Akabaki na wasiwasi hajui kama ndio akaribie ndani au
ndio anatakiwa kuondoka! Akabakia mlangoni hajui chakufanya. Akageuka baada ya
kuweka mezani. “Njoo ukae hapa. Kuna kitu nilikuwa namalizia kufanya.” Akaenda
kukaa pembeni yake akamuona anaandika kwenye laptop yake amezama kwa muda kisha
akaifunga na kuanza kula.
“Pole kwa majukumu Colins, na asante kuwahi kurudi kuwa
na mimi. Najua una mambo mengi.” Akacheka akimtizama.
“Usijali. Najua siku ya leo ni ngumu kwako. Sikutaka kukuacha peke yako muda mrefu.” “Nashukuru.”
Wakatulia akila.
“Vipi lakini kazini?” “Safi tu.” Alitegemea. Akamkumbuka
mama yake. Akajaribu kumfanya azungumze zaidi.
“Ndio unakua busy kuanzia unaingia asubuhi mpaka usiku?”
“Tena wakati mwingine inanilazimu tu kutoka, lakini pale majukumu hayaishi. Ni
hospitali. Wagonjwa ni masaa 24. Na kila anayekuja pale anataka huduma nzuri na kwa haraka. Awe amefika pale
asubuhi au usiku wa saa nane, atataka huduma nzuri. Inamaana anatarajia
kukutana na muhudumu aliye tayari kumuhudumia. Bila mtu wa kuhakikisha hayo yanatokea,
ujue hakuna atakayefanya kwa kujituma.”
“Kwa hiyo wewe ndio unahakikisha wanafanya?” “Kwa
asilimia 80. Ndiyo.” “Unafanyaje?” “Kwanza kuhakikisha juhudi zao zinaendana na ninachowalipa.
Inamaana kama nawalipa vizuri,
nataka kuona matokeo mazuri. Nafuatilia kwa kila namna. Viongozi wao, kamera
zinazonionyesha jinsi wanavyofanya kazi na kuhudumia kila mgonjwa, na wakati
mwingine na mimi nakuwa nao pale mapokezi ambapo ni kioo cha hospitali nzima.”
“Haya, kuweka sawa madaktari wanaowahudumia. Malipo yao
kwa wakati na kuweka mazingira rafiki kwao na mengine mengi ilimradi tu
kuhakikisha kila mmoja anafanya chake kwa makini na vizuri. Hakuna mwenye kazi
ndogo ambaye simuhitaji. Kila mtu nataka afanye kazi yake vizuri, kwa wakati na
kifasaha. Wote nawahitaji na kuwathamini.” Akashangaa kweli anamuelezea kwa
kirefu, kitu ambacho hakuwahi kukifanya hata kwa Mike.
Alikuwa akishaulizia tu za kazini, akiambiwa nzuri. Basi. Hakujua kama nyuma ya nzuri
kunakuwa na mengi ya kiasi hicho! Akamsikiliza akizingatia akiuliza hapa na
pale.
“Kumbe ndio una mambo mengi hivyo!” Colins akacheka tu.
“Niambie jinsi ya kukusaidia.”
Colins hakutegemea. “Kweli tena. Kwa namna yeyote ile, wewe niambie tu. Naweza
nisiwe msaada mkubwa sana kwa kuwa sijasoma sana, lakini hata kwa kidogo
sio mbaya. Naweza saidia.” “Nashukuru kujali. Na shule sio kila kitu
kinahitajika pale. Utayari wako na hata hicho unachofanya sasahivi ni msaada mkubwa sana. Na ulipo, namshukuru
Mungu mzee Yusuf, mumeo amepawezea.”
Kamila alicheka sana.
“Kwa hiyo ofisi ya familia ipo vizuri?” “Pale sina shida.
Na hivi na wewe umeongeza nguvu! Basi ni msaada zaidi.” “Ila kukiwa na kitu
kingine unahitaji msaada, utaniambia?” Colins akacheka.
“Kumbe unamanisha?!” “Sina ninapokwenda Colins.
Nipo hapa na wewe.” “Una uhakika? Maana uliniambia unampango wa kununua nyumba
yako.” “Kabla hujanipa familia. Shida yangu ni hiki ulichonipa. Hakuna pesa
inanunua familia yenye mama kama mama yako na nyumba tulivu hivi. Mama yako
ameniambia naweza baki hata mpaka wanioze.” Colins akacheka.
“Siondoki Colins. Mimi nipo.” Akabaki akimwangalia kama
anayetafuta uhakika kutoka usoni kwake. “Siondoki. Hata hivyo niondoke niende
wapi?” “Sijui Kamila!” “Nitabaki na wewe Colins.” Akaiongea kwa kuibembeleza
na upendo mkubwa lakini ikamuia ngumu kwa Colins kuiingiza
moyoni.
“Sasahivi upo kwenye kipindi kigumu, Kamila. Unaweza sema
na kuahidi chochote. Tafadhali pata muda wa kupokea taarifa za leo
kwanza. Zikubali. Ziombolezee kwa namna yako. Kisha chukua hatua baada
ya hapo kabla hujanipa ahadi yeyote ile.” “Namaanisha Colins!” “Hapana.
Tafadhali pata muda kwanza. Ni mapema sana kutoa ahadi yeyote. Tafadhali
Kamila.” Akasimama kabisa na kuondoka hapo walipokuwa wamekaa.
“Tafadhali usiniahidi chochote kwa sasa. Tuache iwe kama ilivyo.”
Akamuona amebadilika kabisa. “Colins mimi ndio mbaya wa kiasi hicho!?” “Hapana
Kamila. Na naongea hivi kwa heshima
kabisa. Wewe ni msichana mzuri sana. Mwanaume yeyote yule atabahatika kuwa na
wewe.” “Lakini sio wewe!?” Akauliza kwa uchungu sana akijihisi
kukataliwa waziwazi.
“Kamila! Ninachoomba ni uchukue muda, tafadhali.” Hapo
amesimama kabisa. “Nakuelewa Colins.” “Tafadhali iwe umenielewa vizuri. Sio kwa
ubaya. Na si kwa upande wako tu. Mimi mwenyewe nina mambo mengi sana
yanayo endelea kwenye maisha yangu. Nahitaji kujipanga kabla sijaanzisha jambo
jingine. Kwa hiyo mimi mwenyewe nahitaji muda.” “Sikuwa na nia mbaya na
samahani kama nimevuka mpaka.” Akabaki kimya.
Kamila alipoona vile akachukua vyombo. Colins akiwa
amesimama kama anayefikiria. “Acha nikuache upumzike.” Kabla hajatoka akamuwahi
akiwa anahofia uwezekano wa kuja kuishia kwake. Asije akamkataa
kama alivyoanza na Jelini, akaishia kumpenda ila kumuacha moyoni na mwanzo
mbaya ambao alishindwa kuja kubadilisha kwa Jelini mpaka mwisho wao akaishia
kujua Love ndiye aliyependwa zaidi.
Akaamua kujirudi. “Kamila?” Akageuka. “Nimekuja na movie
nzuri. Utazipenda.” Kamila akacheka kwa utulivu na kuinama kama na yeye anayejishauri.
“Nitakusubiri mpaka ulale?” “Sitaki kuwa mzigo
kwako Colins. Sipendi niwe hivyo.” “Na sivyo ulivyo kwangu.” Akanyamaza
akiwa amesimama hapo na vyombo vyake kama anayemkatalia. Hataki tena. “Kamila?”
“Jana
ulinikatalia Colins. Ulinikatalia nikiwa nakuhitaji.” Mrembo akaanza kulia taratibu.
“Nisikilize Kamila. Nilifanya kwa nia nzuri tu, ila si kukukatalia.
Sikutaka kukuchanganya au kujichanganya. Njoo.” Akamsogelea yeye mwenyewe na
kumpokea vyombo na kuvirudisha mezani.
Akamsaidia kujifuta machozi kabisa. “Tafadhali naomba
unielewe Kamila. Sitaki kukuchanganya zaidi.” “Mimi sijachanganyikiwa
Colins.” “Naelewa. Lakini bado Mike alikuwa kwenye picha. Au niseme bado yupo
kwenye picha. Na mimi vilevile. Bado nipo kwenye kumsaidia Jelini. Nimemuingiza
matatizoni, hivi leo alikuwa mahakamani, akilipa garama ya uzembe
wangu.” Kidogo Kamila akashangaa.
Akamuelezea mkasa wa kuwekewa sumu kwenye chakula. “Lakini
si makosa yako Colins!?” “Siwezi kuepuka kujilaumu Kamila! Mimi ndiye niliye lazimishia
ile miahadi. Jelini alishatulia na mchumba wake. Nikalazimishia hiyo miahadi.
Ni kama nilimtoa mafichoni, sehemu salama na kumrudisha tena kwa watesi
wangu ambao wanajua wazi, kumgusa Jelini ndio kunikomoa mimi kwa
upande mwingine.”
“Kilichompata Mike, ndicho kilimpata Jelini lakini yeye aliwahiwa.”
“Roho inaniuma ukiniambia hivyo! Naona kama nilizembea! Pengine na mimi
ningemuokoa Mike!” “Sasa kwa upande fulani, ya Mike na Jelini ni tofauti
kidogo. Yeye alijua mapema sana kama alipewa sumu kwa sababu ya yale
mazingira na wale walishakuwa maadui zetu, akawaona.”
“Moja kwa moja hali ilipobadilika, akajua itakua
ni sumu tu. Lakini kama sihivyo asingejua. Wewe hukujua mpaka hivi leo ndio
umejua kama alinyweshwa sumu. Ulichukua hatua ya haraka kumuokoa, ila tu
wote, hata wauguzi pia, hamkujua ni nini kimempata kwa hakika. Tafadhali
usijilaumu.” Hapo akawa anambembeleza kwa kujirudi kwelikweli.
“Kwa hiyo nipo kwenye wakati mgumu, wala wewe hauusiki
kabisa. Ingekuwa ni wakati mwingine, mazingira mengine, ingekua tofauti. Huna tatizo
lolote lile, ila mimi nina mambo mengi, sitaki kukuchanganya. Natamani kumsaidia
Jelini mpaka nihakikishe nimemtoa kabisa matatizoni ndipo nitatulia.”
“Ndio unafanyaje?” “Hata mimi sina mipango ya kueleweka
ndio maana sitaki kukuchanganya hapo katikati. Najiona mimi mwenyewe sijatulia,
siwezi kukuongeza na wewe kwenye hiyo hali. Sijui kama unanielewa?” “Nimeelewa
kwamba sasahivi kichwa chako kimejaa Jelini, huna nafasi ya mtu mwingine.”
Colins akafikiria kidogo. Akaona akubali tu. “Ila naomba usiumie.
Ila upo sahihi.” “Siwezi kuumia kwa sababu nimemkuta kwenye maisha yako. Na
nashukuru kuwa muwazi kwangu.” Akatulia akitamani kurekebisha asieleweke
vibaya, ila akashindwa. Hakujua atafanyaje kwa kuwa ni kweli bado Jelini
yupo kwenye picha.
“Ila nataka ujue, usije nielewa vibaya ukadhani nakutega.
Ni kweli mimi huwa naogopa usiku. Naogopa sana, na sijui ni kwa nini! Giza na mimi hatuna urafiki kabisa. Mpaka
nataka kumuomba mama, pengine niwe nalala na msichana wake wa kazi.”
“Hapana. Naomba
nichukue mimi hilo jukumu, tafadhali. Naomba nijirudi. Siwezi kushindwa
kukufanya wewe ukaweza kulala.” Kamila moyo wake mwepesi, hajui kuweka jambo,
akasahau yote, dhambi zote akasamehe, akajawa na furaha ya namna yake.
“Eti Kamila! Na utayari wote huo wa kutaka kunisaidia,
halafu eti mimi nishindwe kukufanya ukalala tu!” Akacheka kwa deko,
furaha yote moyoni. Angalau safari hii tena, Colins
akaweza kujirudi kwa haraka. Akawa ameshajua si ngumu kumridhisha Kamila.
“Kila siku usiku nitahakikisha unalala. Kwa njia gani, sijui.
Tuanze leo tutaona inaendaje.” “Asante Colins. Nashukuru kujali. Ndio maana
mwenzio nilikuwa naogopa, namlilia Mike. Alikuwa akinifaa kweli mida ya
usiku.” “Basi hilo limekaa sawa. Mengine taratibu, Mungu atakufungulia mlango.
Naomba jipe muda. Nataka kukuona na furaha, na ndio maana sitaki ukwame
kwangu. Unanielewa?” Hilo ni kama alilisisitiza sana Colins, ila ni kama
Kamila alichelewa kuliingiza akilini.
“Nahisi ni kama nimekuelewa.
Ila nilijua umenikataa tu! Kama vile mimi sio type yako.” Colins
akacheka bila ya kumjibu ndio au hapana ila akaongeza. “Utakua
sawa Kamila. Kwanza huna shida. Mnyenyekevu. Unaridhishwa na mambo madogo
madogo!” “Na Mike alikuwa akiniambia hivyohivyo.” “Unaona! Kumbe sijakosea.”
“Chakula.” Wakasikia sauti ya msichana wa kazi nje ya mlango. Wakatoka.
Wakati wa Kujenga.
Wakajikuta mezani, safari hii kama familia kweli. Mpaka
mzee na msichana wa kazi walikuwepo mezani. Kimya kwa muda maana wakati wote
Colins alikuwa kama akila mezani, basi wao hawapo, vinginevyo alikuwa akilia
chumbani kwake.
“Unaendeleaje Kamila?” Mzee akavunja ukimya. “Naendelea
vizuri. Nashukuru kunisindikiza.” “Utakuwa sawa mama. Weka akili kwenye kazi
hiyo unayoipenda. Utashangaa mawazo yanaanza kukaa vizuri. Hofu inapungua
taratibu.” “Asante. Nitajitahi kazini. Na nashukuru mmenikaribisha hapa. Sipo
tena peke yangu.”
“Nimesikia unapenda kupika.” Wakashangaa mzee anaendeleza
mazungumzo na si kawaida yake. “Napenda sana kupika japo na mimi sijasoma sana.
Ila nilisomea mapishi nikiwa tayari ni kitu ninachokipenda.” Akajihami, maana alisikia Jelini alikataliwa hapo sababu ya shule ndogo.
“Sasa hivi nikifikiria kusoma tena, sio kwamba nakataa, ila sijui sasa kama nikisoma
nitafanya nini!” Akaongea kwa hofu kidogo akimtizama Colins. Kimya kidogo wote
wakijua anachozungumzia.
“Watu wengi waliobahatika kurudi shule, hufanya kwa ajili
ya kuendeleza ujuzi au kutafuta ujuzi. Sasa maadamu wewe
umeshapata kitu unachokipenda, na unakiwezea, sidhani kama kuna sababu ya
kurudi tena shule. Iwe kupenda kwako na kuwe na sababu ya kutafuta ujuzi
zaidi.” Kidogo pakawa kama kuna amani.
“Nashukuru.” “Nimesikia umepata mchumba huko kazini.” Alicheka
Kamila, mpaka wote wakacheka. “Sasa mwambie mzee Yusuf nataka mahari yangu.”
“Amejipanga huyo! Amesema hivi.” Kila mtu akawa akimwangalia anaongea na
kucheka, kama mazuri.
“Amesema yeye akimfukuza mama Hiza, Mungu atamlaani.
Kwa hiyo anamtoa mjini kwa mahesabu. Anamwambia warudi kijijjni,
wakamalizie huko maisha. Mama Hiza akikubali, basi anamwambia yeye atangulie.
Akishatangulia, huku nyuma anauza nyumba, anakuja lipa mahari.”
Walicheka hapo, mpaka basi.
“Kumbe mipango imekamilika!” “Amesema yeye lazima
atanioa.” Akajibu mwenyewe cheko lote. “Kwa hiyo atakuficha huku mjini?” Mama
Colins akachomekea kwenye mazungumzo ya Kamila na mumewe.
“Ujue mama, mzee Yusuf kajipanga?” “Eeh?” Mama Colins
akaitikia kishabiki. “Sisi tunamuhisi Dula anatuonea wivu, sababu yeye
ndio anakazi yakuweka vipingamizi. Akasema kwa jinsi anavyomjua mama
Hiza, ni kama anazungumza na Mungu ana kwa ana, atajua tu.” Wote
hawana mbavu.
“Sasa mzee Yusuf akamwambia wala hatakuwa Mungu ni yeye
tu mchonganishi wetu ndiye atakaye mpelekea maneno mama Hiza. Lakini
Mzee Yusuf amesema akishanioa tu, atanipeleka kwa mama Hiza, nikamsalimie.
Eti mama Hiza akiniona tu, yaani yeye mwenyewe ataanza kumgombesha kwa
nini amechelewa kunioa.” Walicheka hapo, mbavu hawana.
“Sasa, mimi si kama Dula, ila nina swali. Akikuoa,
na nyumba kauza, mtakwenda kuishi wapi!?” Wakamuona ametulia.
Wote wanamwangalia na cheko. “Mimi huko sijafikiria baba yangu. Sasa
nitakachomwambia, namwambia baba yangu anakuita. Ili umuulize maswali
vizuri.” “Mwishoe na wewe atakurudisha kijijini.” “Umeona mama yangu! Mimi naona
huyu mkwe aje hapahapa mumuulize maswali vizuri.” Colins alikuwa
akimwangalia akicheka haamini.
Wakati Wakuvuna Ulicho Panda.
Wakiwa kwenye ile hali ya furaha wakasikia mageti
yanafunguliwa, gari linaingia. Kwa kutoulizwa kama wafungue geti, wakajua huyo
ni mgeni mwenyeji. Wakaangaliana.
Hawajakaa sawa, hodi mlangoni. Mzee akasimama kwenda kufungua. Kimya mlangoni akiwa
ameshafungua mlango, mpaka wa ndani wakashangaa ni nani hao mlangoni mbona hawakaribishwi
ndani!?
~~~~~~~~~~~~~~~
Colins anacheza mchezo hatari na yeye anajua, ila
hawezi kujisaidia. Anamng’ata na kumpuliza Kamila
atakavyo, huku mawazo na moyo vimebaki kwa Jelini. Hofu ya kukosa kotekote ipo, ila hawezi
kuachia aliposhikilia kwa Jelini.
Mwisho wake ni nini?
Kina nani wapo mlangoni?
INAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment