Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 7. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 7.

Huku kwa Jelini yeye alisharuhusiwa kurudi nyumbani. Alichokifanya ni kurudi chumbani kwake na kulala mpaka jioni alipoamshwa kuwa wageni wamefika, muda wa chakula kisha ibada ya shukurani. “Na zawadi zako hizi kutoka kwa Ezra na Junior.” Mama yake akamuwekea hapo mezani kwake na kutoka. Akaangalia na kujikuta akicheka. Maua, baluni na chokleti kama alivyokuwa ameletewa na Kasa.

         Akajisafi kidogo, na kutoka. Akawasalimia wote kisha akaelekea moja kwa moja sehemu aliyokuwa amekaa Ezra na Junior. Ila akakaaa pembeni ya Ezra, akatulia. “Vipi?” Akamuuliza kwa upendo akimshika mkono na kuangalia pale alipochomwa sindano ya dripu. “Nipo sawa ila usingizi hauishi!” “Pole. Mama aliniambia uliweza kunywa uji.” Akatingisha kichwa kukubali kisha akatulia.

“Kuna nini, mbona kama una kitu unashindwa kusema?” “Niliambiwa Kasa na yeye alikuja tena jana usiku.” “Ndiyo.” Jelini akamwangalia na kunyamaza maana alijibu kwa kifupi tu.

“Ni nini?” “Mimi najua utanichoka Ezra. Ila mimi hao watu nilishamalizana nao muda mrefu hata wao wanajua.” Kidogo akafarijika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Yeye Jelini alidhania anahofu, lakini asijue yeye Ezra ni zaidi. Alijiona yupo na upinzani mkubwa, kila kona. Tena wenzie ni kama wanamzidi kwa mbali sana.

Alishakutana na Kasa. Akaona nguvu ya pesa na uwezo mkubwa wakufikiria na kuchukua hatua kwa haraka. Kisha Colins. Kwa upande fulani ni kweli walimtisha. Sasa kusikia mrembo mwenyewe anahofia asimuache, hali ya uwanaume ikainuka ndani yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Halafu na leo tena ametuma mtu alete maua na chokleti.” Jelini akaendelea kuongea na Ezra kwa sauti ya chini. Kama anayesemelezea na kujihami hapohapo. “Ila nilimrudisha navyo huyo aliyetumwa. Halafu tena akaja yeye mwenyewe Kasa.” Hapo anamwambia kumbe huyo Ezra alishapata taarifa zote. Akajadili na Junior, kisha kupewa ushauri na mama yake juu jinsi ya kukabiliana na hao EX wa Jelini. Hapo alipo alishajua nini chakufanya. Jelini anatoa taarifa kwenye fikra zilizokwisha tishwa, kisha kupata muda wa kujadili hali nzima na kupata jibs. Hapo alipo alikuwa ametulia. Si taarifa za kushitukizwa. Ila furaha ya kuona amemwamini na hizo taarifa pia. Hajamficha.

“Nisikilize Jelini na hili hata mimi najikumbusha. Hizi ni kelele za muovu tu, kutaka kututoa barabarani kwenye safari yetu. Sisi hatujui kesho yetu. Pengine yeye muovu inamtisha. Shetani hapendi familia wala ndoa. Popote kwenye ndoa takatifu na familia bora, ambao ni msingi wa kila kitu. Jamii mpaka taifa, anaharibu. Anajua akigusa familia, amegusa taifa na ndio ulimwengu mzuma na vijazavyo.”

“Atafanya kila namna aharibu. Sisi ndio tusimpe nafasi. Tumeshajua tunachotaka.” “Mimi nakutaka wewe Ezra.” Hakujua faraja anayompa kijana huyo. Na sifa mbele ya familia pia. “Basi tutulie. Tutafika tu. Na usiogope. Mimi nakupenda na nimeamua kukuoa. Tutafanikiwa. Acha wapige kelele kwa kadiri ya uwezo wao. Sisi tusonge mbele, tusipoteze lengo.” Hapo akamuona amejiegemeza kabisa kwenye bega amemlalia na ni hapo sebuleni kila mtu yupo.

“Unataka nikuletee nini chakula?” Junior akamuuliza kwa kujali. Jelini akacheka na kumwangalia. “Pole na kazi, na usingizi.” “Pole wewe kwa upweke.” “Nimelala siku nzima. Nimefurahi kuwaona.” “Na mimi pia. Sasa niambie nikupe nini. Lakini isiwe kitu kigumu.” “Wameniambia.” “Namletea uji huyo.” Mama Jema akadakia. “Basi acha mimi niufute, wewe uendelee na kingine.” Akasimama na kuelekea jikoni alipokuwepo Emelda, Jema, mama yao na mama mchungaji wakiandaa vyakula. Kuweka mezani na kupasha moto.

Walipata mlo wa pamoja. Wakamshukuru Mungu. Kwamba yale aliyokuwa amekusudia shetani kwa ubaya, basi Mungu ameyabadili kwa wema. Wakapata muda mzuri hapo, usiku huo wakawahi kutawanyika. Kesho yake ilikuwa siku ya kazi. Na usiku uliopita ni kama hawakulala vizuri.

 Halafu mama Emelda alikuwa anakutana na daktari asubuhi ya siku inayofuata. Akisindikizwa na mama mchungaji pia. Na Jelini mwenyewe alikuwa akisinzia muda wote, hata maneno mengi hakuwa nayo. Kwa hiyo kila mmoja alikuwa na sababu ya kuwahi kulala.

 ~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati anakaribia kulala, ujumbe ukaingia. Akavuta simu kwa haraka akidhania ni Jelini, ndio akakutana na huo ujumbe kutoka kwenye namba ngeni. Unasema hivi.

‘Kuna usemi unasema, ‘If you love something, set it free. If it comes back, it's yours. If not, it was never meant to be.’ Ndicho ninachokifanya kwa Jelini, mwanamke ninayempenda sana hapa duniani. Kwa sasa, kuwa na mimi imekua ni mateso kwake, kitu kinachoniumiza sana. Namuacha huru, kwako, lakini nina ombi moja ambalo litabaki kuwa deni, na tafadhali hakikisha unakumbuka.’

 ‘Mlinde Jelini kama mboni ya jicho lako. Lakini, ikitokea tu, umemchoka au umeamua kumuacha, kwa sababu yeyote ile, tafadhali, kabla hajatoka kwako, mimi niwe wa kwanza kujua. Haijalishi muda. Iwe kesho au miaka 10 ijayo. Ana mtoto mmoja na wewe au 7, tafadhali ukumbuke kunitaarifu. Ni hilo tu. Na nakuahidi sitakuwa mbali, ila nitaheshimu maisha yenu. Sitaingilia, mpaka inilazimu.’

Moja kwa moja akajua ni Colins tu, japo hakuweka jina. Akafikiria kwa muda wa kutosha, bila ya kupata jibu sahihi lakumjibu. Mwishoe akautuma kama ulivyo kwa Junior. Baada ya muda akarudisha majibu. ‘Colins?’ ‘100%.’ Ezra akajibu. Kimya kwa muda. Kisha akamtumia tena ujumbe mwingine. ‘Hekima tu.’ ‘100%.’ Ezra akajibu tena  hivyo akiwa amemuelewa vizuri sana Junior. Lugha yao ya mafumbo kwa kifupi. Kweli hakumjibu kitu, akalala.

Secret Admirer.

Huku kwa Colins wakati akisubiria majibu ya Ezra kuona anajibu nini, bado alikuwa kazini mida hiyo. Alishazunguka tena karibu hospitali nzima. Gorofa hilo la uongozi alibakia peke yake. Hana pakwenda, hana afanyalo isipokuwa hiyo kazi tu. Ujumbe ukaingia kwenye simu yenye namba mpya kabisa aliyokuwa ameagiza asubuhi hiyo. Aliletewa ila sababu ya mambo mengi wala hakuwa ameigusa. Ilibakia tu hapo mezani ilipokuwa imeachwa na sekretari. Akafikiria kidogo, akaona afungue na kusoma.

Akakutana na ujumbe uliomshangaza. ‘Ninapo kwambia nakupenda kila wakati, sisemei mazoea. Wewe ni kitu pekee na cha thamani ulichowahi tokea maishani mwangu.’ Colins akakunja ndita, asielewe. Ila akapuuzia.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake asubuhi akiwa anajiandaa kwenda kazini, akasikia kama ujumbe umeingia tena kwenye simu ileile mpya kwake. Akaisogelea pale ilipokuwa mezani na kukuta kweli kuna ujumbe. Akasoma. ‘Kukuona usiku kwenye ndoto zangu, kumenipa nguvu ya kuianza siku yangu vizuri. Daima utabakia kuwa nguvu yangu.’ Colins akashangazwa na kukaa kabisa kitandani na kurudia kusoma. “Ni nini kinaendelea!?” Akajiuliza bila ya jibu. Akajiambia akitulia, atafuatilia kujua ni nani anamtumia hizo jumbe.

Alipofika tu hata kabla hajaingia ofisini kwake, ikabidi amuulize aliyemtuma kununua hiyo simu. “Nilipokwambia ukaninunulie simu na line mpya, ulifanya hivyo?” “Kabisa. Hiyo simu nimetoa mwenyewe kwenye karatasi na boksi lake na line tumesajili kwa matumizi ya kiofisi. Ni mpya kabisa. Kwani vipi!?” Colins akaondoka na kutunza hilo moyoni akijiambia atafuatilia kimyakimya.

 Bahati Haichezewi.

Ezra.

Ilipofika majira ya saa nne asubuhi Ezra akapokea ujumbe kutoka kwa Jelini. ‘Nimeamka nina hamu na wewe tu, mpenzi wangu. Hujanikumbatia muda mrefu!’ Aliposoma tu vile akili ikavurugika. “Tafadhali tuoe Junior. Mimi siwezi tena kusubiri.” Ilikuwa katikati ya kazi. Wawili hao walikuwa wamezama kila mmoja mezani kwake na yake, kimya hapo ofisini kwao hawakuwa wameongeleshana kwa muda wa kutosha tu, kuashiria wamebanwa na majukumu yao mpaka hapo alipomtoa mwenzie katikati ya hayo majukumu mazito.

Akamtizama kwa sekunde kadhaa kama anayejaribu kuelewa hayo yanatoka wapi na mipango ipo tayari! “Tafadhali tukamilishe hii safari.” “Sawa. Si ndio nachumbia jumapili hii na hapohapo tangazo letu la kwanza la ndoa linatoka?” “Mimi nataka kumuoa Jelini.” Junior akabaki akimtizama. “Namaanisha kumuoa kwa haraka kwa sababu watu wengi wanakuwa wanamuwinda. Kuendelea kuchelewa nakuwa kama nachezea bahati.” “Sawa.” Akamuona anasimama na simu yake nakutoka.

Bale!

Huku kwa kina Bale na Vai wao mambo yalikuwa yakiwaendea sawa kabisa chini ya uangalizi wa Joshua. Walishapewa orodha ya mahari ikabaki kazi ya manunuzi, na muongoza manunuzi ili wapeleke vitu vizuri ukweni siku ya jumamosi ni mama G. Hakutaka kitu kiharibike. Mipango ilikuwa ikiendelea ili kufanya kwa kiwango cha juu, haraka na uhakika ili harusi ufungwe kwa wakati kabla Vai hajarudi chuo.

Mpaka Grace alikuwa akienda Moshi kusindikiza kulipwa hiyo mahari. Kukawa na uungwaji mkono wa hali ya juu, kila mtu akijitolea kwa heshima ya baba Naya, na Joshua aliyegeuka pacha wa Geb. Ilikuwa ngumu kuwatenganisha tena. La Geb ujue ni la Joshua. Mchana na usiku lao moja.

Jema na wifi zake walikuwa wakiondoka hapo siku ya ijumaa alfajiri sana, angalau kuandaa mazingira huko kwa mzee aliyekuwa amechwa peke yake huko kwao. James alikuwa akiondoka na mama yao ijumaa hiyohiyo ila jioni baada ya kutoka kazini, kisha kina Joshua, familia yake na ya Magesa pamoja na bwana harusi, Bale, walipanga kuondoka siku ya jumamosi alfajiri sana. Kwamba hata kifungua kinywa wakapate hukohuko Moshi ambako wangekutana na familia ya Grace kwenye hoteli ambayo wangelala hapo. Maandalizi yakaendelea wawili hao wakishindwa kabisa kutengana.

Alijaribu Naya akiwa na Joshua. “Pengine kipindi hiki cha karibia ya harusi mngeishi tofauti.” Walikuwa nyumbani kwao, wamewakaribisha kuweka mipango sawa. Wazo hilo Naya alilitoa mezani wakila. Wote waliwaona jinsi walivyo badilika. Hata chakula kilishindikana kula. Wote wawili kimya. Hakuna aliyejibu.

“We Bale? Sasa mnakwenda kufunga ndoa mnatokea nyumba moja?!” “Acha tufikirie kisha tutaamua na Vai.” Ndio likawa jibu lao ambalo hata Vai akaiga. Jema naye alipomshauri, akajibu hivyohivyo kama Bale. Walipoambizana, Joshua akashauri waachwee tu. Maana ilikuwa kama kitu kinachowanyima raha kabisa, na inakuwa kama umewafukuza hapo. Ukishaanzisha tu hayo mazungumzo, jua hawataendelea kukaa hapo. Wataaga na kuondoka kabisa. Kwa hiyo maandalizi yakaendelea kwa kasi ili jumamosi hiyo ikalipwe mahari, maharusi hao bado wakiishi pamoja.

Kwamba Vai arudi kuishi kwa mama yake pamoja na Viola na mwanae! Aache ule utulivu pale kwa Bale anakopikiwa na kubembelezwa! Hakutaka tena. Na kwa upande wa Bale yeye Upweke ulishaondoka. Akapata mtu wake wa uhakika. Analala akiangalia mlango akijua mrembo Vai yupo ndani! Hajaonja hata mara moja! Na mara ya mwisho Vai kutoka hapo aliishia hotelini na mwanaume! Hakutaka kumpa shetani nafasi ya majaribio tena.

Colins!

Mambo yakawa mengi akajikuta ametingwa na kusahau jumbe zote. Akili ikawa imezama kabisa kwenye kazi. Mara ujumbe mwingine tena ukaingia kwenye simu ileile. ‘Ulikuwa sahihi juu ya Luca, japo sikutaka kukwambia. Imekua kama ulivyosema. Aliniomba tukutane naye kwa chakula cha mchana. Nikadhania anataka kuzungumzia juu ya hatima ya biashara ambayo hata sisi tuliwekeza hapo. Lakini imekua tofauti. Anataka mahusiano. Lakini moyo wangu umekataa kabisa.’

‘Nilipomwambia si sawa, tutakuwa wasaliti kwako, imekua mbaya sana. Anahakikisha kuyafanya maisha yangu kuwa magumu kwa makusudi ili kunikomoa. Jana ndio amemalizia kwa kunipokonya ile pete uliyonivalisha na gari uliyonipa, akisema ilikuwa kishika uchumba, sasa maadamu hutanioa, na nimemkataa yeye kama muendeleza ukoo, eti basi sistahili tena.’

‘Lakini sijali. Hakuna na sitaki mtu azibe pengo lako. Nakusubiria wewe tu. Hata kama itachukia miaka zaidi ya miaka 10 kuanzia sasa, nipo tayari kukusubiri. Moyo wangu umekosa nafasi ya mtu mwingine ila wewe tu. Nakupenda na nitaendelea kukupenda mpaka pumzi yangu ya mwisho.’ Ujumbe ukaishia hapo na kumtoa Colins kwenye kazi kabisa na kubaki akitafakari.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo Yanazidi Kuchanganya.

Akiwa Amejipanga na yupo katikati ya uwanja wa Vita, kutaka kulipa kisasi kwa kila aliyemtenda, jumbe za mapenzi tena zinaanza kwa Colins. Ni nini tena Kinaendelea?

Love huko Lupango!? Kemi!?


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment