Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 4 – SEHEMU YA 9. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 4 – SEHEMU YA 9.

Alipofungua tu Instagram, akakutana na kijana mzuri sana. Alishituka sana aliposoma comments. ‘RIP’. Mwili mzima ulikufa ganzi. Ndipo akajua huyo msichana anamwandikia marehemu mpenzi wake. Akashangaa sana. Akaangalia mwaka aliokufa, tayari ilikuwa ikikaribia miaka miwili. Akapata hamasa ya kumtafuta huyo mrembo aliyeachwa na donda moyoni.

Akaendelea kupekua zaidi ndipo akakutana nao. Colins mwenyewe akajikuta akihamaki kwa sauti. “Haaaah!” Alitegemea kukutana na choka mbaya, lakini akaja kukutana na pisi kali, yeye mwenyewe akapigwa na butwaa! Huo ukurasa wa huyo marehemu Mike, ulipambwa  picha zake na huyo mrembo na walikuwa na watu wengi sana wanao wafuatilia.

Kwa aina ya picha zao na muonekano wao, hata yeye Colins aliona wanastahili kufuatiliwa. Kwanza wao wenyewe walikuwa wazuri sana wa sura na waliendana mno. Walionekana walikuwa na uwezo wa kutoka hata nje ya nchi. Nadhifu kwa mavazi tofauti tofauti. Colins akajikuta amezama hapo akiendelea kuangalia muda ukienda hamalizi na hataki kutoka.

Yeye mwenyewe alikubaliana na mrembo Kamila, ni kwa nini abaki akimuwaza huyo jamaa. Tukio lililomsikitisha la mwisho, ni kama ndio amemvalisha pete ya uchumba. Hawakuonekana kama walifikia ndoa. Akajikuta akimuhurumia huyo Kamila ambaye alijua jina lake kwa pongezi walizokuwa wakipewa huko mtandaoni. Akabaki ameduaa akimtizama jinsi alivyokuwa mzuri. Kila picha hapo aliyoona, alijawa cheko halafu akawa na dimpozi zilizoongeza uzuri wa kucheka. “Hata meno yake ni mazuri sana.” Akajikuta akimsifia kwa sauti na kubaki akimtizama.

Loreta kwa Colins

Simu ya Loreta ikamtoa kwenye kurasa ya marehemu Mike na mchumba wake. Akaitizama bila ya kupokea mpaka ikakata. Alishajua shida yake. Akapiga tena. Hakupokea. Kisha akamtumia ujumbe. ‘Tafadhali naomba nisikilize tu Colins, ndio uamue.’ Akasubiri kidogo, akaona anampigia tena.

“Ni usiku sana sasahivi, unataka nini?” “Naomba unikopeshe pesa.” “Sina.” Akamjibu kirahisi tu na kukata simu. Akampigia tena. “Naahidi kukulipa Colins. Tumekwama. Tupo kwenye kukusanya pesa. Najua sisi ni watu wa mwisho kabisa kutaka kutusikia, lakini hatuna jinsi. Na ukumbuke katika yote, mimi sihusiki kabisa. Hapa nipo mimi kama mimi, naomba msaada wako.” “Ni nini kinakupelekea kudhania ninayo hiyo pesa unayo ihitaji?” “Baba ametuambia sasahivi wewe ndiye unayeshikilia kampuni nzima ikiwepo hospitali. Na nakumbuka mshahara alioniambia Love uliokuwa ukilipwa zamani. Sasa..” “Loreta. Sina muda wa kukusikiliza.” Akamkatia tena simu.

Akampigia tena. “Basi kama huamini kama naweza kukulipa, tuandikishiane kabisa na nakupa ruhusa upeleke hayo makubaliano mpaka kazini kwangu, mwisho wa mwezi wawe wananikata na kukulipa, endapo sitakulipa. Tafadhali Colins.” “Njoo hapa hospitalini, ila iwe ndani ya dakika 45, vinginevyo hutanikuta.” Kisha akakata simu.

Wakati wa Kukusanya.

Colins alijawa furaha kwani ni kama mipango yake ilikuwa inakwenda kama alivyopanga. Kila kitu kilikuwa kikiangukia kwenye mstari. Akaandaa karatasi yake na mazingira, ndani ya dakika 20 Loreta akawa amewasili. Akaanza kumrubuni kimapenzi. “Nisikilize Loreta. Kwa kuwa nyinyi nawafahamu, tokea unaingia hapa ndani, kuna kamera zinakuchukua, ili usije nibadilikia.” Alishituka sana, mpaka Colins akajua alikuwa sahihi, ni kweli alikuwa na lengo baya kwake. Zaidi kupiga kelele kuwa anambaka.

“Mimi si mjinga, kama mnavyonifikiria. Nimeishi na nyinyi nawafahamu vizuri tu. Matapeli wa bila huruma. Waongo msiofikiria mnaye muangamiza, na wezi msio na aibu kuvuna msipopanda. Kuchukua kisicho chenu si tatizo. Nyinyi wawili na wazazi wenu ni waovu kama mlioingia ubia kufanya kazi za shetani kwenye maisha ya watu. Sasa tulia tufanye ya msingi. Hila zako hapa hutafanikiwa. Na sina shida na wewe kimapenzi. Unanielewa?” Alinywea Loreta kama siye yeye. Umapepe wote kwisha.

“Unahitaji kiasi gani?” Akamtajia. “Unampango wa kunilipa vipi?” Akakwama ndipo alipojua alitaka kumtapeli tu. “Sasa mimi nina njia naweza kukusaidia endapo utakubali.” Akakaa sawa. “Wewe una share hapa. Naweza kuzinunua kwa hiyo pesa unayotaka.” Loreta akashangaa sana. Hospitali yenyewe ni kama wazazi wake alisikia wakilalamikia muda wote. Hakuna cha maana na wala hakujua hizo share zitamsaidia vipi. Kulinganisha na pesa aliyoahidiwa kupewa, alivyo mapepe, akakubali kusaini karatasi alizopewa bila ya kusoma asujue share anazouza hapo ni za kampuni nzima. Sio tu hospitali.

Colins akampa hundi, asiamini. “Haya, usiku mwema. Na acha dhuluma.” “Mimi sijadhulumu mtu.” “Ila ulipanga ukikutana na mimi upige kelele nimekubaka ili niishie jela, mnidhulumu haki zangu zote! Si ndivyo ulivyokuwa mmepanga na wewe ukajitolea kuja hapa kutekeleza?” Alivyopoa, akajua ni kweli. Akacheka kwa masikitiko sana. “Mnaamini mimi ni mjinga kama mlivyokuwa mkinisema na dada yako!” Kimya. “Haya toka. Nenda kawaambie waliokutuma kuwa umekutana na Colins ambaye hukuwa ukimjua kabla. Haya toka.” Akatoka kinyonge lakini akiwa na pesa.

Colins na yeye akafunga ofisi kurudi nyumbani akiwa na furaha ya ajabu. Kwamba amemudu kupata na hisa za Loreta pia! Akafurahi sana. Akajiambia ni kuendelea kupanga kwa makini bila ya kuchoka. Ila akawa ameongezeka tatizo Chris, wakili wa Love na Kemi.

Mapenzi.

Mchana wake huku kwa Ezra alitoka hapo ofisini akikimbilia kwa Jelini muda uleule alipotumiwa ujumbe. Akili ilishavurugwa. Nia yake aione tu sura yake na kutimiza shauku ya kumuweka mikononi kama alivyomuahidi. Alifika kwao mama yake hakuwepo, Jeremy yupo shule. Mungu ampe nini! Lakini Ezra si Colins, hawezi kukaribia chumbani. Baba ambaye ni mchungaji ni yule anayeanza kuchunga nyumbani kwake kwanza. Hao vijana amewasimamia kwenye mstari, hazembei. Hawaangalii umri wala pesa. Ikifika kukemea, hajali kama ni waajiriwa wa benki kuu ya Tanzania, ila vijana wake.

Akajipanga kwenye kochi, Jelini akajisogeza. Hakuhitaji kufikiria jinsi ya kukaa mikononi kwake. Mpenda mikono akawa ameshajiweka sawa mpaka Ezra akafurahia jinsi alivyotulia hapo.

Nakupenda Ezra. Na mimi nataka tubaki hivihivi mpaka kifo.” “Ile ahadi ya kunisubiria ili tuoe pamoja na Junior si bado ipo?” Hapo anamuuliza akimbembeleza kwa kumpapasa taratibu. Sauti nzuri, Jelini akatingisha kichwa kukubali nakuongeza. “Nitakusubiri Ezra. Ila natamani tusivute tena. Natamani tuishi wote.” Akambusu pale alipokuwa amemuegemea. Na kumnong’oneza sikioni. “Nakuahidi haitavuta. Hata mimi nakuhitaji Jelini.” Akajigeuza vizuri ili afikie midomo ya Ezra. Kiss za kujinafasi zikaanza ila kwa makini ili asipitilize kama alivyoonywa na baba yake, akikumbuka madhara ya kuonja kabla hajakabidhiwa chakula. Wakaendelea mpaka Jeremy aliporudi kutoka shule. Akamsalimia na kuuliza habari za shule, akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alitoka hapo amejiwasha moto, hawezi kujisaidia. Jelini mikononi, halafu apewe na kiss ya muda mrefu! Hoi taabani. Akiilaani amri ya 6. Kwa nini iliwekwa! ‘Tafadhali tuoe Junior.’ Ujumbe ukaingia Junior akizungumza na Emelda. Akamjibu, ‘Nitakupigia tujipange vizuri. Nipo na Emelda kwenye simu.’ Junior akajua mwenzie amelemewa, lazima waharakishe.

Kule Kuliko Ungua Penzi, Kukabaki Donda.

Wakati anakaribia kupata usingizi ujumbe ukaingia kutoka kwa Kamila akimtumia Mike. ‘Tutakapo kutana tena, nitakung’ang’ania ili isiwahi kutokea tunatengana daima. Ulale ukijua unapendwa daima.’ Ikawa faraja ya ajabu kwa Colins, japo ujumbe alijua fika si wake. Akabaki akiikumbuka sura yake na hayo maneno mpaka akapitiwa na usingizi.

KESHO YAKE.

         Mida ya saa nne asubuhi mzee Simba akapiga simu anawaka kama pilipili. “Hizo mali unazotaka kunidhulumu nazo, nimeamza kutafuta hata kabla mimba yako haijatungwa. Huwezi kunizuia mimi nisikope benki kwa kutumia hati ya nyumba yangu.” “Kabisa.” Colins akamjibu akijua fika alipo kwama. “Sasa mbona umeweka vipingamizi kwenye mabenki nisikope?” “Nafikiri utakuwa hujapewa taarifa kamili. Pingamizi zipo kwenye mali ya kampuni ambayo mlitafuta na baba yangu, kabla mimba yangu haijatungwa, kama sikosei. Sasa kama hizo ndizo unazotumia sasahivi kujipatia mikopo yako binafsi, haitawezekana.”

         “Kwa nini isiwezekane wakati ni jasho langu!?” “Jasho lako na baba yangu kwa familia NZIMA na kizazi kijacho. Nafikiri hilo ndilo lengo la tokea mwanzo na hatuwezi kuyumba hapa katikati.” “Sasa Love si ni mmoja wa hao uliowataja? Atanufaika vipi na hiyo kampuni kama kipindi kama hiki anauhitaji hatasaidiwa na hiyo kampuni?!” “Tukianza kuweka matatizo yetu binafsi hatutafika popote. Kila mtu anauhitaji wake na lazima tufuate utaratibu. Hatutafanya tena mambo kiholelaholela kama hivyo unavyokwenda kukopa bila yeyote yule kujua. Na nina uhakika hata baba hajui kama unampango wa kukopea nyumba za kampuni.”

         “Usitufundishe jinsi tunavyoendesha mambo yetu mimi na baba yako. Tumefika hapa tulipo kwa kuaminiana.” Colins akacheka sana na kuongeza.  “Mambo yalikuwa yakienda kwa kuwa nyinyi, familia ya Simba, ndio mlikuwa mkinufaika na ukimya au kubali yaishe ya wazazi wangu. Sasa, narudia tena mzee Simba, mambo YAMEBADILIKA. Fuata utaratibu sahihi, utapelitapeli wenu, umefika mwisho. Uwe na siku njema.” Akamkatia simu, mzee asiamini.

~~~~~~~~~~~~~~~

         Akafurahia kumuwahi kabla. Inamaana angechelewa kidogo tu kuweka kikwazo kwenye mabenki, mzee angejishindia mkopo wa mamilioni ya pesa, ambayo hata asingelipa, inamaana kampuni ndio ingeingia hasara. Na hata kama hiyo pesa anayohangaikia hivyo kulipa dhamana ya Love, ingerudishwa na mahakama pindi kesi inapoisha, angeamua asiirudishe kwenye kampuni abaki nayo, pia hakuna ambaye angemuuliza wakabakia wao kina Simba kunufaika zaidi na zaidi. Akacheka kwa masikitiko.

         Akajipongeza kuwahi ila bado Chris akabaki tatizo. Anamtoaje katikati ya familia ya Simba ili asiwasaidie? Anampunguza vipi makali! Akaanza kusaka taarifa zake. Yeye ni nani! Anawasiliana na nani! Ana siri gani mbaya anayoweza kutumia kumpunguza nguvu! Yupo karibu na nani ili asije mgusa yeye na kutibua wakubwa wa nchi! Kazi ya kumsoma Chris ikaanza.

Subira Inapovuta Heri.

Mchungaji alikuwa na mshirika anayefanya kazi kitengo cha mifupa, kama dakatri huko. Akajitolea kumsaidia mama yake Emelda. Akawa ameshaanzishiwa matibabu. Alipigwa x-ray na kugundulika kuvunjika kwa mfupa wa mguu mpaka kwenye paja mara tatu. Na kwa kuwa hakuwa amefungwa, basi mifupa hiyo ikawa ikisuguana, mpaka imelika. Alihitajika kuwekewa vyuma ili kuunganisha mifupa hiyo. Junior akawa mstari wa mbele kufuatilia na kuhakikisha hilo linakaa sawa.

Wakazungumza na daktari kuomba awaambie kina Emelda kuwa huo upasuaji wa mama yao ungefanyika juma linalofuata. Ili kusudi tu huyo mama awepo kwenye kuvalishwa pete ya uchumba kwa mwanae japo hakuwa akijua mambo hayo. Naye daktari akawaambia kila kitu kipo sawa, akawapa siku ya jumanne. Hilo likawafurahisha sana kina Emelda. Kaka yake akajawa furaha na shukurani.

Ikabaki swala la maandalizi ya huko kuchumbiwa kwa Emelda ambako Junior alitaka msaada wa Jelini. Akamfuata kwao, akamkuta amelala. “Pona bwana Jelini, mbona hivyo!” Jelini akabaki kucheka. “Ugonjwa hauishi bwana! Nataka kuchumbia, na nataka msaada wako! Uniandalie kitu kizuri na cha pekee kwa Emelda. Amenisubiria sana. Nataka afurahi.” Mipango ikaanza.

Colins.

Kazi zikaanza kuwa ngumu. Kila wakati macho kwenye simu. “Si kawaida ya Kamila. Sasahivi angekuwa ameshawasiliana!” Gafla jumbe zikawa zikimuhusu yeye kuliko hata Mike mwenyewe! “Kuna kitu hakipo sawa. Kamila si wakuacha kuwasiliana.” Yaani tayari yeye akawa akimfahamu sana Kamila! Wasiwasi ukazidi.

Kwenye mida ya saa nane mchana akaamua aweke kila kitu pembeni aanze kufuatilia kujua kulikoni. Akapiga simu kwa sekretari kuwa asiruhusu mtu wala simu kuingia ofisini kwake mpaka atakapo mtaarifu.

Aliporidhika yupo peke yake, akatoa laptop yake. Kwa mara ya kwanza akaingia kwenye simu ya Kamila kuchunguza mara ya mwisho aliwasiliana na nani! Akakuta ujumbe aliomtumia usiku ndio ulikuwa wa mwisho ila kukawa na missed call kadhaa zimeingia kwenye simu yake. Hakuona kupokea kwake. Wasiwasi ukamzidi.

“Sijui anaishi na nani! Asije kuwa yupo peke yake, ameanguka, hakuna wa kumsaidia!” Akaendelea kuwaza akiendelea kupekua simu ya huyo mrembo kwenye laptop yake, akiwa amejawa wasiwasi vilivyo.

Mwishoe akaona aangalie kwa mara ya mwisho alikuwa wapi! Akijua ilipo hiyo simu ndipo na yeye atakuwepo. Akaingia kwenye location. Akaanza utundu wake akifuatilia GPS mpaka akampata na kushituka sana.

~~~~~~~~~~~~~~~

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment