Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! - PART 4 – SEHEMU YA 8. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! - PART 4 – SEHEMU YA 8.

Huku kwa kina Love hapakuwa na kulala wala jingine isipokuwa jinsi yakumtoa

Love rumande hata kwa dhamana ya namna gani. Chris alishinda mahakamani na polisi akihangaikia dhamana ya Love. Akafanikiwa kusikilizwa ombi lake la dhamana. Sasa kwa kuwa Colins alishamsambaza kila kona na hatari ya kuweza kukimbia nchini, basi hatimaye ilipofika jioni wakakubaliwa dhamana lakini kwa pesa nyingi sana.

Mzee Simba akaona si tatizo. Pesa yake, mkewe na hospitali! Akajua atafanikisha tu. Akamwambia Chris ampe muda mfupi tu, akusanye pesa, asijue Colins alishaliona hilo. Akatoka mahakamani hapo kwa haraka akimshangaza hata Chris! Kwamba pesa yoye hiyo atapata wapi kwa haraka hivyo! Lakini wakamwambia yeye akae tayari, pesa inakuja.

Bila ya kumwambia mwenzie, yaani baba yake Colins, mzee Komba, akakimbilia hospitalini, moja kwa moja kwa muhasibu akitaka saini yake tu, akiwa ameshaandika hundi ya kiasi cha pesa kilichobakia kukamilisha dhamana nzima. Yaani hapo ilikuwa akipata tu hiyo saini ya pili, basi anajishindia hayo mamilioni ya pesa bila shida.

Maana wawili hao, wamiliki kuu, mzee Simba na mzee Komba, ilikuwa wakiweza kuchukua pesa hapo, ilimradi tu wataarifiane na kupata saini ya pili ya muhasibu ambaye anatunza hesabu na kumbukumbu ya pesa zote hapo hospitalini.

Akashindwa kusubiria lifti kwa haraka. Akapanda ngazi akikimbia mpaka ofisini kwa muhasibu akihema kama anayetaka kutapika roho! Roho ya uzazi ikimsumbua asijali ngazi hizo, akitaka kumuokoa binti yake, asiyejua ametumbukia kwenye shimo alilotoka Colins, tena kwa kulichimba yeye mwenyewe akisaidiana na Kemi.

 “Nimeshaandika kila kitu, naomba tu saini yako.” Hakuweza hata kusalimia ili awahi benki kabla hazijafungwa kisha kulipia hiyo dhamana.

“Utaratibu umebadilishwa mzee wangu. Majibu yote ya swali lolote utayapata kwa kiongozi.” Mzee Simba akawa hajaelewa. “Kiongozi ni nani?! Mimi ndiye mmiliki hapa!” “Hata hilo swali nashauri ukazungumze naye Colins.” Mzee akatoka akikimbia mpaka ofisini kwa Colins.

Wakati Wakutafuta,Wakati Wakupoteza.

 Akanyanyua kichwa alipoingia kwa kasi bila hata hodi. “Nataka saini ya pili ili nikatoe pesa benki. Ni haraka tafadhali.” “Unakwenda benki kutoa pesa ya kampuni kwa matumizi gani?” “Nisikilize Colins. Sina muda wakujieleza kwako sasahivi, nina haraka.” “Nashauri utafute muda uzungumze vizuri. Hatuendeshi tena mambo kiholela.” “Yaani unataka nijieleze kwenye kampuni yangu?!” “Hii ni kampuni ya ubia mzee Simba. Si yako peke yako. Utaratibu umebadilishwa, ili kuzuia mambo kama haya. Huwezi kuchota pesa ya kampuni kwa matumizi yako binafsi.”

“Nani anabadili sheria ya hapa bila idhini yangu?!” “Wenye mamlaka makubwa dhidi yako.” Mzee akashangaa sana. “Hakuna mwenye mamlaka hapa dhidi yangu!” Colins akabaki akimtizama. “Sina muda wakupoteza Colins. Hivyo visasi vyenu mtalipizana wakati mwingine. Huu sio wakati wake. Love amefanikiwa kupata dhamana, inahitajika pesa.” “Nashauri matatizo ya kifamilia, mkamalize kifamilia. Hapa si sehemu yake. Michezo mliyokuwa mkicheza zamani, imebadilika. Sasahivi nipo kwenye kurekebisha matatizo ya hii hospitali. Ifanye kazi kifasaha ikitoa huduma nzuri kwa kila anayekuja hapa. Nina shida na pesa, na sina ya ziada. Kama huna la nyongeza tafadhali funga mlango nyuma yako, na siku nyingine acha kuingia ofisini kwangu kama chooni.” Mzee Simba hakuamini.

Hapohapo akampigia simu baba yake na kuweka simu kwenye spika kabisa ili na Colins asikie, akijua baba yake atamdhibiti kama walivyowazoea familia hiyo kufanya kila wanachotaka wao, asijue Colins ashawaweka sawa, mambo yamebadilika.

“Huyu kijana wako amechanganyikiwa?” Kimya upande wa pili. “Mimi nataka pesa ananizuia kuchukua pesa yangu!?” “Haijawahi kuwa pesa yako peke yako Simba! Hiyo ni pesa ya kampuni. Na usisahau lengo la kumuweka hapo Colins. Ilikuwa ni ili aendeshe hiyo kampuni vizuri tukiwa tumekubaliana pamoja kwa sababu sisi wote hatuna muda. Sasa nashauri uheshimu maamuzi yetu na uongozi wa Colins kwa sasa. Hapo mambo yamebadilika. Sio kama zamani kujichotea pesa utakavyo. Colins yule mliyekuwa mkimuona mjinga na kama ulivyomuita sasahivi kuwa amechanganyikiwa, basi jua ameweka utaratibu mzuri tu wakuendesha mambo.”

“Utaratibu huo ameidhinisha nani?!” Hapo anazungumza bado yupo ofisini kwa Colins na simu ipo kwenye spika. “Unasahau tu Simba kwa sababu yale tuliyokuwa tumekubaliana kwa pamoja, sasahivi Colins ndio ameamua kuyatekeleza. Lakini sisi wenyewe tulipanga na kumtaka Colins asimamie. Sasa pengine uniambie hukudhani kuwa anao huo uwezo.”

“Basi mimi leo nafuta kila kitu mpaka tutakapo panga upya.” “Huna mamlaka hiyo tena Simba. Huyo Colins ana ubia mkubwa hapo kutuzidi sisi wote. Kwa kukusaidia tu, yupo hapo akiwa na share zangu mimi kama mdau mkubwa, mke wangu, Connie na zake yeye mwenyewe Colins. Ukimuona amekaa hapo, ujue mbali ya kuwa ni kiongozi mkubwa hapo, ambaye tulimchagua sisi wenyewe, basi ujue ni mmiliki mwenye hisa kubwa kutuzidi sisi sote.” Hizo habari zikazidi kumchanganya Simba.

“Haiwezekani kabisa! Basi na mimi nazungumza kwa niaba ya familia yangu yote.” “Hamna shida kabisa. Kama nilivyotangulia kukwambia, mambo yamebadilika. Ule mtindo wa kuzungumza jambo kisha tunazungukana, umefika mwisho. Tunakwenda kisheria na kwa makaratasi. Muonyeshe uthibitisho wa hicho unachosema. Tukae kikao sisi wote kama wabia, tujipange kwa upya. Lakini hicho alichokwambia Colins jua kina baraka zangu na zako. Tulimtuma sisi wenyewe, aongoze hapo. Sasa NAKUONYA Simba, acha kumchanganya kijana wangu.” Mpaka Colins akashangaa.

“Unanisikia Simba?” “Umepatwa na nini Henry wewe?! Mbona tulikuwa tukienda vizuri tu, mimi na wewe?!” Alikuwa kwenye mshituko mpaka akamtaja jina la ujanani. “Tulikuwa tukienda vile unavyotaka wewe na mkeo, mkisaidiwa na binti yenu, tena kiholela holela tu, halafu mimi na mke wangu tukiwafuata nyuma kama kondoo! Mambo yamebadilika Simba, hilo lazima ulipokee. Tumejifunza kutoka kwenu. Kipimo kilekile mlichotupimia, ndio tunawapimia na nyinyi, sema hamjazoea hivyo ndio unashangazwa.”

 “Na hayo ni matokeo yetu sisi wote tuliyopanga mwanzoni kabisa. Ila hukujua kama ipo siku utavuna kwa sababu mlidhania Colins hana huo uwezo. Sasahivi anafanya kilekile tulichomtaka afanye tokea mwanzo, unarudi kinyumenyume! Hakika sitakuruhusu Simba. Unanielewa?!” Kimya Simba haamini kama Colins mwenyewe.

“Tofauti yetu na nyinyi, sisi hatuta kiuka makubaliano yetu na nyinyi. Na hatutajipinga. Hatuna hila, tutasimamia kila kitu kwa haki, tukiendelea kuamini uwezo wa Colins. Sasa nakuomba tafadhali mpishe afanye majukumu yake. Na siku nyingine omba kikao, sio kumvamia ofisini kwake. Si sawa kwa sababu hata wewe usingependa kufanyiwa hivyo. Na sitakuruhusu. Jioni njema.” Simu ikakatwa, Simba asiamini.

Colins akabaki akimtizama ila akiwa amefurahishwa sana na baba yake. “Mtatumiwa kalenda kuwataarifu kikao kitakachofuata cha wadau wote. Swali lolote ulilo nalo hata sasahivi hapo, litajibiwa kwenye kikao. Jioni njema.” Mzee akatoka haamini. Ila akiwa amenasa kwenye mtego aliokwisha tega Colins hata kabla Love hajakamatwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ila Chris akawa ameshaingia kwenye hasira ya Colins. “Huyu ameshakuwa tatizo.” Akawaza Colins akikumbuka jinsi alivyowasaidia Love na Kemi kwenye swala la kuweka sumu kwenye kinywaji cha Jelini. Mpaka hapo akajua wameshinda hiyo kesi kwa asilimia 70. Ni kiasi cha Chris kuongeza tu nguvu ya kisheria, washinde kabisa na kulipwa fidia huku yule mmiliki asiyekuwa na hatia yeyote kuingia yeye matatizoni zaidi kwani mpaka hapo alishafungiwa upande wa jiko na vinywaji. Ni kama kulibakia sehemu ya kulaza tu wateja kitu ambacho ni hasara kwake. Biashara ya jikoni na vinywaji ndio ilikuwa ikivutia wateja zaidi.

Haya, huyohuyo Chris amefanikiwa kupambana mahakamani, ndani ya masaa 24 kupata dhamana. Kwamba mzee akikamilisha tu pesa, Love atakuwa uraiani. Colins akaanza kumfikiria Chris na jinsi ya kumdhibiti. “Lazima kukata makali.” Akabaki akiwaza peke yake hapo ofisi mzee Simba akiwa ameshaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

‘Neno nakupenda pekee, ni kama halitoshelezi kuwakilisha vile ninavyojisikia kwako. Na nahofia unaweza usielewe vile ninavyo maanisha na kujisikia kwenye neno dogo tu kama hilo, tena ninalo lirudia kwako mara kwa mara. Lakini haijalishi ni mara ngapi nakwambia hivyo, tafadhali mpenzi usilichukulie tu kirahisi. Kwa sababu namaanisha kuwa wewe ni maisha yangu, kipenzi pekee wa moyo wangu. Nakupenda sasa zaidi ya nilivyokupenda kabla. Daima utabakia kwenye moyo wangu.’ Huo ujumbe tena ulioingia kwenye hiyo simu mpya ndio ukahitimisha siku ya kazi kwa Colins.

Hata hivyo ilishakuwa saa tatu usiku. Yupo peke yake kwenye gorofa hilo. Alitoka tena kuzungukia hilo eneo zima la hospitali, ndipo akarudi na kuanza kuandika mapungufu aliyokutana nayo. Akaanza kuweka mikakati mpaka huo ujumbe ukaingia.

Akabaki akijiuliza sasa. “Huyu msichana, ni kwa nini hachoki kutuma jumbe zote hizi zisizopata majibu?!” Akajiuliza na kuanza kufikiria anaye muandikia. “Pengine ni mume wa mtu, amemtumia huyu binti kisha kubadili namba?!” Akawaza. “Naye atakuwa msichana wa namna gani asiyechoka!” Akajiuliza ila akavutiwa na subira yake kwa huyo ampendaye.

“Ni wasichana wachache sana wanaweza kumsubiria mtu kwa muda mrefu hivi tena bila kuchoka!” Akaendelea kuwaza huku akirudia jumbe zake. Akaona aanze kumsaka aliyekuwa na hiyo namba ya simu kabla yake. Akatoa laptop yake iliyojaa siri humo, si rahisi mtu kufikiri mambo yaliyojaza hiyo kompyuta. Hakuna kona anataka kufikia akashindwa. Akishika hiyo laptop yake, ni kama ameshika ulimwengu kwenye mkono wake.

Akaanza kusaka. Akakuta imeshamilikiwa na watu wawili, kwani ilikuwa na namba nzuri sana na rahisi kukariri. Akamtafuta mtu wa mwisho kuwa nayo. Maana alijua huyo ndiye muhusika mwenyewe. Akavuta jina kamili, kisha akahamia kwenye mitandao ya kijamii ili kuweka sura kwenye jina kamili.

~~~~~~~~~~~~~~~

Colins atamfanya nini Chris anayefanikiwa kutegua mitego yake!?

Familia ya Simba Imeanza kuangukia kwenye mitego ya Colins. Itakuaje?

Je, Colins atafanikiwa kuweka sura sahihi kwenye jumbe hizo za mapenzi? Kwa nini Colins? Upo Mtego KWENYE namba hiyo mpya?

INAENDELEA.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment