendeshwa kiholelaholela pale. Kwamba mzee Simba akitaka pesa, anakutaarifu tu wewe, kisha kwenda benki na kuchota pesa. Sitafanya mchezo huo. Kwanza nataka kubadilisha kabisa ile hospitali. Na sitaweza bila pesa na dhamana.” “Dhamana umepewa Colins. Wewe ndio kiongozi wa pale.”

“Hayo ndiyo mambo ninayozungumzia. Sitaendesha mambo kiholela. Kuandika bila kalamu na kula nyama bila meno. Sijui kama unanielewa?” Mzee kimya akijaribu kuelewa. Maana Colins alikuwa akizungumza na sura ya kazi tena akiamrisha.

“Mimi nikiongozi lakini wewe na Simba ndio mna share kubwa pale. Kwamba bila ya nyinyi kuidhinisha jambo, halifanyiki. Sijui kama unanielewa mzee?” “Najaribu kuelewa.” “Basi kwa kifupi, ili kuweza kufanya ulichoniamuru kufanya kwa usahihi, nahitaji nyenzo. Na nyenzo ya kwanza ni ofisi ambayo nimeona umeihangaikia mpaka jana ilikuwa ikinisubiria. Jambo la pili, nataka mamlaka na uwezo wa kufanya mambo kwa haraka bila kucheleweshwa.”

“Kwa sababu mimi sio kama Love. Au sisi sio kama familia ya kina Simba. Wao wanakaa na kusikiliza watoto wao, kisha kuamua pamoja. Sisi ni familia ya mmoja anaamua, mwingine anafuata mkumbo, kisha familia yote tunaishia kutumbukia shimoni. Huko sirudi tena.” Alisikika ana shutuma nyingi, muda mfupi na uchungu moyoni umemlemea hawezi kufikisha shutuma zake kwa ufasaha.

“Hivyo basi, kwa kuwa nimekataa kutawaliwa au kuongozwa na Love, pamoja na wazazi wake, na nyinyi mkisaidia kuhakikisha Love pamoja na wazazi wake wanapata wanachokihitaji, kwa garama yeyote ile, sasa huo mchezo wenu sitaki TENA. Familia zote mbili hatuwezi kuongozwa na Love, ambapo mwisho kwa jinsi ninavyowajua nyinyi, mtakuja kuanza kusema na Festo, mume wa Love ameamuru hiki, lazima tufanye. Huko sitafika tena. Na kuhakikisha hilo halitokei tena, tuanze kwa kile mlichotaka niwafanyie kwa kunipa, nyenzo.” Bado wakawa hawajaelewa kabisa. Ila kumuona yeye mwenyewe kuzidi kupandwa na hasira.

“Nyenzo gani?” Ikabidi mzee ajikaze aulize. “Nyinyi mna share kubwa kuliko sisi wote. Kwa hiyo nahitaji baba na mama mnipunguzie zenu.” Ikawa si ombi ila amri. “Mimi zangu ukitaka chukua zote.” “Hutajitoa kwenye hii safari mama, maana ulitaka wewe mwenyewe na kulipia garama kubwa sana ya kunitoa kafara bila ya huruma. Umenipandisha kwenye treni, halafu wewe unataka kushuka?! Msitake kunichezea na kunichanganya. Treni imeshaondoka. Hapa inashika kasi. Utabaki humuhumu ndani mpaka tuone hiyo treni itakapofika. Msitake kunichanganya! Mmeua ndoto zangu na mipango yangu yote, halafu sasa hivi unataka kujitoa?!” Hapo akaanza kugomba kwa sauti.

“Mmenitoa kwenye ramani yangu ya maisha nikiwa nawalilia na kuwasihi  mniache, halafu..” “Basi Colins. Wewe chukua unazotaka, au unazoona zitatosha. Nia yangu ni kutaka kukusaidia.” “Acha kunidanganya mama. Hujawahi wala hujataka kunisaidia. Usiniudhi tafadhali. Na karatasi hii hapa, weka saini.” Akapokea na kuweka saini  kwa haraka bila ya kusoma.

“Na mimi nipo tayari kusaini.” Mzee hakutaka mengi. Akamkabidhi. Akaweka na yeye saini bila ya kusoma hizo karatasi zilizokuwa zimeandaliwa kwa makini sana tena akiwa na hasira na hizo familia zote mbili. Karatasi hizo zilijawa hila, wasijue makubwa na machungu yatakayo wakabili mbeleni, zaidi familia ya Simba. Ila mzee alishakinahiwa, nia na malengo yote kwa huyo kijana wao maishani vilishageuka vichungu kuliko shubiri.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Baada ya hapa baba, nataka uzungumze na yule mtoto wako kipenzi ambaye mnaelewana naye lugha. Mwambie kwa kuwa wewe unataka nikawafanyie kazi, unaniongezea na nguvu. Unanipa na nusu ya share zake.” Hapo mzee akagutuka.

“Kwa hizi share zangu, mama yako na zako, utakuwa hata juu yake. Kwa nini usimuachie na yeye akawa na..” “Unanitania au? Mbona sijaona yeye mlipomtoa kafara, mkampokonya ndoto zake, ili aishi ndoto zenu?! Kwa hiyo mnachotaka ni yeye aishi ndoto zake, zenu na zangu?”

“Yaani mnataka nikitaka kufanya jambo ni mpaka nikamtafute yeye, akikubali au akiwa na muda wakunisikiliza, baada ya kazi ya ndoto yake kuisha, pengine familia yake ya mume na watoto ambayo nyinyi mnahangaika aipate huku mkiua yangu, ndio mimi nimsubirie, nimueleze juu ya ninachotaka kufanya, akikubali au akiwa na muda aidhinishe?” Akauliza kwa ukali sana, na sauti ya juu.

“Hata hivyo Colins, kumbuka hata sisi tukikupa share zetu, kuna asilimia 15 tuliuza kwa watu wengine ili kupata pesa ya kuendeleza pale.” “Wewe huko kwingine niachie mimi. Si umetaka mimi ndio nikuendelezee mali ili ufe tajiri kwa garama ya maisha yangu?” Mzee kimya. “Basi usiwe na wasiwasi, huko niachie mimi. Ushamaliza ya kwako, nataka na ya Connie. Tena acha nimpigie sasahivi, tumalizane kabisa. Ili wakati nyinyi mnafanya kazi zenu huko, na mimi nikawafanyie za kwenu huko kwa ufasaha.”

Akatoa simu na kuipiga palepale wazazi wamepigwa na butwaa. Ilikuwa bado ni saa 12 asubuhi wazazi wanawahi foleni wafike kazini kwa wakati. Connie akapokea kwa haraka maana hakutegemea simu kutoka kwa kaka yake. Hakuwa amezungumza naye wala kurudi hapo kwao tokea amfukuze.

“Coly!” Akaanza kwa upendo. “Baba anataka kuzungumza na wewe.” Akawa anamkabidhi simu baba yao, mzee akabaki ameduaa hajui azungumze nini. “Au unataka mimi ndio nizungumze naye?” Colins akauliza kwa mkwara. Alimjua baba yake. Huyo binti yake ni mboni ya jicho. Anaongeaga naye kwa kubembeleza.

“Labda nikazungumze naye nikifika kazini tukiwa ana kwa ana.” “Hivi nyinyi, mnataka nini kwangu? Eti mzee? Hukunikuta na maisha yangu, mkayatoa hapa duniani, tena nyinyi wote watatu mkisaidiana, ukitaka nikutumikie? Sasa, sasahivi nipo tayari, unataka kunizungusha?” Mzee akapokea simu. “Tafadhali iwe kwa kifupi na mimi niwahi kazini.” Akaongeza kama ambaye hataki tena kupotezewa muda. Mzee akameza mate na kuanza.

“Umeamka salama mama mzazi?” Akaanza mzee, Connie akasalimia na kuuliza. “Kuna nini dad?!” “Nitakueleza zaidi tukikutana ila ili kufanya Colins afanye kazi kwa kifasaha, anaomba sehemu ya share zako za ile kampuni ambayo ina hospitali.” “Achukue tu hata zote.” “Nafikiri ubakiwe na kiasi, mama. Itasaidia baadaye kwenye kufanya kazi pale kama mtawala pia, sio mwajiriwa wa kawaida.” “Natakiwa kufanya nini?” Akauliza Connie taratibu tu.

“Mwambie afungue email yake sasahivi. Aweke saini, kisha anitumie. Sasahivi tafadhali.” “Umesikia Connie?” Mzee akamuuliza kwa upendo. “Nishafungua dad.” “Mwisho kabisa kuna sehemu ya jina lake na saini. Atatakiwa ai print, ajaze jina kamili na kuweka saini kwa mkono. Kisha aiscan na kunitumia.” “Nitafanya hivyo.” Alivyosikia hivyo akaanza kukusanya karatasi walizosaini wazazi wake.

“Sasa, kwa kuwa wote mna share pale, nataka wamiliki hai. Ninapoitisha kikao cha wamiliki wa ile kampuni, mfike. Msinipotezee muda na kutoa sababu ya majukumu mengi, wakati wote tuna majukumu. Nitatuma kalenda ya vikao vyote kwa mwaka mzima, na muda wake ili mjue mapema na kujipanga kuhudhuria tuendeleze mali ya familia.” “Wazo zuri.” Mzee akaongeza kwa kujihami.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Cha mwisho nisiwapotezee muda wenu zaidi. Nimebadili mawazo. Narudi kuishi nyumbani kwangu. Ile nyumba ya Kigamboni ni mali ya kampuni, inaanza kuingiza pesa kwa sababu lengo lenu naona limeshindikana. Ilikuwa nikaishi kule na Love, kama tungeoana. Lakini kwa taarifa za kusadikika, Love yupo kwenye mahusiano na Festo tangia nikiwa nikiishi naye. Kwa ninavyowafuatilia mipango yao, wataoana na wana baraka za wazazi wa pande zote mbili, wakiwepo rafiki zenu wapenzi, kina Simba.”

“Yaani wakati nyinyi mnanitoa mimi kwa mwanamke ninayempenda sana kwa dhati, ili kuwafurahisha wao, mkiniumiza mimi, rafiki zenu wao walikuwa wakimsikiliza binti yao. Aliponigeuza tahira, akiwa ananifungia ndani bila chakula, wakati na nyinyi mmenitelekeza nikiishi kama yatima, basi alipoona sifai tena, akazungumza na wazazi wake tena, wakati uleule wakamuunga tena mkono awe na Festo.” Wazazi kimya wakizidi kuumia.

“Sasa basi, najua kwa kuwa Festo sio mtoto wenu, hawataweza kwenda kuishi pale. Na mimi sitaishi pale kwa sababu nahitaji pesa kwa ajili ya kuendeleza kampuni, zaidi ile hospitali. Nishaanza kuandaa matangazo mtandaoni. Nitatuma watu wakasafishe, niweke iwe AIR BNB. Nitakodisha mpaka kwa wageni wanaoingia nchini au familia inayotaka mapumziko kwa siku chache eneo la ufukweni kwenye mazingira mazuri kama yale.”

“Sasa basi, mwambie mpangaji wako, nampa siku 5 tu, awe ametoka kwenye nyumba YANGU.” “Naomba uvumilie mpaka mwisho wa mwezi huu. Nikishazungumza naye kuwa mkata…” Colins akaondoka bila kusubiri baba yake amalizie. Wote wakahema kama waliopata aghueni baada ya kusikia mlango wa chumbani kwake umebamizwa kwa nguvu sana.

Wakati Wa Kubomoa Na Wakati Wa Kujenga.

Alipotoka majira ya saa moja, hakuwakuta wazazi wake. Akapata kifungua kinywa vizuri na kwa amani, kwa kuwa hakuwakuta pale. Yaani ilikuwa akiwaona wazazi wake ndio hasira zinampanda. Hapo akawa ametulia. Akala vizuri na kutoka na yeye kwenda kazini. Alifika akakuta ofisi yake ipo safi ikimsubiria. Alishajua ni jitihada za baba yake. Alizungumza nini na Simba, hakutaka kujihusisha nayo.

Akamuita sekretari wa upande huo wa ofisi za viongozi. Akamsalimia kwa uchangamfu na kumpa pole ya kuugua lakini Colins akamkata vibaya sana. “Tafadhali fanya utaratibu nipate simu mpya yenye namba mpya. Iwe leo tafadhali.” Akatoka maana hakumuwekea sura ya kirafiki kabisa akijua ni mmoja wa vibaraka wa Love pamoja na wazazi wake Love, waliokuwa wakitumwa kutoa taarifa za uongo juu yake wakati wamemfungia akiwa tahira akiwa anaishi na Love.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaanza kazi zake akiwa tayari na mamlaka hapo zaidi ya kila mmoja wao. Akamuita muhasibu kutaka kujua hali ya kifedha inavyoendelea. Na utaratibu ulivyo wa kutoa pesa. Akajieleza kwa kina Colins akimsikiliza na kuandika mpaka akamaliza. “Sasa kuanzia leo huo utaratibu unabadilika. Nimeshakutumia wewe barua. Kuanzia leo, kila matumizi ni lazima mimi ndio niidhinishe hata kama ni madogo vipi. Hakuna yeyote anaruhusiwa kutoa pesa bila na mimi kuidhinisha. Yeyote yule. Namaanisha hata mzee Simba akikuuliza, mwambie aje kwangu.”

“Utaratibu mwingine wote nimeandika hapo na nimewatumia viongozi wengine wote, pamoja na wadau wakubwa. Matumizi yote na mapato, kila siku, kabla hujatoka ofisini, hakikisha vimekaa sawa na mimi naona hapa kwenye kompyuta yangu. Nitakachokiona kwenye mahesabu yako, kiwe kimefanana na uhalisia wa pesa iliyopo benki. Ni hilo tu.” Akimuashiria amemalizana naye. Akaondoka akijua ndio wizi wa pesa ndogondogo walizokuwa wakigawana hapo, ndio MWISHO.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaomba kuongea pia na kiongozi wa utawala, masijala na kila aliyeona anashikilia nafasi hapo ofisini, akaomba kuzungumza nao mmoja mmoja akiwasikiliza, kuandika kila anachoona anahitaji kuja kukifanyia kazi, huku akiuliza maswali. Akiridhika anampa utaratibu mpya wa jinsi ya kuendesha mambo.

Pesa haikutakiwa kulala kwingine isipokiwa kila siku na mwisho wa zamu wa kila anayepokea pesa, kukabidhisha kwa muhasibu akiwa na mahesabu yaliyo kamilika. Hapo anatoa muongozo huku akiweka muundo mpya mzuri wakueleweka kwenye hizo kompyuta za hospitali nzima.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akawa ameshapigia simu mafundi wa kamera. Zikawekwa mpaka mapokezi. Kisha akazungumza na watu wa mapokezi. “Hapa ni hospitalini, wote wanaofika hapa wanakuwa wanatumaini sisi ndio tuwasaidie. Majibu yasiyoridhisha kwa yeyote, kwenye hospitali hii sio sehemu yake. Kutakuwa na kamera na vinasa sauti vikifanya kazi masaa 24 kama huduma zetu zilivyo. Siku unapotakiwa kuwa umesimama pale, na hujisikii kuzungumza au kusaidia wagonjwa wanaofika hapa kutaka msaada, tafadhali usisimame pale. Tuwapishe wenye uwezo na nia ya kazi.” Akawaweka sawa, mpaka inafika jioni kila mmoja akajua mambo yamebadilika hapo. Na Colins huyu siye aliyeondoka mwanzo.

Kumbe muda aliokuwa akijiuguza, pia alikuwa akipanga ya hapo. Akaomba sekretari atume ujumbe kwa madaktari wote wanaofanya kazi hapo, kuwa kesho yake, wale wanao ingia asubuhi, basi wajue kutakuwa na kikao kabla ya kazi, na wa jioni hivyohivyo. Kichaa kapewa rungu!

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati Colins anaendelea na yake, familia ya Simba bado ilikuwa imetaharuki hawajui Love alipo mpaka ilipofika jioni kabisa ndipo mtu mmoja akawapigia simu na kuwaambia kuwa Love ameshikiliwa na polisi kwa kosa la wizi, yupo kituo kikubwa cha Oysterbay. Ndipo sasa wote kukimbilia polisi wakiwa wamemuomba Chris na yeye afike kuwasaidia.

Wakaomba kujua habari zake, wakaambiwa anashikiliwa kwa kosa la wizi wa mamilioni ya pesa tena la muda mrefu. Kwamba alikuwa akiibia kampuni kidogo kidogo kwa muda mrefu. Alipotaka kuombewa dhamana, muda ulishaisha, alikuwa akipelekwa mahabusu ya Keko.

Mama Simba alikuwa na hali mbaya kuweza kufikiria kwani hata Love mwenyewe walikataliwa kumuona, waliambiwa wasubiri mpaka kesho yake wafanye utaratibu wa kumuona  huko mahabusu ya Keko. Ila Chris yeye kama wakili wake alipewa dakika chache sana akiwa anakwenda kupandishwa kwenye karandinga, kutolewa hapo. Siku yao ikazidi kuwa mbaya. Ni Love, mtoto waliyemsomesha na matunzo ya hali ya juu hivyo! Leo anakwenda lala na wahalifu, tena wanao waona ni wa hali ya chini! Ilikuwa msiba kamili.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kichaa Kapewa Rungu!

Ni nini atafanyia hayo madaraka makubwa hivyo yaliyopo mkononi mwake Colins aliyejeruhiwa moyo?

Hatimaye amefanikiwa kumlaza Love GEREZANI. Kwa muda gani?

Je, atafanikiwa dhamana?

 Kemi je?

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment