“Kwa nini tusikae tukazungumza?” Wakasikia sauti ya mama
Simba. “Ukiwa kule kazini, wewe ni kiongozi wa mke wangu. Ndio maana
nimekuacha umnyanyase mke wangu vile utakavyo wewe. Lakini hapa,
ni kwake. Na usiku huu aliotulia, huruhusiwi kuingia humu na kumtibua
zaidi. Na nitahakikisha ile tabia yako yakumpelekesha mke wangu inafika mwisho.
Unanielewa mama Simba?” Kabla hajajibu akaongeza.
“Ukifika hapa, wewe hutatoa amri tena, ila mama
Colins. Ila ukiwa kazini, mchafue yeye na kijana wake utakavyo. Mnyanyase
na kutuma mabosi zake wampangie kazi kana kwamba ndio anaanza kazi jana,
wakati ulimkuta kazini.” “Watu wanataka kutuchonganisha shemeji.” “Usinifanye
mimi mtoto mdogo. Anayesambaza habari za ndani kabisa juu ya familia
yangu, ni nani kama sio wewe mtu tuliyekuwa naye karibu?” Kabla hajajibu
akaongeza.
“Unamuanika mke wangu na kijana wangu kwa habari unazotengeneza
wewe na binti yako!? Unamtangaza mke wangu mvivu, umetengeneza ushoga na
mabosi zake wamfanyishe kazi kama punda! Tangia anaingia kazini mpaka mke wangu
anatoka, nasikia mnamfanyisha kazi kwa makusudi wakati watoto wadogo walioanza
kazi juzi tu, wamekaa wanamtizama! Halafu eti leo mnakuja nyumbani kwangu mkiwa
nyinyi mnashida!”
“Halafu kingine, hivi mlikuwa wapi wakati namuuguza
kijana wangu? Eti Simba? Si mimi niliyekuwa nikikuulizia habari za Colins, nakwambia sijamsikia muda mrefu, unanipa majibu
ya uongo?” Kabla hajajibu akaongeza. “Mara ya mwisho nilikufuata ofisini
kwako nikakwambia kabisa, nina wasiwasi na Colins, hatujamsikia kwa muda mrefu.
Unakumbuka jibu lako?” Kabla hajajibu akaongeza.
“Uliniambia mlimuunganisha na hospitali moja huko nchini
India, amekwenda kujifunza jinsi wanavyoongoza mambo huko, ili ahamishie
hapa. Nikakuuliza kwa kukuamini kabisa, itachukua muda gani, ukanijibu
unashauri tumpe nafasi. Akirudi atatutafuta. Nikiamini tupo upande
mmoja. Huwezi kunidanganya, nikawa na subira. Kumbe kijana wangu
anatembea mtaani ni kichaa kabisa, tahira hajitambui!” “Na mimi
ndivyo nilivyokuwa nikijibiwa.”
“Na siku niliposhinda Kigamboni, nikimtafuta mpaka usiku,
nikimsihi Love japo anielekeze alipo, nikamtafute mwenyewe. Binti yako akanidanganya,
lakini nikashindwa kuondoka mpaka walipomrudisha kijana wangu wamemfunga kamba
kama kondoo anayepelekwa machinjioni! Namuuliza binti yako kwa heshima
tu, wewe unaingia kwenye simu na kunifoka mbele ya binti yako
akikusikiliza!”
“Ukanifoka bila heshima ukijua nalilia hali ya
mwanangu! Mtu mliyeniambia yupo nchini India, leo ni kichaa, tahira,
mnamfunga na kamba na kumburuza kama mnyama, tena mnyama asiye na
thamani kabisa! Kana kwamba haitoshi, wewe na familia yako, mkijua hali
yake mpaka nakuja kumchukua, msipige simu hata siku moja kuulizia hali
yake! Wala sijawaona mkija hapa kumuona kwa ugonjwa mlio msababishia
nyinyi wenyewe!” Mzee Simba akashangaa sana.
“Henry umekasirika, ila shutuma unazotupa si kweli.”
“Muulize mkeo kichaa alichokipata mwanangu kilitokana na nini kama si binti
yako, Love kumtafutia mwanangu mganga wa kienyeji, aliyemloga.”
“Haiwezekani!” Aakahamaki.
“Mimi niliambiwa…” “Sasa nimekwambia ukweli ulivyo,
kachunguze mwenyewe. Lakini hata hivyo, wewe unayesema tumetoka mbali, ungali
ukijua kijana wangu ni mgonjwa, mbona usiniulizie hata mara moja hali
yake?” Kimya.
“Mmemchezea mwanangu mpaka mmemfanya kichaa,
halafu mkamuacha anamangamanga mtaani huku mkituficha! Kilichowashinda
kutuambia tukaja kumchukua sisi wenyewe ni nini? Mngepungua wapi kututaarifu tu
kwamba kijana wetu ni mgonjwa, hamuwezi au hamtaki kumsaidia. Lakini
mkafanya kinyume kabisa, mmemficha kisha mkageuza mioyo ya wafanyakazi
wote wadanganye alipo.”
“Mke wangu kazi zinamshinda sababu ya kumtafuta,
usivyo na ubinadamu wewe mama Simba, eti unarudi kumtangaza ni mvivu
kama kijana wake, hawapendi kazi, huku ukijua fika, anahangaika
kumtafuta Colins!”
“Mkanyamazia hilo. Mke wangu anateseka
kazini, kijana wangu anateseka mtaani, nyinyi yenu yanaendelea tu. Leo
mmetuona tumenyamaza, mnakuja nyumbani kwetu kuanza fujo zenu.” “Si fujo
Henry, tunaomba msaada.”
“Leo ndio mnaona sisi ni watu wa kuwasaidia kweli!? Mke
mvivu, kijana mvivu. Hawajasoma kama nyinyi, hawapendi kazi kama nyinyi. Msaada
huo kwa nyinyi mliofanikiwa, sisi tutaweza wapi? Kama si kutaka kunivurugia
usiku wangu na mke wangu?”
“Basi kama msaada umeshindikana, na mahusiano yamekufa
kati yetu, tupeni sehemu ya mali yetu tutumie tutakavyo.” Hapo
Colins akasimama. “Mama wewe tulia tu hapa.” Mama Colins kimya.
Colins akasogea mlangoni. “Mnaposema sehemu ya mali
yenu, mnamaanisha nini?” “Kwa kuanzia sisi tunataka kuuza ile nyumba ya
Kigamboni, tupate pesa, tuitumie kwa dhamana ya Love.” “Sisi kina
Komba, hatutaki kuuza.” Akajibu Colins akiwa ameshabadilika tokea
alipokuwa akiwasikiliza mazungumzo yao na baba yake hapo mlangoni.
Ndio kwa mara ya kwanza anasikia juhudi zilizofanyika kumsaka.
Hakuwahi kukaa na baba yake kuzungumza, ndio anasikia hapo. “Sasa sijui
itakuaje! Maana kama mmeshindwa kutusaidia, au kuzungumza kifamilia, sisi tupo
tayari kwenda mahakamani. Kuomba mahakama itusaidie kuiuza, tugawane.”
“Haiwezekani Simba.” “Subiri kwanza baba.” Colins akamtuliza baba yake.
“Kwa uharaka mlio nao, mnataka ile nyumba iuzwe kwa kiasi
gani ndipo sisi watano tugawane?” “Unamaanisha nini mkisema watano?!”
Mama Simba akahamaki.
“Kwa sababu Loreta hana ubia kwenye sehemu yeyote kwenye
ile kampuni. Aliniuzia share zake zote.” “Haiwezekani!” Wote
wakashangaa mpaka wazazi wake mwenyewe huyo Colins.
“Kwani hakuwaambia kama aliniuzia mimi? Tena kwa kunifuata
yeye mwenyewe ofisini kwangu! Kila kitu kipo kisheria kabisa, mpigieni simu
mumuulize. Na mnaruhusiwa kwenda kufikiria bei ya ile nyumba, mkirudi na pesa
inayoeleweka, sisi tutanunua sehemu yenu, tuwape pesa yenu hapohapo bila ya
kuchelewa, tuachane kwa upande wa ile nyumba.” Wakawa wamepata habari nyingi
kwa wakati mmoja.
Loreta,
kisha kuna uwezekano wa kupata pesa kwa haraka. Shida yao kubwa na ya
haraka ni kumtoa Love lumande. Kesi ya Loreta ikaanza kutokuwa na
umuhimu sana ila wakataka kuthibitisha wakiwa hawaamini. “Ngoja nimuite Loreta,
tukae tuzungumze.” “Sio hapa.” Colins akamuwahi mama Simba.
“Mzee ameshakwambia. Ukiwa kazini, kule, wewe ndio
bosi wa mama. Hapa, mwenye kauli ya mwisho ni mama ambaye unamdharau. Ule ubabe wako na ushauri uliokuwa ukiutoa
zamani ukitumia vibaya wema na upole wa mama yangu, umefika mwisho. Mlishaua undugu hapa.
Kwa hiyo vikao vyenu, kafanyieni kwenu.”
“Sasa kama tumeshafikia muafaka, mnataka tuendelee
kuzungumzia hapahapa mlangoni! Na mbu?” “Kwani mbu mlikuja nao nyinyi kwamba mnahofia
mbu wenu wataingia kwetu, halafu watagoma kurudi kwenu!?” Colins
akawauliza kwa kuwashangaa kabisa.
“Mbu mmewakuta hapahapa kwetu, mnawasiwasi gani
nao?” “Sawa, acha tumuite Loreta.” “Wakati mnamsubiria, tunaomba tufunge
mlango. Kafanyeni kikao chenu huko, mkirudi hapa mje na bei, tumalizane.
Haya, usiku mwema.” “Si umesema turudi!?” “Msiporudi je?” Colins akamuuliza
mama Simba. Kimya. Akafunga mlango na kuwaacha wamesimama nje wasiamini.
Ukitaka Kuruka, Agana Na Nyonga.
Hawakurudi tena mezani pale walipomuacha mama Colins,
dada wa kazi na Kamila. Wakakaa sebuleni wakisubiria. Msichana wa kazi akaanza
kutoa vyombo taratibu, Kamila akaona na yeye asaidie.
“Sasa wakija wanataka pesa kubwa, utakuwa nayo?” Baba
yake akamuuliza kwa sauti ya chini. “Usiwe na wasiwasi baba. Nimejipanga.
Hizi siku niliziona nikiwa najiuguza hapo chumbani, wakiwa wamenitelekeza.
Niliziona na nimejipanga. Hichi wanachokifanya nilikitarajia kabisa ndio
maana nimejiweka tayari.”
“Na kama si kumdhibiti huyo rafiki yako mliye toka naye
mbali, asingekuja hapa. Maana alishazoea kuchota pesa kule
hospitalini, wewe na mama hamna habari. Nimemdhibiti kule, nikijua atarudi
tu hapa, niwatoe kwenye maisha yetu kihalali. Kama mnataka kuwa
marafiki, iwe urafiki wa kawaida si mpaka mali.” Mzee akamtizama Colins
asiamini.
“Kwamba ndio umejipanga kwa kiasi hicho!?” “Kuishi nao
hawa, nimejifunza mengi sana. Wadhulumishi
sana.” “Na mkewe huyu ni mnyanyasaji
kupita kiasi.” “Kama binti yake.” Wakaendelea kuzungumza hapo wao wawili, mama
Colins kimya hapo mezani.
Ufalme Umeshagawanyika.
Wakasikia huko nje wakimgombesha Loreta. “Ulifanyia nini
pesa zote hizo?!” “Baadhi si ndio nimewapa kama mchango wangu wa kumtoa
Love! Sasa mlitaka nijimalize kabisa kwa ajili yake! Halafu mimi ndio niishiwe,
mzidi kuniona mjinga, muendelee kumuona yeye ndio mwenye akili?” Wakamsikia
na yeye Loreta anawajia juu.
“Akifanya yeye jambo, mnamuona anaakili.
Hata sasa anashitakiwa kwa kosa la wizi, lakini pia mnahangaika kuuza
mali zote ili mumtoe yeye! Mmeshafikiria baada ya yote inakuaje?”
“Kwa hiyo wewe unaona sawa vile dada yako alivyo mgonjwa na yupo mahabusu?”
“Mwache twende tukamalizane nao hawa, tuondoke hapa. Sitaki kudhalilishwa
zaidi.” Wakawasikia wakirudi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Hodi tena. Wakasimama wote na kuwafungulia. “Tumefikia
muafaka. Tunauza sehemu yetu kwa..” Wakawatajia. Colins akaanza kucheka.
“Kwamba ile nyumba ina thamani kama hiyo, halafu ongeza na ya kwetu sisi wanne!?”
“Kabisa.” “Basi pelekeni mahakamani. Mahakama iuze, muone mtapata kwa
kiasi gani. Na kama hamuamini, mpigieni simu yule mwanasheria wenu, muulizeni
mahakama inapouza nyumba huwa inauza kwa faida au hasara. Na mjue
sisi tutainunua tu. Muwe mnauza nyinyi au mahakama, sisi kina
Komba, tutainunua. Haya, usiku mwema. Sisi tunakwenda kulala.”
“Mbona hatujamaliza?!” “Naona mnaendeleza ile tabia yenu
ya dhuluma. Mnakuja mpaka kwetu kutudhulumu! Hamuoni aibu?”
“Basi…” “Hapana mzee Simba. Nendeni mkafikirie vizuri. Njooni kesho na
mwanasheria wenu, na barua mliyoeleza mnatuuzia sisi sehemu ya ile
nyumba. Kwa kiasi kinachoeleweka. Iwe na saini zenu nyinyi wote watatu, ikiwemo
na ya Love. Maana asije toka na kuanza na yeye habari nyingine za kurukana.”
“Mkishakamilisha hilo, na tukipokea hiyo barua yenu kwa
utaratibu sahihi, mbele ya mwanasheria wenu, tutawalipa kesho hiyohiyo. Haya, usiku mwema.” Akafunga mlango kabisa, mzee
Komba akijivunia kijana wake.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Twende tukalale.” Akamsikia mzee akimwambia mkewe
aliyekuwa amebaki mezani peke yake wao wanasaidiana kusafisha jikoni. “Twende.”
Akamsikia mzee akiongeza kwa kubembeleza. Kimya. “Upo sawa mama?” Akamsikia na
Colins akimuuliza kwa kujali. “Nipo sawa. Acha nikampumzike.”
“Punguza mawazo. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Unajua mimi
sipendi vurugu, Colins. Huwa navurugukiwa kabisa. Hivi mimi siwezi
mwenzenu.” Akamsikia akiongea kwa sauti yake ya upole, kama alivyo. “Basi mama.
Kelele humu ndani zitaisha. Na wao nitawaambia tuwe tunamalizana hukohuko
wasiwe wanakuja hapa.”
Hisia Zilizoshindwa Kufichika.
Kamila akaona ajirudie tu chumbani kwake. Mengi yalizungumzwa
usiku huo. Na kwa jinsi alivyomuona Colins akibadilika pale mezani kadiri
habari zake zilivyokuwa zikizidi kuzungumzwa kati ya baba yake na wageni
waliofika usiku huo, akajua usiku huo ahadi ya kusubiriwa kulala ndio imeisha.
Akaingia bafuni kuoga akiwa na huzuni. Usiku aliofikiria
utaishia pazuri ndio umeshaingia dosari! Akaoga na kutoka. Akiwa anarudi
chumbani na taulo dogo alilokuwa amefunga, akamkuta Colins amekaa kitandani
kama anayemsubiria.
Akashituka sana kama Colins. “Samahani sana. Nimeona
kimya ndio nikakaa. Sikujua kama unaoga.” Akasimama na kutoka kabisa hapo.
Kamila akabaki amepigwa na butwaa. Alipofunga mlango ndio akawa kama amegutuka.
Akavaa harakahara
na kumtumia ujumbe. ‘Nimeshavaa tayari. Unaweza rudi kama bado si usumbufu. Vinginevyo
uwe na usiku mwema. Na pole. Najua umekumbushwa mambo mabaya. Pole sana
Colins.’ Akamtumia hivyo akabaki kusubiria majibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mapenzi & Pesa!
Mapambano
Bado Yanaendelea…
0 Comments:
Post a Comment